Na Mwandishi wetu
Aliyekuwa mweka hazina wa Bunge
la SADC, Said Seleman Jaffo, ameutaka uongozi mpya wa Bunge hilo (SADC PF)
kuendeleza mazuri yaliyoanchwa na uongozi unaomaliza muda ikiwa ni pamoja na
kuzingatia matumizi bora ya fedha.
Alisema hayo mjini Victoria
Falls alipokuwa akisomo taarifa ya mapato na matumizi ya bunge hilo kabla ya
kukabidhi madaraka yake kwa uongozi mpya uliochaguliwa Novemba 2 mwaka huu.
Alisema katika kipindi kifupi
cha uongozi wake, aliweka utaratibu madhubuti wa kudhibiti matumizi ya fedha
kwa kuanzisha mfumo maalumu uliosaidia kuhakikisha matumizi ya fedha ndani ya bunge
hilo yanakuwa ya wazi na yanadhibitiwa.
“Mfumo huu umetusaidia kuleta uwajibikaji
ndani ya bunge hili na hasa katika kuhakikisha matumizi ya fedha yote ndani ya bunge
hayaidhinishwi na sekretariati pekee,bali Rais wa Bunge hili, Mweka hazina
pamoja kamati tendaji wanapata taarifa za matumizi ya fedha kupitia mtandao
jambo ambalo si rahisi kwa mtu mmoja kufuja fedha kirahisi kwa kwa kuwa kila
kitu kipo katika mtandao,” alisema.
Alisema katika kipindi cha miezi sita baada ya uanzishwaji wa mfumo huo,
bunge hilo limeweza kufanikiwa kuondoa mapungufu yote yaliyokuwa yakijitokeza
mara kwa mara kama vile upungufu wa fedha na kushindwa kufikia malengo kutokana na ukosefu wa fedha.
“Napenda kuwafahamisha kuwa
hadi kufikia mwezi Machi, 2014, taarifa ya Mkaguzi wa Hesabu za Bunge hili
zilikuwa zinaonesha kuwa tuna upungufu wa fedha, lakini hivi ninavyowaambia
mwezi, kasoro hizo hamna tena bali tuna fedha zaidi ndani ya bajeti yetu ambazo
ni zaidi ya dola 824,000,” alisema.
Akizungumza nje ya ukumbi baada
ya kuwasilisha ripoti hiyo na kumkabidhi mweka hazina mpya mikoba ambaye ni
Gary Nkombo kutoka Zambia, Jaffo alisema uanzishwaji wa mfumo huo sio tu
umelisaida bunge hilo bali umeipa heshima Tanzania kwa kuwa utaratibu huo ni mpya
na umeonesha mafanikio.
Alisema zamani viongozi
walikuwa hawana mawasiliano ya moja kwa moja ya nini kinafanyika kuhusu fedha
za bunge lakini baada ya kuazishwa mfumo huo kila kitu kipo wazi na hakuna anaeweza
kufichwa taarifa inazohusu fedha.
Jaffo alichukua nafasi ya mweka
hazina mwezi Juni mwaka huu baada ya aliyekuwepo, Dk. Titus Kamani, kuchaguliwa
katika baraza la Mawaziri.
No comments:
Post a Comment