Habari za Punde

Kutoka baraza la Wawakilishi: Wananchi wana haki ya kuwauliza wawakilishi wao


Na Abdulla Ali na Rahma Khamis - Maelezo

Wananchi wana haki ya kuwauliza Wawakilishi wao kuhusiana na Fedha wanazozipatiwa kutoka Serikalini kwa ajili ya maendeleo ya Majimbo yao.

Hayo ameyaeleza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais Zanzibar Mhe. Mohamed Aboud Mohamed wakati akijibu swali la mwakilishi wa nafasi za wanawake Mhe. Shadya Mohammed Suleiman katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar alipotaka kujua hatua zinazochukuliwa na Serikali kwa wale wote walioshindwa kuwasilisha ripoti zao za fedha za majimbo yao.

Amesema Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanatakiwa kuwasilisha kwa wakati ripoti za matumizi ya fedha za Majimbo yao wanazopatiwa na Serikali ili kuimarisha maendeleo ya wananchi wao.

Aidha amekiri kuwa hadi sasa Majimbo mengi bado hayajafanya marejesho ya matumizi ya fedha za mfuko wa Mwaka wa fedha 2013/2014.

“Hata hivyo napenda kutoa pongezi zangu za dhati kwa waheshimiwa wawakilishi wa majimbo 3 ambayo ni Mtoni, Donge na Chambani pamoja na Kamati zao kwa kufanya marejesho kwa Mwaka 2013/2014 kwa wakati”, ameeleza Waziri Mohamed.

Amesema kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais inawataka waheshimiwa kutekeleza matakwa ya Sheria ili lengo lililokusudiwa kufikiwa kwa nia ya kuwaletea maendeleo wananchi katika maeneo yao.  

Vilevile Waziri huyo amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ina nia njema kwa wananchi wake na ndio maana wawakilishi wao wa majimbo wanapewa kipaombele cha kupatiwa fedha za Mfuko wa Jimbo ili ziwasaidie katika matatizo yao madogomadogo lakini kwa masikitiko makubwa wawakilishi hao wanashindwa kuwasilisha ripoti zao za fedha hizo jambo linalopelekea kurejesha nyuma maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Hata hivyo amefahamisha kuwa serikali imejiwekea kuleta maendeleo katika majimbo yake yote bila ya kuangalia kuwa majimbo hayo yanaongozwa na vyama pinzani au chama tawala.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.