HOTUBA YA NAIBU MAKAMU WA MKUU WA CHUO - UTAFITI, CHUO
KIKUU CHA DAR ES SALAAM, PROF. CUTHBERT Z.
M. KIMAMBO KATIKA SHEREHE ZA UFUNGUZI WA WIKI YA UTAFITI YA CHUO KIKUU CHA DAR
ES SALAAM - TAASISI YA SAYANSI ZA BAHARI, ZANZIBAR, TAREHE 22 APRILI 2015
·
Ndugu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo -Taaluma, Chuo Kikuu cha
Taifa cha Zanzibar, Prof.
.......................................................................;
·
Ndugu Mkurugenzi wa Taasisi ya Sayansi za Bahari, Chuo
Kikuu Dar es Salaam, Dr. Yohana Shaghude;
·
Ndugu Wakurugenzi na Wawakilishi wa Wakurugenzi wa
Idara mbalimbali za Serikali zetu, yaani Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
·
Ndugu Wageni Waalikwa;
·
Wana Taasisi ya Sayansi za Bahari, Chuo Kikuu Dar es
Salaam;
·
Wawakilishi wote wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kutoka
Dar es Salaam mliohudhuria;
·
Wanahabari;
·
Mabibi na Mabwana.
Vile vile nachukua fursa hii kuwapongeza na kuwashukuru wageni wote mliofika hapa kujumuika na wana Taasisi ya Sayansi za Bahari. Kwenu nyote nasema ahsanteni sana kwa kuitikia mwaliko wa wana Taasisi ya Sayansi za Bahari.
Kabla ya kufungua
rasmi sherehe hizi, naomba mniruhusu nieleze kwa muhtasari tu mambo machache kuhusu
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na maadhimisho haya ya Wiki ya Utafiti. Kama
mtakavyokumbuka, siyo muda mrefu uliyopita, Chuo Kikuu cha Dae es Salaam
kiliadhimisha miaka hamsini (50) tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 1961. Baada
ya kufanya tathimini ya mafanikio na changamoto chuo kilizokabiliana nazo
katika kipindi cha miaka hamsini ya kuwepo kwake, kilibuni Dira yake kuelekea miaka
hamsini mingine, yaani Dira ya 2061. Pamoja na mambo mengine muhimu, Dira ya
2061 inakielekeza Chuo kujikita zaidi kwenye utafiti.
Sambamba na Dira ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam 2061,
Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, ambayo ilianza kutekelezwa mwaka 2000, kwa
ajili ya kuongoza harakati za maendeleo ya uchumi na jamii zitakazoiwezesha
Tanzania kufikia hadhi ya nchi zenye kipato cha kati na kuondokana na umaskini
uliokithiri ifikapo mwaka 2025. Aidha dira hii imekuwa na malengo makuu yakiwemo haya mawili yafuatayo:
(i) Kuwa na jamii iliyoelimika vyema na inayojifunza na(ii) Kujenga uchumi imara unaoweza kukabiliana na ushindani kutoka nchi nyingine.
Ndugu Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Kwa kutambua umuhimu wa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi, programu na mikakati ya maendeleo kuelekea 2025, Taifa limejiwekea mkakati mpya wa Matokeo Makubwa Sasa uliozinduliwa na Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, mnamo Februari 2013. Moja ya sekta sita muhimu zilizoteuliwa kwa utekelezaji wa mkakati huo, katika awamu ya kwanza ilikuwa ni sekta ya elimu. Hii ni kwa kuzingatia ukweli kwamba misingi ya ukuaji wa uchumi wa nchi yoyote ni pamoja na kuimarisha viwango vya elimu, ujuzi, sayansi, technolojia uvumbuzi na ubunifu.
Kwa kuzingatia mategemeo haya makubwa ya kitaifa, Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam kimeweka msititizo wa pekee wa kukuza utafiti na ubunifu. Mojawapo ya
mikakati ya kufanikisha azima hiyo ni kusambaza matokeo ya utafiti ili yaweze
kutumika katika kuleta maendeleo kwenye sekta husika. Hivyo basi, Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, kimepanga kuwa
na Wiki ya Utafiti, kwa vitengo vyake vyote ambayo itakuwa inafanyika mara moja
kila mwaka kwa ajili ya kuimarisha juhudi za utafiti unaoendelea kwa njia ya
kuyatangaza na kuyaonesha kwa uma, mafanikio ya utafiti yanayotokana miradi ya
utafiti ya wanafunzi wetu na wanataaluma mabingwa na kazi mbalimbali za
ubunifu. Kwa lengo hili, wanafunzi na wanataaluma wataonyesha machapisho,
watatoa mihadhara na kuonyesha matokeo mbalimbali ya utafiti. Hii ni fursa ya pekee
ya kuwawezesha wanajumuia ya Chuo Kikuu Dar es Salaam kukutana na wadau
mbalimbali, wakiwemo walengwa wa kazi hizo za utafiti kwa lengo la kubalidilishana
maarifa katika kubuni njia mbalimbali za kukabiliana na changamoto za maendeleo
ya nchi yetu na dunia kwa jumla. Matukio muhimu katika wiki ya utafiti ni pamoja
na kutolewa kwa mihadhara na kufanya maonyesho ya matokeo ya utafiti na
ugunduzi.
Ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati huu, wiki ya utafiti ya Chuo
Kikuu Dar Salaam, Taasisi ya Sayansi za Bahari, pamoja na sherehe hii ya ufunguzi
huu, itakuwa na mihadhara itakayotolewa katika siku ya kwanza ambayo ni leo na
maonyesho ya kazi za utafiti
yataonyeshwa siku inayofuata, yaani kesho. Ninawashukuru wadau
mbalimbali walioitikia mwito wa kuja ili kushirikiana na wana Taasisi ya
Sayansi za Bahari ya Chuo Kikuu Dar es Salaam, hapa Zanzibar.
Ndugu Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Jambo la pili linahusiana na azima ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ya
kuendelea kuwa Chuo cha kutegemewa kitaifa na kimataifa katika kutoa wataalamu
na matokeo ya utafiti yatakayokwamua uzalishaji wa sekta mbalimbali za uchumi wa Tanzania. Ili kutekeleza azima hiyo,
Chuo Kikuu Dar es Salaam, kimeamua kurudisha tena taaluma ilizozipoteza baada
ya kuzilea na hatimaye kuzaa vyuo vikuu vinavyojitegemea vya kilimo, sayansi ya
tiba na taaluma za ardhi na usanifu majengo. Aidha, Chuo Kikuu Dar es Salaam
kimeweka msisitizo wa kuziendeleza ipasavyo sayansi na teknolojia za bahari.
Sote tunakumbuka kwamba Taasisi hii imeanzishwa mara baada ya nchi yetu
kugundua na kuthibitisha uwepo wa gesi asilia na uwezekano wa kuwepo mafuta ya
petroli katika maeneo ya bahari ya Tanzania katika miaka ya 1970. Hata hivyo, nchi
yetu bado haina uwezo wa kutosha katika kuendeleza taaluma za ugunduzi wa mafuta ya petroli na uchimbaji
wa gesi asilia kutoka baharini na namna za kudhibiti uchafuzi wa mazingira utokanao
na shughuli za ugunduzi wa rasilimali hizo,
uchimbaji na usafirishaji wake katika maeneo ya mwambao wa Tanzania kwa
ajili ya maendeleo ya jamii.
Pamoja na tafiti zinazohusiana na rasilimali za petroli na gesi
asilia, tafiti za kibunifu nyingine zinazotakiwa kupewa kipaumbele ni pamoja na
tafiti zinazolenga katika uvunaji wa
nishati endelevu kutoka Baharini; nishati kama upepo, mawimbi, kujaa na
kupwa kwa maji ya bahari, joto la maji ya bahari, uvuvi endelevu, uchakataji wa
mazao mbalimbali ya bahari kwa ajili ya kuyaongezea thamani ili kukidhi soko la
kitaifa na kimataifa, utafutaji na uchimbaji wa vito vya thamani na madini
kutoka baharini bila kuathiri mazingira, utalii endelevu baharini na maeneo ya
mwambao, ukulima/ufugaji wa samaki wa mabwawa na matundu (cage culture) kwa
ajili ya kupunguza “uwindaji wa samaki”, teknolojia ya mawasiliano baharini,
Sera za uchumi na biashara ya mazao ya bahari: uvuvi, ufugaji, biashara na
masoko, utalii, nishati n.k.
Maeneo niliyoyataja hapo juu ni maeneo ambayo ninapendekeza kuwa Taasisi ya Sayansi za Bahari ya Chuo Kikuu Dar
es Salaam iweze kuyapa umuhimu mkubwa kwa siku zijazo, hasa inapofikiria
kupanua shughuli zake za utafiti na kufundisha kwa ajili ya kutoa mchango
mkubwa zaidi kwa Taifa la Tanzania na wananchi wanaoishi visiwani na kwenye
maeneo ya mwambao wa Tanzania.
Ndugu Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Nimejulishwa kwamba mwaka huu maonyesho yatahusu nyanja tano
ambazo ni:1. Ufugaji wa samaki,
2. Kilimo cha lulu na utengenezaji wa mapambo,
3. Ukulima wa mwani na uongezaji wa thamani wa mazao yake,
4. Matumizi ya teknolojia ya habari katika kusamabaza matokeo ya utafiti na
5. Miundombinu ya utafiti na machapisho.
Pia nimejulishwa kwamba moja ya machapisho muhimu ni
Kitabu kipya juu ya “Mabadiliko ya Fukwe
katika mwambao wa Tanzania na Kenya: Kitabu kwa ajili ya kutathmini mabadiliko
ya mwambao na kutengeneza mikakati ya kudhibiti mabadiliko ya mwambao (Shoreline changes in Tanzania and Kenya: A
manual for assessment and design for
mitigation strategies) ambacho ninafurahi kupewa heshima ya kukizindua hivi
punde.
Ni matumaini yangu kwamba, katika wiki ya utafiti ya mwakani,
Taasisi itatuonesha maendeleo zaidi ya utafiti, ubunifu, na teknolojia katika nyanja
nyingine nyingi zinazogusa maisha ya watu na kuimarisha uzalishaji wa sekta ya
bahari.
Baada ya kusema haya machache, ninayo heshima kubwa kutangaza
rasmi kwamba Wiki ya Utafiti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika Taasisi ya
Sayansi za Bahari imefunguliwa rasmi. Ninawatakieni mafanikio mema.
Asanteni sana
kwa kunisikiliza.
** Mara tu baada ya hotuba ya Ufunguzi litafuatia tendo la kuzindua Kitabu
Kipya
No comments:
Post a Comment