Habari za Punde

Hotuba ya Mkurugenzi Taasisi ya Sayansi za Bahari katika ufunguzi wa wiki ya utafiti

 HOTUBA YA MKURUGENZI TAASISI YA SAYANSI ZA BAHARI CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM, DR. Y. W. SHAGHUDE, SHEREHE ZA UFUNGUZI WA WIKI YA UTAFITI YA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM - TAASISI YA SAYANSI ZA BAHARI, ZANZIBAR, TAREHE 22 APRIL 2015
Dk. Yohana .W.Shaghude
 Ndugu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Utafiti, Chuo Kikuu cha Dar es Saslaam, Prof. C. Z. Kimambo,

Ndugu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Utafiti, Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar, Prof. H. Mwevura,

Ndugu Wakurugenzi na Wawakilishi wa Wakurugenzi wa Idara mbalimbali za Serikali zetu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar and Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Ndugu Wageni Waalikwa,

Wana Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wote waliohudhuria kutoka Dar es Salaam,

Wana Taasisi ya Sayansi za Bahari,

Mabibi na Mabwana,

Asalaam Alaykum


Awali ya yote nachukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa fursa hii ya kukutana kwa ajili ya kusherehekea wiki hii ya Utafiti Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hapa katika Taasisi ya Sayansi za Bahari.

Pili kwa niaba ya jamii yote ya Taasisi ya Sayansi za Bahari  kwa moyo wa dhati kabisa napenda kukushukuru Mheshimiwa Naibu Makamu wa Mkuu wa Chuo Utafiti wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mgeni Wetu Rasmi, kwa kukubali kwako kuja kuzindua rasmi sherehe hizi za Wiki ya Utafiti ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Taasisi ya Sayansi za Bahari, tena kwa kudharurishwa. Kuja kwako hapa wewe mwenyewe binafsi kunaonyesha umuhimu mkubwa unaoyapa masuala ya utafiti ya mambo ya bahari na usambazaji wa matokeo yake kwa wadau mbalimbali. Aidha napenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha wageni wote waalikwa pamoja na wananchi wote waliofika hapa kushiriki ufunguzi wake na hatimaye mihadhara na majadiliano mbalimbali na hapo kesho maonyesho mbalimbali.


Mheshimiwa mgeni rasmi na wageni waalikwa, baada ya ukaribisho huo,  napenda kuchukua fursa hii kutoa historia fupi ya Taasisi ya Sayansi za Bahari. Taasisi hii ni moja ya Taasisi nne za Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Taasisi hii ilianzishwa tarehe 17 Oktober 1978 kutokana na uamuzi wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wa kuanzisha taasisi ambayo ingeshughulikia sayansi na elimu ya matumizi endelevu ya raslimali za bahari. Taasisi hii wakati wa kuanzishwa kwake ilipewa majukumu makuu manne:


1)      Kufanya utafiti katika fani zote za sayansi za bahari,

2)      Kutoa taaluma kwa wanafunzi wa shahada za uzamili (tukimaanisha shahada ya uzamivu na umahiri/falsafa) na baadaye kutoa elimu ya shahada ya kwanza kulingana na mahitaji ya Taifa.

3)      Kutoa ushauri wa kitaaluma katika masuala ya bahari, na

4)      Kutoa ushauri wa njia bora za matumizi endelevu ya maliasili za baharini.


Mheshimiwa mgeni rasmi na wageni waalikwa, Taasisi ilipoanzishwa ilirithi majengo tuliyomo, vifaa na vyombo vya kilichokuwa kitengo cha Afrika Mashariki cha Utafiti na Uvuvi wa Bahari (East African Marine Fisheries Research Organisation, EAMFRO) kilichokuwa chini ya iliyokuwa Jumuia ya Afrika Mashariki iliyovunjika mwaka 1977. Kwa kuzingatia majumu makubwa niliyokwisha yataja ya Taasisi mpya, ni wazi majengo na eneo hili la Mizingani visingekidhi mahitaji ya kufanya utafiti, kufundisha pamoja na mipango ya upanuzi kila ulipohitajika. Kutokana na upungufu huo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kiliomba kupatiwa eneo linguine kubwa linaloendana na upeo wa majukumu yake, na hivyo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilitoa ekari 200 maeneo ya Mkokotoni mnamo mwaka 1978 ili kujenga maabara, madarasa, ofisi na huduma nyingine kwa ajili wa wafanyakazi na wanafunzi wake.

