Kwa siku akivuna shilingi 150,000
sasa hazidi shilingi 5000
Na Haji Nassor, Pemba
“MIMI na umaskini tulishaachana
kitambo, lakini sasa naurejea taratibu maana…!!!!...’’,aliniambia mwanamke huyo
huku akipata kigugumizi.
Ni
mcheshi na mchangamfu wakati wote na hasa anapokuwa kwenye biashara yake ya
duka la vinywaji na vyombo vya matumizi ya nyumbani eneo la Wawi wilaya ya
Chakechake ndani ya kisiwa cha Pemba.
Siti
Rashid Salim (39), ambae kwa sasa ni ameshatalikiwa na aliekuwa mume wake miaka
minne iliopita, aliamua kujiingiza kwenye biashara ya duka akiamini kuwa huko
ataagana na umaskini.
“Naam
biashara ya vyombo, juisi, soda na vitafunwa ilinikubwali kisawa sawa na mimi
nilishaagana na umaskini, na maisha yangu yalikuwa juu na nikawa mwanamke wa
kutegemewa na familia’’,anihadithia.
Siti
alienza biashara hiyo miaka minne iliopita, alilinunua duka hilo kutoka kwa
mwanajeshi mmoja, ambae yeye alipata uhamisho na kuhamia kisiwani Unguja kikazi.
Ndipo
alipojitokeza yeye kuchukua nafasi ya kuendeleza duka hilo, na kujikusanyia
idadi ya wateja wafikao 40 wa siku moja, na wakati akifunga duka mishale ya saa
3:30 usiku mapato hakuyaamini.
“Mimi
ilikuwa nahesbu mauzo, na kisha najikuta na shilingi 150,000 hadi shiingi
160,000 na hapo sasa familia ilianza kuniangalia kwa jicho la
utajiri’’,alifafanua.
Nikizungumza
nae kwenye duka lake eneo la Wawi, kwa muda wa saa moja bila ya kupokea mteja
kutokana na kugomewa kwa sababu ya chama anachokishabikia, anasema sasa yeye na
umaskini yuko karibu mno mithili ya meno na ulimi.
“Ahaa…duka
limekuwa limejaa hadi bidhaa nyengine kama chupa za chai zilikuwa nimezipanga
chini hadi nje barazani, sasa unaona kama lililoingia moto, hakuna liwalo na
umaskini umeshanipiga mbeleko’’,alinieleza kwa huzuni.
Ubeleko
kwa Pemba ni mtu kumchukua na kumuweka mgongoni, ndiovyo mjasiriamali huyu,
anavyojifafanisha yeye na kurejea tena kwenye umaskini, baada ya kubaguliwa na
wanakijiji wenzake.
Kwenye
biashara yake hiyo mchanganyiko, alininong’neza kwa sauti nyembamba kuwa,
uuzaji wa kinywaji cha juisi pekee ya matunda aliokuwa akiitengeneza mwenyewe,
akiuza kati ya shilingi 35,000 hadi shilingi 40,000 kwa siku moja.
Kumbe
ndoo nne za juisi kwa wakati huo kabla ya kugomewa, zilimtosheleza kumuda
gharama za kodi ya mlango, ambao ni shilingi 40,000 kwa mwezi mmoja.
Lakini
sasa kutokana na kuteswa na wanakijiji wenzake kwa kutomnulilia bidhaa zake, na
kuanza kujihesabu anaerudia kwenye dimbwi kama sio mto wa umaskini, ana deni la
mezi sita la kodi ya mlango.
“Hivi
sasa mwenye mlango juzi kaja kunikumbusha deni la mwezi Disemba mwaka 2015 hadi
Aprili mwaka 2016, sijamlipa, lakini kanipa tena muda’’,alinionyesha mkataba
wake mwanadada huyo.
Kumbe
mwanamke huyu mfanyabishara, ikifika mwezi Oktoba mwaka huu, atakuwa
ameshajikusanyia deni la kodi ya mlango la mwaka mmoja, la shilingi 480,000
sawa na shilingi 240,000 kwa kila miezi sita.
Nilipotaka
kufahamu mauzaji yake kwa siku, ili amudu gharama walau za kodi ya mlango na yeye
kujipatia mahitaji yake kwa siku, alisema hilo kwa sasa ni gumu.
