Na Mwandishi wetu
JESHI la Polisi Kanda Maalum ya
Dar es Salaam limewaachia huru Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Maendeleo ya
Petroli Tanzania (TPDC), Michael Petro Mwanda na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
shirika hilo, James Andilile, kusubiri
ufafanuzi wa Bunge kutokana na tuhuma zinazowakabili.
Awali, juzi Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Serikali chini ya Mwenyekiti wake, Zitto Kabwe, ilikutana kujadili
suala hilo baada ya viongozi hao kukamatwa.
Kuachiwa kwao kunatokana na
kutokuwepo mlalamikaji aliefungua jalada
na kutoa ufafanuzi kuhusu mashtaka yanayowakabili viongozi hao.
Aidha, maofisa wawili wa sekretarieti ya bunge
waliitwa polisi kutoa ufafanuzi kuhusu kadhia hiyo wakiwemo pia mawakili wa
watuhumiwa.
Pia iligundulika katika sheria
ya haki, kinga na madaraka ya bunge sura ya 296 kifungu 12 (3) kinaonesha
kwamba Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali alitakiwa kwanza
apendekeze kwa Spika wa bunge juu ya jambo lolote aliloliona kama ni kosa.
Na Spika akiridhia kuhusu
tuhuma zozote zilizoletwa kwake na Mwenyekiti wa kamati ya bunge, ndipo anamwandikia
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili suala hilo lipate ufafanuzi wa kisheria ikiwa
ni pamoja na hatua za kisheria zinazostahili kuchukuliwa.
Katika kikao na jopo la
wanasheria iligundulika kwamba katika sheria ya haki, kinga na madaraka ya
bunge, agizo la kukamatwa watu hao lililotolewa na Mwenyekiti wa kamati ya bunge
lakini halikuzingatia taratibu hali iliyosababisha polisi kuwaachia huru.
No comments:
Post a Comment