Hata hivyo, kutokana na sababu mbali mbali hasa za kiuchumi, eneo hilo halikuweza kuendelezwa kwa wakati kama ilivyokusudiwa na kwa hiyo wananchi wa sehemu husika waliendelea kuimarish makaazi, wengine shughuli za kilimo na maendeleo mengine. Kwa kuepusha athari za kuhamisha watu na mali katika eneo hilo, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iliona ni busara kutoa eneo la ekari 125 maeneo ya  Buyu mwaka 2003 kwa ajili ya shughuli za Taasisi kama ilivyokusudiwa mwanzo. Jiwe la Msingi liliwekwa tarehe 11 Januari 2004 na ujenzi ukaanza.  Awamu ya kwanza ya ujenzi uliohusisha jengo la utawala uliokadiriwa kugharimu Shilingi 6,291,056,108.10 ulikabidhiwa kwa kampuni ya China Railway (M/S China Railways Jianchang Engineering Co. Ltd.) tarehe 3 Machi, 2006. Serikali ya Jamhuri ya Muungano ilijitolea kutoa pesa kwa ajili ya ujenzi uliodhamiriwa kuchukua wiki 73. Hata hivyo kutokana na pesa za ujenzi kutopatikana kwa wakati, ujenzi ulisimama Desemba 2006 na kurejea tena 2011 wakati gharama za ujenzi zikiwa zimepanda hadi kufikia bilioni 10.4. Hivyo ujenzi wa jengo la utawala uliazimiwa kufanywa kwa awamu tano (A-E), na awamu mbilin za kwanza (A na B) umegharimu shilingi bilioni 4.8.


Mheshimiwa mgeni rasmi na wageni waalikwa, kimsingi ujenzi wa sehemu A na B umekamilika. Hata hivyo, ikumbukwe kwamba gharama iliyotajwa ya ujenzi wa awamu A na B haikujumuisha samani, mfumo wa kupoza hewa, uzio ambao unahitajika kwa ajili ya  kuimarisha ulinzi wa eneo na ujenzi wa barabara. Mikakati inayoendelea ya Uongozi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam ya kufabikisha upatikanaji wa samani kwa sehemu iliyokamilika ya mradi wa Buyu ni mikakati ambayo inapongezwa na wana jumuia wa Taasisi ya Sayansi za Bahari kwa sababu ndoto yetu ya muda mrefu ya kukaa katika majengo yanafanana na upeo wa majukumu tuliyokabidhiwa na Taifa karibuni zitatimia . Kwa kuwa ujenzi wa maabara umo katika awamu ya C-E, mpango uliopo wa kuhamia Buyu utailazimu IMS kuendelea kutumia majengo yaliyopo hapa ili kupata huduma hiyo. Huduma nyingine zitakazokosekana Buyu ni pamoja na:

·         mabweni ya wanafunzi,

·         kantini

·         kituo cha afya

·         viwanja vya michezo

·         aquarium

·         nyumba za wafanyakazi n.k.


Mheshimiwa mgeni rasmi na wageni waalikwa, pamoja na vikwazo mbalimbali vya ujenzi wa makao makuu yake, Taasisi imepata mafanikio makubwa katika kujipatia raslimali watu na miundombinu ya utafiti. Taasisi ilianza 1978 ikiwa na wanataaluma 6 tu na hivi leo tuna fahari ya kusema tunao wanataluma 14 wote wakiwa wamehitimu na kupata shahada ya udaktari wa falsafa katika sayansi za bahari. Pia Taasisi inao Wanasayansi wa Maabara (Laboratory Scientists) wawili, wote wenye shahada ya udaktari na falsafa.  Hata hivyo Taasisi imepoteza wanataluma waliokwisha someshwa kumi na moja ambao wako kwenye vyuo vikuu vipya (3), vitengo vingine vya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (3), taasisi za kimataifa (1) na waliostaafu (4). Kwa kuwa hao wote wameondoka pasipo kupata mbadala ni dhahiri kwamba Taasisi ina kiu kubwa ya kuajiri. Kiu hii ni kubwa zaidi kwa kuzingatia kwamba wanataluma wake 2 wako kwa mkataba na watano watastaafu ndani ya kipindi cha  miaka minne ijayo. Wakati huo huo, Taasisi imeazimia kupanuka na kuanzisha idara tano tofauti ili kukidhi mahitaji mapya kitaifa. Pendekezo juu ya uanzishwaji wa idara hizo linaandaliwa ili kuwasilishwa rasmi kwa mamlaka ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.


Mheshimiwa mgeni rasmi na wageni waalikwa, kwa ujumla Taasisi hii ya Sayansi za Bahari inaendelea kutoa mchango mkubwa kitaifa na kimataifa. Taasisi inashiriki ipasavyo katika kutoa ushauri wa kisera kama vile uanzishwaji hifadhi, kutoa tathmini za maliasili hasa mikoko na matumbawe, namna ya kudhibiti mabadiliko ya maeneo ya mwambao  na ushauri wa matumizi endelevu wa rasilmali za bahari na maeneo ya mwambao. Taasisi pia imesimamia ukuaji wa kilimo cha mwani katika maeneo ya pwani hasa Unguja, Pemba na Mtwara na uchakataji wa zao hilo ili kuongeza matumizi na thamani yake. Hivi sasa Taasisi inaimarisha shughuli za ufugaji samaki na inatoa taaluma za uvuvi bora na utalii endelevu wa baharini unaohusiana na utunzaji wa pomboo. Pia Taasisi inaimarisha ukulima wa chaza kwa ajili ya uzalisaji lulu na matengenezo ya mapambo, shughuli inayokuwa kwa kasi katika pwani zetu. Senta za utafiti, ubunifu na uendelezaji wa ufugaji wa samaki na chaza zitajengwa katika eneo jpya la Taasisi lililoko Buyu na kituo kingine cha Taasisi kilichopo kule Pangani, katika Mkoa wa Tanga.