Maana
kabla ya kususiwa na wateja wake ambao wengi wako vyama tofauti na yeye,
alikuwa akiiuza wastani wa shilingi 150,000 hasi shilingi 160,000 ambapo kwa
sasa hazidi shilingi 5000 kutoka asubuhi anapofungua hadi usiku.
“Sasa
biashara yangu imekufa mwandishi, nakushuruku wewe kuninunulia hiyo soda ya
shilingi 600, na mauzo yangu jana yalipanda kutoka shilingi 5,000 za kawaida
hadi shilingi 5,500 tu’’,alinieleza siku ya pili yake baada ya mahojiano haya.
Ukifika
ndani ya duka lake lililo nje kidogo ya mji wa Chakechake, utakaribisha na
nyuzi nyuzi alizokuwa akifungia biashara za kuning’nia sambamba na femu za
vyakula zikiwa tupu.
Ukandamiziaji
kama sio udhalilishwa kwa mwanamke huyu anaofanyiwa anasema haoni msaidizi
walau kama vyombo vya haki za binadamu wala viongozi wa dini.
Sas
anafungua duka hilo sio wakati wa kawaida, wala kwa ajili ya kujipatia kipato,
bali ni baada ya kumaliza shughuli zake za nyumbani, na hufanya kama sehemu ya mapunziko
tu.
“Silifungi
duka hata kama hawaninunulii, maana nikimaliza kazi za nyumbani hujazangu hapa
kama kijiweni kwangu, na walau kutia chaji simu yangu’’,alisema kwa huzini
sana.
Siti
ambae ni mjane, anaeishi na mama yake wa kambo na baba yake mazazi akiwa na
watoto watano, wanaomtegemea anahisi dunia na walimwengu kama waliomuinamia kwa
kukumba na hali ngumu ya maisha.
Ndani
ya duka laki hilo ambalo liko pacha na mwenzake mmoja ambae yeye hana shida na
wateja, anasema zipo bidhaa kama sahani za kigae, sabuni za unga, soda, juisi
zimeshakaa kwa muda bila ya kununuliwa jambo analolitarajia kumuongezea hasara.
“Sahani
sasa nazishusha bei kutoka shilingi 3,000 na sasa shilingi 2,000 na nashukuru
mwandishi walau umenunua sahani nne, lakini sijui hizi nyengine na vikombe nizifanye
nini’’,aliniambia akitiriri maneno ya huzuni.
Kwani
wateja wako unategemea wakaazi wa hapa kijiji cha Mbuni shehia za Wara na Wawi
pekee, nilimuuliza na kujibu kuwa hata wapita njia, lakini hao ndio wachache
sana.
Kutokana
na kukataliwa na wateja wake kwa sababu ya kushiriki uchaguzi wa marudio wa
Mchi 20, mwaka huu anaona dhahiri malengo ya kujenga nyumba yake ya kudumu
yamepotea.
“Unajua
malengo kwanza ni kujenga nyumba yangu, ili tusisongamane kwenye myumba ya
familia na kisha kukuza biashara ili niuze kwa jumla, lakini sasa wapi nimerudi
nyuma’’,anasema kwa uchungu.
Pamoja
na kuambiwa uso kwa uso na baadhi ya watu kwamba amegomewa lakini mwezi wa Machi
mwaka huu alibandikiwa karatasi ikitoa onyo kwamba kusiwe na mtu atakae mnunulia
mfanyabiashara.
“Tangaazo
si ruhusa mtu yoyote kutumiya dula la siti atakaeonekana kazi kwake’
ilieleza karatasi aliobandikiwa kwenye mlango wake wa duka na kuamua
kukihifadhi hadi leo.
Anasema
wapo watu wa familia yake wamekubaliana na wanakijiji kumgomea kwenye biashara,
ingawa anadhani kwenye harusi na misiba wanaweza kushiriki.
“Sijapa
harusi wala msiba tokea umalizike uchaguzi wa marudio, lakini sidhani kuwa
hawatashirikiana na mimi, wao zaidi ni kwenye biashara maana lengo mpaka
nihame’’,alifafanua.
Mmoja
wa wazazi wake ambae alisema asitangaazwe jina lake, alikiri kuwa mtoto wao
alishaanza kuwaonyesha njia ya kupunguza ukali wa maisha.
“Unajua
mwandishi ndani mwetu ilikuwa tukihitaji sabuni au kitoweleo lazima tukutane,
lakini biashara ilipokuwa imemkubali mtoto wetu Siti, wala hatukuwa na
shida’’,alisema mzazi huyo.
