Na Mwandishi wetu
Chama cha Wanahabari Wanawake
Tanzania (TAMWA) kimevitaka vyombo vya usalama wa taifa, polisi na mahakama
kushirikiana katika kupambana na wahalifu na wote wanaohusika katika kutekeleza
vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu na unyanyasaji wa watoto nchini.
Kauli hiyo imetokana na idadi
ya kesi za ukatili na utekwaji watoto wa kike zinazoripotiwa katika Dawati la
Jinsia na Watoto kwenye vituo vya polisi nchini kuongezeka.
Takwimu zinaonesha kuwa katika
kipindi cha Januari mpaka Septemba, 2014 idadi ya kesi za ukatili wa kijinsia
kwa watoto kwa mkoa wa Dar es Salaam ni 519 hii ni pamoja na mikoa mitatu ya
kipolisi yaani Kinondoni, Temeke na Ilala, ikifuatiwa na Zanzibar 219 (Unguja magharibi
na kusini), Shinyanga 69, Mara 62, Tabora 55, Morogoro 36, Kagera 32 na mkoa wa
Pwani 20.
Katika taarifa za vitendo vya
kikatili kwa watoto matukio yaliyojitokeza ni yale ambayo yanahusisha vitendo
vya ubakaji, ulawiti, mateso, kutelekezwa kwa watoto, utekwaji nyara na kupotea
kwa watoto wa kike.
Taarifa ya TAMWA ilisema hivi
karibuni mkoani wa Dar es Salaam zililipotiwa taarifa za watoto watatu
waliokuwa wakisoma skuli ya msingi Miembeni, Vingunguti waliopotea katika
mazingira ya kutatanisha.
Taarifa hizo zilitolewa na
wananchi waishio maeneo ya Mbezi kwa Msuguri, Mbezi Msigani na kwamba vitendo vyengine
vya kikatili vimeripotiwa katika wilaya ya Kinondoni na Temeke.
TAMWA katika mradi wake wa
Kujenga na Kuimarisha Usawa wa Kijinsia na Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia (GEWE
II) kupitia kituo chake cha Usuluhishi cha (CRC), kwa kipindi cha mwezi Oktoba
mwaka huu kimepokea matukio 16 ya kikatili kwa watoto ambapo yameongezeka
kutoka matukio tisa ya mwezi Septemba.
Aidha, kwa ujumla katika
kipindi cha mwaka 2014 idadi ya matukio hadi sasa yameongezeka kuwa 66
ikilinganishwa na ya mwaka 2013 ambapo taarifa za matukio zilikuwa ni 41.
No comments:
Post a Comment