![]() |
TUME
YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Kitalu
Na. 8, Mtaa wa Luthuli
S.L.P
2643, DAR ES SALAAM
Simu:
+255 22 2135747/8; 2137125; 2135222
Faksi:
+255 22 2111281
Barua
Pepe: chragg@chragg.go.tz
Tovuti:
www.chragg.go.tz
|
Septemba 13, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tamko la kulaani mauaji na matukio
ya uvunjifu wa sheria wakati wa kampeni za uchaguzi wa Rais, Wabunge na
Madiwani huko Tarime
TUME ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesikitishwa sana na vurugu za ushabiki wa
kisiasa zilizoanza kujitokeza wakati wa mikutano ya kampeni za vyama vya siasa
katika sehemu kadhaa nchini.
Matukio ya
uvunjifu wa amani na sheria za nchi ambayo yametangazwa na vyombo vya habari
hivi karibuni, ni tofauti na jinsi mikutano mikubwa iliyofanyika kwa amani siku
za mwanzo za uzinduzi wa kampeni za vyama na wagombea urais wa vyama vya
siasa.
Kwa mujibu wa
taarifa za vyombo vya habari inaonyesha kwamba kuna ongezeko la vurugu
zinazotokea kutokana na wafuasi wa vyama
vya siasa kuingiliana katika mikutano ya kampeni na kusababisha vurugu, ama wafuasi
hao kupigana.
Tume imepata
taarifa ya kutokea vurugu kama hizo ambazo zimesababisha kifo cha mtu mmoja na
watu wengine kujeruhiwa kwa kukatwa mapanga, uharibifu wa gari la mgombea
ubunge wa jimbo la Tarime mjini, Bi. Esther Matiko. Vurugu hizo zilizowahusisha
wafuasi wa
vyama vya CCM
na CHADEMA zilitokea kijiji cha Mangucha, jimbo la Tarime Vijijini, Septemba
10, 2015.
Pia Tume
imesikitishwa na taarifa za vyombo vya habari zinazoelezea vurugu zilizofanyika
hivi karibuni wakati wa kampeni zinazoendelea katika baadhi ya maeneo nchini,
yakiwemo majimbo ya uchaguzi ya Kyela, Bunda mjini, Dodoma mjini, Dar es Salaam
na Zanzibar.
Matukio haya
yote ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, na yanaenda kinyume na Maadili ya
Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2015 yaliyotiwa saini na vyama
vya siasa, ambayo yanavitaka vyama vya siasa na wahusika wote kukataa na
kulaani vitendo vya vurugu, fujo, chuki, mafarakano, matumizi ya lugha za
matusi na kejeli na kubeba silaha yoyote inayoweza kumdhuru mtu.
Tume inalitaka
Jeshi la Polisi kuhakikisha linatoa ulinzi wakati wa mikusanyiko yote wakati wa
kampeni za uchaguzi mkuu.
Kila ilipopata
fursa ya kukumbusha umuhimu wa amani wakati wa uchaguzi, THBUB imefanya hivyo.
Tume inapenda tena kuchukua fursa hii kuwakumbusha viongozi wa vyama vya siasa
kuwaasa wanachama na wafuasi wao kuzingatia amani wakati wote wa mchakato wa
kampeni na hadi uchaguzi tarehe 25 Oktoba 2015. Aidha, Tume inawakumbusha
viongozi wa vyama vya siasa kuacha kabisa kauli zinazoweza kuchochea wafuasi
wao kufanya fujo na vitendo vya uvunjifu wa amani.
Kutokana na
hali hiyo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inalaani vikali vitendo
hivyo na kutoa rai kama ifuatavyo:
1. Vyama
vya Siasa, wagombea na wafuasi wao wazingatie Maadili ya Uchaguzi wa Rais,
Wabunge na Madiwani ya Mwaka 2015. Aidha, viongozi wa vyama vya Siasa
wawahamasishe na kuwasisitiza wafuasi wao kutanguliza uzalendo zaidi, kuwa na
uvumilivu wa kisiasa na
umuhimu wa kuilinda amani hasa kipindi hiki cha kampeni na kuelekea upigaji
kura.
2. Wanasiasa
wafanye kampeni za kistaarabu na kujiepusha na matamshi au vitendo
vitakavyoashiria uvunjifu wa amani vinavyoweza kuwatia hofu wananchi hata
washindwe kujitokeza kwenye mikutano ya kampeni.
3. Wananchi
na wafuasi wa vyama kwa ujumla waache jazba na tabia ya kujichukulia sheria
mkononi hali inayohatarisha amani na utulivu wa nchi.
4. Wananchi
watambue kuwa wanao wajibu wa kuheshimu uhuru na haki za watu wengine, ikiwemo
haki za kuishi na uhuru wa kujumuika na kushiriki katika masuala ya kisiasa.
5. Jeshi
la Polisi lifanye uchunguzi wa kina na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria wote
watakaobainika kuwa walihusika na mauaji, au uharibifu wa mali na vurugu
zilizotokea maeneo mbalimbali.
6. Mwisho,
Tume inatoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi katika
kuhakikisha wale wote waliohusika na matukio ya mauaji, vurugu na uharibifu wa
mali wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo husika ili sheria ichukue mkondo
wake.
Imetolewa
na:

TUME YA HAKI ZA
BINADAMU NA UTAWALA BORA
Septemba
13, 2015
No comments:
Post a Comment