Anazidi
kunihadithi kuwa, hata eneo la kujenga nyumba ya kudumu kwa mtoto wao
walishakuwa nalo kwa ajili yake, lakini kutumia demokrasia yake Machi 20 ndio
matokeo yake hayo.
“Sisi
hatuachana na chama chetu cha CCM kwa sababu wengine tu hawapendi, wao
wanachama chao na sisi tuna chetu, sasa vyama na biashara havina uhusiano,
maana vipo vingi kusudi mtu achague atakacho’’,alisema.
Mmoja
kati yavijana wanaoishi mtaani hapo Ali Mohamed ambalo sio jina lake rasmi,
alinieleza kuwa kulikuwa na kikao maalumu kwa kila mtu hata awe CUF, ADC, CCM,
CHADEMA akishiriki uchaguzi wa marudio atengewe.
Lakini
mwanamke mmoja (45) wa kijiji hicho anasema hata wao walitakiwa wasinunue
bidhaa kwenye duka la Siti, ingawa hawakubaliana na wazo hilo.
Wamekuwa
wakitamani sana kumnunulia bidhaa mwanamke mwezao, ingawa wanahofu ya kutengwa
na wao na wakijiji kama agizo lilivyotoka.
Nilitaka
kujua kwa ndani juu ya hili, nilimtafuta Mwenyekiti wa CUF wilaya ya Chakechake
Saleh Nassor Juma, na kuthibitisha kuwa ndio agizo la baraza kuu la Chama
kutoshirikiana na mwanaCCM.
“Unajua
yaliojitokeza Oktoba 28 mwaka jana kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi, sasa CUF
iliazimia hata mwanachama wake akishirikia uchaguzi wa marudio, basi nae
atengwe na hayo yanayowakumba wenye biashara’’,alifafanua.
Yussuf
Ali Juma yeye ni Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Chakechake anaelewa vyema mateso yanayoendelea
kuwapata mwanachama wao kwa kugomewa biashara zao na shughuli za kiutu.
“Sisi
kama CCM twaseme hili wanalofanyiwa wanachama wetu, sio siasa tene ni ukiukwaji
wa haki za binadamu, lakini naamini yatakwisha siku moja’’,alieleza.
Anasema
wanachofikiria ni kuangalia uwezekano wa mwanachama wao Siti kuhamia eneo
jengine kibiashara ili ajikombowe na umaskini kama akihisi eneo alillo
linaendelea kumpotezea malengo.
CCM
inaendelea kushangaa kilichowakuta wanaowanachama wao zaidi ya 16, waliokumbwa
na mkasa wa kupewa talaka kwa sababu ya kushiriki uchaguzi wa marudio.
Lakini
Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania ofisi ya Zanzibar TAMWA kupitia
Mratib wake Mzuri Issa, hivi karibuni akizungumza na vyombo vya habari, alisema
lazima udhalilishaji wa aina hii upigwe vita.
“Mwanamke
kumzuilia kushiriki uchaguzi, au kumlazimisha kuchagua kiongozi anaetaka mwanamme
au kumsusia kwa sababu ya kutumia demokrasia yake ni udhalilisha mkubwa na
haufai’’,alisisitiza.
Haki
ya kupiga kura, ambayo ni haki ya kikatiba kwenye kifungu cha 7, cha Katiba ya
Zanzibar ya mwaka 1984, bado inaendelea kulitesa kundi la wanawake hapa
Zanzibar.
Huku
baadhi ya wanaharakati wa masuala ya kutetea haki za wanawake na watoto,
wakiwataja baadhi ya wanaume waliokwenye ndoa kuyatumia vibaya madaraka yao.
POLE SANA MAMA LAKINI KWA NINI USIJIUNGE NA WENZAKO UKAWA CUF KAMA WALIVYO WA PEMBA WENGI?UMEJIUNGA CCM HIYO NDIO SHIDA,KWA USHAURI WANGU WAOMBE RADHI WA PEMBA WENZAKO NA UJIUNGE NA CHAMA CHA CUF MAMBO YAKO YATAKWENDA SAWA KAMA MWAZO KUMBUKA WENGI WAPE IJAPOKUWA MAPEPE.HUWEZI KUWA CCM NDANI YA PEMBA UKAISHI KWA RAHA HIYO NI AFRICA NA HIZI NDIO SIASA ZETU.
ReplyDelete