Na Kauthar Abdalla
WIZARA ya Ushirikiano wa Afrika
Mashariki ya Tanzania imeandaa mkakati wa utekelezaji itifaki ya soko la pamoja
ili kurahisisha na kuondoa changamoto zinazolikabili soko la pamoja la Jumuiya
ya Afrika Mashariki.
Mkakati huo unatoa muelekeo wa
utekelezaji wa soko la pamoja katika ngazi ya kitaifa kwa kuendeleza muundo, mipango
ya kisekta na programu zitakazosaidia ukuaji wa uchumi.
Hayo yalielezwa na Katibu Mkuu
Ofisi ya Rais Ikulu na Utawala Bora, Salum Maulid Salum, katika ufunguzi wa warsha
ya kujadili rasimu ya mkakati wa utekelezaji wa soko la pamoja la Jumuiya ya
Afrika Mashariki, iliyofanyika hoteli ya Zanzibar Beach Resort.
Alisema dhamira ya mkakati huo
ni pamoja na kuziainisha changamoto na fursa za soko la pamoja,kuonesha uwezo na
upungufu wa Watanzania katika kuchangamkia fursa za soko hilo.
Pia alisema dhamira nyengine ni
kuainisha mbinu za kupambana na changamoto, nafasi za taasisi za serikali
katika utekelezaji wa soko hilo na kutoa muongozo wa kimkakati katika
kuchangamkia fursa zilizopo ndani ya soko hilo.
Aidha alisema utekelezaji wa
mkakati huo utasaidia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuongeza fursa za
biashara na uzalishaji,kupanua soko la bidhaa za kilimo na viwanda,kutoa fursa
kwa wawekezaji na kuwasaidia Watanzania kupata ajira.
Hata hivyo, alisema utekelezaji
wa itifaki ya soko hilo umeanza rasmi 2010 leo ilikiwa ni kuimarisha ukuaji wa
uchumi na maendeleo kwa kurahisisha mzunguko huru wa bidhaa, watu, wafanyakazi,
huduma na mitaji ndani ya nchi wanachama.
Mkurugenzi Msaidizi idara biashara,
uwekezaji na sekta za uzalishaji Wizara
ya Ushirikiano Afrika Mashariki, Dk. Abdul Makame, alisema nchi wanachama zinatambua umuhimu wa sekta
binafsi na kuzipa kipaombele.
Alisema itifaki ya soko la
pamoja inaangalia zaidi uchumi huru wa mitaji ya wanachama ili kuhakikisha lengo
linafikiwa.

No comments:
Post a Comment