Habari za Punde

Serikali kuwachukulia hatua waliojenga nyumba bila ya vibali

Na Othman Khamis Ame, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali italazimika kuchukuwa maamuzi magumu katika kukabiliana na watu waliojenga nyumba bila ya vibali wala kuzingatia taratibu za Taasisi za Ardhi hasa maeneo yaliyowekwa kwa ajili ya miradi ya Kijamii,vianzio vya Maji pamoja na mitaro ya kupitishia maji ya mvua.

Alisema hatua inaandaliwa kuchukuliwa na Serikali kupitia Taasisi husika chini ya usimamizi wa Viongozi watakaosimamia taasisi zao katika azma ya kutekeleza agizo la Rais wa Zanzibar alilolitoa wakati akilizindua Baraza la Wawakilishi Zanzibar juu ya kukabiliana na migogoro ya ardhi ndani ya kipindi cha miaka mitano ijayo.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Masheha pamoja na watendaji wa Taasisi zote zinazohusika na masuala ya Ardhi wa Wilaya zote mbili za Magharibi “A” na “ B” mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Makamu Makao Makuu ya 
Kikosi cha Valantia { KVZ } Mtoni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Alisema Serikali imebaini kwamba uuzaji holela wa maeneo ya ardhi unaofanywa na baadhi ya watu wakiwemo pia masheha na hata watendaji wa Idara ardhi ni chanzo cha ujenzi mbovu wa makaazi ya watu usiozingatia Mipango Miji na hatimae kusababisha matatizo ya kutowafikia wananchi katika kupatiwa huduma muhimu za kijamii.

Balozi Seif alieleza kwamba Taifa lazima lirejee katika heshima yake ya kuwa na mipango bora ya ardhi itakayozingatia mazingira kwa lengo la kuondosha migogoro ya ardhi inayoonekana kuongezeka kila siku hasa katika Wilaya za Magharibi “A” na “ B”.


Alitolea mfano eneo la chuini lililotengwa maalum na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa Afisi zake, licha ya tangazo lililobandikwa likitoa indhari ya kutofanyika ujenzi wa aina yoyote lakini baadhi ya watu waliamua kuvamia kwa ujenzi wa nyumba za kudumu na viongozi wa eneo hilo wakishuhudia kutendeka kwa mambo hayo.

Alisema kuachiliwa kuendelea kwa tabia hii inaweza kufika wakati hata ikakosekana maeneo ya kilimo cha mboga mboga kwenye Wilaya hizo kama Wilaya ya Mjini ilivyokosa maeneo ya wazi kwa ajili ya shughuli za Jamii.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa agizo kwa Masheha wote wa Wilaya mbili za Magharibi “A” na “ B” kuanza kufanya uhakiki wa kuziorodhesha nyumba zote zilizojengwa bila ya kibali na katika maeneo yasiyostahiki.

“ Tunakusudia kubomoa majengo yote yaliyojengwa bila ya kibali na kwenye maeneo ya njia za maji ikiwa ni mwanzo wa maamuzi magumu yatakayochukuliwa na Serikali ”. Alisema Balozi Seif.

Alisema sambamba na hilo kuanzia sasa hakuna sheha atakayepaswa wala kuruhusiwa kutoa, kuuza au kukata viwanja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba jukumu ambalo liko chini ya dhama ya Wizara ya Ardhi, Maji Nishati na Mazingira.

Mapema Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara 
Maalum za SMZ Mh. Haji Omar Kheir alisema katika kukabiliana na migogoro ya Ardhi Sheha ye yote atakayebainika kuhusika na suala la ardhi  itakuwa ndio kibali chake cha kuachia madaraka.

Mh. Haji alisema ameamua yeye pamoja na Uongozi wa Wizara yake kuanza ziara za kukagua maeneo mbali mbali Mjini na Vijijini ili kubaini uzembe na udhaifu uliofanywa na baadhi ya viongozi hao na atakapobaini uzembe wowote atalazimika kuchukua hatua zinazofaa hapo hapo.

Alisema kazi iliyo mbele ya Viongozi hao kwa sasa ni kuhakikisha  kwamba agizo la Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohammed Shein linaanza kuchukuliwa hatua mara moja.

Naye kwa upande wake Waziri wa Ardhi, Maji,Nishati na Mazingira Mh. Salama Aboud Talib aliwaahidi Masheha na Viongozi hao wa Wilaya za Magharibi “A” na “ B ” kwamba atasimamia  kwa uadilifu jukumu alilokabidhiwa ili kuona haki ya kila raia wa Nchi hii inapatikana.

Waziri Salama alisema wapo baadhi ya watendaji wakiwemo pia wa Taasisi zilizo chini ya Wizara yake ambao wamekuwa wakisababisha kuibuka kwa migogoro ya ardhi katika maeneo mengi kwa kuendekeza tama na kukosa uadilifu.

Mh. Salama Aboud aliwahakikishia masheha na Viongozi hao wa Wilaya za Magharibi  “ A ” na “ B ”kwamba Maamuzi magumu yanayopaswa kuchukuliwa na Serikali Kuu dhidi ya wanaosababisha migogoro hiyo atakuwa wa kwanza kuanza  kuyatekeleza.

Mkutano huo umewashirikisha Masheha wote wa Wilaya za Magharibi “A” na “B”, Wakuu wa Wilaya hizo, Watendaji wa Ardhi, Mazingira, na Mkoa wa Mjini Magharibi akiwemo pia Meya wa Manispaa ya Zanzibar Mstahiki Khatib Abdulrahman Khatib.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.