Kwa upande wa utoaji elimu, wanataluma wa Taasisi wanasimamia wanafunzi wa shahada za uzamili na falsafa kutoka vyuo vyetu nchini na vyuo vya nje na vilevile Taasisi inatoa nyenzo za kufanyia kazi baharini na katika maabara. Pia kwa kupitia ufadhili wa mashirika ya nchi mbalimbali kama vile Sida  kutoka nchi ya Sweden na CIDA (Cananda) na WIORISE, Taasisi imekuwa ikitoa ufadhili kwa masomo ya uzamili (yaani uzamivu na umahiri) tangu mwaka 1992. Kupitia mpango huo, watanzania 25 waliweza kuhitimu kiwango cha umahiri (Udaktari wa falsafa (PhD)) na wengine 56 kwa kiwango  cha uzamivu (MSc). Asilimia 80% ya hao wote wapo katika vyuo vyetu vikuu na waliobaki wako katika taasisi za Serikali zinazojishughulisha na maendeleo ya uvuvi na utunzanji wa mazingira. Hivi sasa Taasisi inatoa mafunzo kwa wanataaluma kutoka nchi nyingine za Afrika zilizopo magharibi mwa Bahari ya Hindi kama vile Kenya, Mozambique, Mauritius kulingana na mahitaji yao. Pia Taasisi inatoa  mafunzo ya muda mfupi kwa wanafunzi wa nchi mbalimbali za Marekani, Uholanzi, Sweden na Norway. Pia wanataluma wetu huwa wanakwenda kufundisha kwa muda mfupi katika vyuo vikuu vya nchi jirani zikiwemo Mozambique, Namibia, Mauritius, Uganda na Ujerumani.


Taasisi pia kupitia kitengo chake cha elimu ya mazingira ya bahari imeshatoa kanda za video zaidi ya 40 amabazo zinaonyesha hali halisi ya mazingira yetu na njia mbalimbali za kuyahifadhi. Aidha watafiti wameandika matokeo ya utafiti wao katika majarida mbalimbali ya hapa nchini na ya kimataifa na pia kutunga vitabu mbalimbali vinavyohusiana na mazingira ya bahari. Kimoja cha vitabu hivyo tunakuomba ukizindue leo. Taasisi pia ni kituo cha taifa cha Takwimu za Bahari ikifadhiliwa na IOC ya UNESCO.


Mheshimiwa mgeni rasmi na wageni waalikwa, kukamilika kwa ujenzi wa Tasisi huko Buyu kutatoa nafasi kwa ajili ya shughuli za utafiti na ufundishaji wa fani zilizopo na uanzishwaji wa fani mpya kama nilivyokwisha dokeza. Kwa mfano uendelezaji wa uvuvi wa bahari kuu, uendelezaji wa vyanzo mbalimbali vya nishati, ufugaji wa samaki katika bahari ya wazi, ni baadhi tu ya maeneo yanayohitaji utafiti na ufundishaji ili Taifa letu lipate kunufaika zaidi za maliasili zetu. Ili kufanikisha haya Taasisi bado inaendelea kuwasiliana na vyombo mbalimbali kitaifa na kimataifa ili kupata meli ya utafiti.

Kwa kumalizia napenda kutoa shukrani zetu za dhati kwanza, kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ikiongozwa na Mhe. Dr. Ali Mohammed Shein kwa kutupa misaada mbalimbali tunayohitaji ili kuendeleza utafiti wetu na kutoa elimu. Tunatoa shukrani za pekee kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kutupatia ardhi kwa ujenzi wa Taasisi pale Buyu. Aidha tunazishukuru Wizara za Elimu za Serikali zote mbili, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  kwa kufanikisha ujenzi wa Taasisi  ya Sayansi za Bahari katika eneo la Buyu. Tunapenda kuwashukuru wafadhili mbalimbali wakiwemo Sida (Sweden), CIDA ya Canada, USAID, WWF, UNEP, UNESCO, IUCN, WIOMSA kwa kufanikisha miradi mbalimbali ya utafiti katika Taasisi yetu. Tunawashukuru majirani zetu wote, wadau wa utafiti hasa akina mama wa vikundi mbalimbali hapa Unguja, Pemba, Mtwara kwa mashirikiano mema. Kwa wote tunasema ahsanteni sana na tuzidi kushirikiana.


Ahsanteni kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.