Habari za Punde

CCM kuendelea kuwalea vijana

 Vijana wa Maskani ya Wingi Sihoja ya Kinyikani Kojani Wete Pemba wakishangiria kwa Dufu wakati wa Hafla ya kukabidhiwa Vyarahani na Vipaza Sauti kutoka kwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa Balozi Seif Ali Iddi hapo katika Bustani ya Hoteli ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Tibirinzi Chake chake Pemba.

Balozi Seif alikuwa akitekeleza ahadi aliyowapa Vijana hao wakati wa ziara yake kwenye Maskani hiyo Tarehe 7 Septembna Mwaka 2015.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif  Ali Iddi akimkabidhi msaada wa  Vyarahani Vitano na Vipaza Sauti Mwenyekiti wa Maskani ya Wingi Sihoja ya Kijiji cha Kinyikani  Jimbo la Kojani Wete Pemba Nd. Makame Hamad Said.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Chama cha Mapinduzi kimeahidi kuendelea kuwalea Vijana wa Chama hicho wa Maskani ya Wingi Sihoja wa Kijiji cha Kinyikani Jimbo la Kojani Wilaya ya Wete kutokana na msimamo wao thabiti  usiotetereka wa kuendelea kukiunga mkono Chama hicho kilichopata ridhaa ya kuongoza dola.

Ahadi  hiyo imetolewa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi katika hafla fupi ya kuwakabidhi Vyarahani Vitano na Mashine ya Kupaza Sauti  hapo Hoteli ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar { ZSSF } Tibirinzi Chake chake Pemba akitekeleza ahadi aliyowapa kipindi alichofanya ziara Kijijini hapo.

Balozi Seif alisema yapo mengi yaliyosemwa dhidi ya CCM lakini inatia moyo kuwaona Vijana wa Maskani hiyo wakiendelea kuthamini kazi kubwa inayofanywa na Chama cha Mapinduzi katika kuwaletea maendeleo Wananchi wote bila ya ubaguzi au itikadi za kisiasa.


Alisema pamoja na dhoruba , vitisho na hujuma mbali mbali wanazozipata na kuendelea kupambana nazo lakini Vijana  hao hawajafanya makosa kwa uamuzi wao huo wa kuunga mkono Chama cha Mapinduzi.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka vijana hao kuhakikisha kwamba vifaa hivyo wanavitumia vyema katika harakati zao za kujitafutia riziki na kupunguza umaskini.

Balozi Seif alisema kwamba vifaa hivyo ni ukombozi kwao ambao unaweza kuwasaidia katika shughuli za kujiajiri  wenyewe badala ya kusubiri ajira za Serikali ambazo kwa kipindi hichi haziwezi kutosheleza vijana wote wanaomaliza masomo yao.

Akitoa shukrani kwa niaba ya viongozi na wanachama wa maskani hiyo ya Wingi Sihoja ya Kinyikani  Kojani Wete Pemba mmoja wa Viongozi wa Maskani hiyo Bwana Said Abeid Mussa alisema Vijana hao wameamua kujitolea kukienzi chama cha Mapinduzi kwa vile wamekirithi kutoka kwa wazazi wao.

Bwana Said alisema katika kutekeleza azma hiyo uongozi wa Maskani hiyo umeandaa mpango maalum wa kuwalea Vijana katika misingi na maadili sahihi yatakayowapa nguvu na uwezo wa kukiheshimu chama chao kikongwe katika Historia ya vyama vya siasa Nchini Tanzania.

Hata hivyo kiongozi huyo wa Maskani ya Wingi Sihoja Kojani alifafanua kwamba Wananchi wa akijiji hicho bado wanaendelea kukabiliwa na changamoto nyingi katika kujikwamua kimaendeleo likiwemo tatizo  sugu la ubovu wa Bara bara yao.

Alisema matatizo ya bara bara hiyo ya kilomita  Sita  yanaendelea kukwamisha malengo yao ya kusafirisha  bidhaa  zao wanazozizalisha  zinazotokana na mazao mengi ya kilimo.

Msaada huo wa Vyarahani na vipaza sauti uliogharimu jumla ya shilingi Milioni Moja na Laki sita umefuatia ziara ya Balozi Seif  aliyoifanya  katika Kijiji cha Kinyikani Kojani Wete ya Tarehe  7 Septemba mwaka 2015 ambapo alipokea changamoto zinazowakabili Vijana wa Maskani hiyo ya Wingi Sihoja.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.