Habari za Punde

Shirika la Afya Duniani (WHO) lakabidhi msaada wa dawa na vifaa dhidi ya maradhi ya kipindupindu

Na Othman Khamsi Ame, OMPR

Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzaia Dkt. Rufaro Chatora alisema uwezo wa jamii kwa kushirikiana na Serikali katika kukabiliana na maradhi ya kipindu pindu unawezekana na ni rahisi iwapo kila Mwananchi atachukua juhudi katika kudumisha mazingira yaliyomzunguuka katika eneo lake.

Alisema tahadhari ya athari yoyote inapaswa kuchukuliwa  mapema katika kukinga badala ya kuendeleza tabia iliyozoeleka ya kusubiri kutibu inayochukuwa wakati mrefu na gharama kubwa.
Mwakilishi huyo wa Shirika la Afya Duniani { WHO } Dr. Rufaro 

Chatora alieleza hayo wakati akikabidhi msaada wa dawa na vifaa mbali mbali vilivyotolewa na Shirika hilo kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Vuga Mjini Zanzibar.

Msaada huo wa Dawa na Vifaa uliogharimu jumla ya shilingi Milioni 39,463,313/- umelenga kuhudumia wagonjwa walioathirika na maradhi ya kipindu pindu katika kambi mbali mbali hapa Zanzibar yaliyoanza tokea mwezi septemba kwamba 2015.

Dr. Rufaro alisema juhudi zaidi zinapaswa kuchukuliwa baina ya Viongozi wa Serikali kwa kushirikiana na Wananchi katika kuweka mikakati itakayosaidia mapambano ya kukabiliana na maradhi  ya Kipindupindu yanayoonekana kuwa tishio kwa maisha ya jamii.

Aliahidi kwamba Shirika la Afya Duniani kwa kushirkiana na lile la kuhudumia Watoto { Unicef } litaendelea kuunga mkono jitihada za Serikali pamoja na Wananchi wa Zanzibar kwenye mapambano yao ya kukabiliana na maradhi mbali mbali yanayowasumbua Wananchi.

Akipokea msaada na vifaa hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya itaendelea kutoa elimu kwa umma jinsi ya namna ya wananchi wanavyoweza kujiepusha na maradhi tofauti ikiwemo Kipindu pindu.

Balozi Seif alisema maradhi ya kuambukiza kama  Kipindu pindu ni hatari na chanzo chake yanayotokana na mazingira mabovu ya makaazi pamoja na udhibiti  wa vyakula usiozingatia kanuni za afya.

Alisema uwezo wa kudhibiti maradhi ya kipindu pindu upo  hapa Nchini kama Zanzibar ilivyofanikiwa katika kudhibiti maradhi ya malaria yaliyopungua kabisa na kufikia hadi asilimia 0.35%.


Balozi Seif aliyapongeza Mashirika ya Kimataifa ya Afya { WHO } na lile la kuhudumia Watoto { UNICEF } kwa juhudi za mashirika hayo katika kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika Sekta ya Afya.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliendelea na ziara yake ya kukagua sehemu mbali mbali zilizoathirika miundombinu yake kutokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia Jumapili iliyopita.

Ziara hiyo ilianzia eneo la Karakana ambapo alipata kujionea hali halisi ya athari hiyo ambapo Mkurugenzi wa Kamisheni ya Maafa Zanzibar Nd. Ali Juma Hamad alisema eneo hilo linaweza kupata salama ya athari ya mafuriko baada ya kumalizika kwa mtaro mkubwa unaoendelea kujengwa katika eneo hilo.

Baadaye Balozi Seif aliangalia Bara bara inayotoka Mwanakwerekwe kuelekea Fuoni ambayo kwa saba bado haijaweza kutoa huduma kutokana na kufurika kwa maji katika ziwa liliopo pembezoni mwa Soko la Mwanakwerekwe. 

Mkuu wa Wilaya ya Magharibi “B” Nd. Ayoub Mohammed Mahmoud alisema Uongozi wa Wilaya hiyo kwa kushirikiana na Taasisi zinazohusika zinajiandaa kuanza usafi baada ya kupunguwa kwa kina cha maji kwenye bara  bara hiyo ili kuona athari zitazojitokeza na baadae iendelea kutoa huduma ya usafiri kama kawaida.

Nd. Ayoub hata hiyo alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Wilaya zote mbili za Magharibi “A” na “B” bado hazijawa na miundombinu ya mitaro ya kupitishia maji ya mvua inayoweza kusaidia wakati wa msimu wa masika.

Akikagua mafuriko katika ziwa Maboga liliopo Kisauni baada ya kuwazuru na kuwapa pole waathirika wa mvua hizo waliohifadhiwa katika Skuli ya Mwanakwerekwe “C” Balozi Seif aliuagiza Uongozi wa Shehia ya Kisauni kwa kushirikiana na Wilaya ya Magharibi “B” kumbomolea mtu ye yote atakayejenga katika eneo hilo.

Balozi Seif alitoa agizo hilo kufuatia nyumba nyingi zilizojengwa ndani ya  eneo la ziwa Maboga kufunikwa kabisa na maji ya mvua  licha ya kwamba eneo hilo linakuwa kavu wakati wa kiangazi.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kamwe haitamvumilia Mtu ye yote atakayekiuka agizo hilo la kujenga eneo hilo la ziwa hata kwa wale wenye tabia ya kujenga usiku na kumaliza pia watabomolewa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.