Habari za Punde

Marufuku kutoa tiba mbadala bila ya kusajiliwa

 Mwenyekiti wa Bodi ya tiba asili na tiba mbadala Zanzibar Mohammed Kheri Mtumwa akitoa tarifa ya kupiga marufuku matangazo na vipindi vinavyotolewa katika vyombo vya habari alipokutana na wawakilishi  wa vituo vinavyotoa huduma hiyo katika Wizara ya  Afya Zanzibar.
  Baadhi ya wawakilishi wa vituo vya tiba asili na tiba mbadala wakimsikiliza Mwenyekiti wao wa Bodi (hayupo pichani) alipotangaza kupiga marufuku matangazo na vipindi vya huduma hizo katika vyombo vya habari.
 Sheikh Sabas Alkubra wa kituo cha tiba cha Jamaatul-Khairi  akitoa mchango wake katika mkutano ulioitishwa na Bodi ya Tiba asili na tiba mbadala katika Ofisi ya Wizara ya Afya Mnazi mmoja Zanzibar.

Mrajisi wa tiba asili Haji Juma Haji akitoa ufafanuzi kuhusu kupigwa marufuku matangazo ya tiba asili na tiba mbadala kwenye vyombo vya habari katika mkutano uliofanyika Wizara ya Afya Zanzibar.
Picha na Makame Mshenga/Maelezo Zanzibar.

Na Ramadhani Ali/Maele

Wizara ya Afya kupitia Baraza la Tiba asili na tiba mbadala imepiga marufuku kwa mtu yeyote kutoa huduma za tiba asili na tiba mbala bila ya kusajiliwa na Baraza hilo.

Akizungumza na wajumbe wa vituo vinavyotoa huduma hizo katika Wizara ya Afya Zanzibar,  Mwenyekiti wa Baraza la tiba asili na tiba mbadala Mohammed Kheri Mtumwa amesema kuanzia sasa hairuhusiwi kuendesha kituo cha kutolea huduma za tiba asili au tiba mbadala bila kusajiliwa.

Amewaeleza wajumbe hao kuwa ni marufuku kuuza au kugawa dawa ya tiba asili ama tiba mbadala mpaka iwe imesajiliwa na kufanyiwa uchunguzi na maabara ya mkemia mkuu wa Serikali na kupewa kibali na Bodi ya Chakula Dawa na Vipodozi.

“Wizara inapiga marufuku kwa mtu binafsi au taasisi yoyote kutumia kifaa tiba chochote bila kusajiliwa katika sehemu husika ya usajili wa vifaa tiba,”alisisitiza Mwenyekiti wa Baraza.

Ameongeza kuwa matangazo yote na vipindi  vinavyohusu tiba asili na tiba mbadala ambayo hayajapitishwa na Baraza yamezuiliwa kuanzia sasa.

Amesema lengo la Wizara kupitia Baraza la tiba asili na tiba mbadala kuweka masharti  ya kutoa huduma hizo ni kutaka kuhakikisha sheria, kanuni na miongozo inayotolewa inafuatwa.

Amesema Serikali inatambua na inathamini huduma za tiba asili na tiba mbadala na ni huduma inayotambuliwa na sayansi ya tiba ya kisasa lakini kwa muda mrefu imekuwa ikiendeshwa kama haina msimamizi.

Mwenyekiti  huyo wa Baraza amewaeleza wajumbe hao kuwa iwapo wataongeza mashirikiano na kuboresha huduma za tiba asili  wataweza kuuza dawa na huduma hizo nje ya nchi na kuimarisha uchumi wa nchi.

Nao wajumbe kutoka vituo vya tiba asili na tiba mbadala wameishauri Wizara ya Afya kupitia Baraza lao kuwajengea mazingira mazuri yatakayowawezesha  kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.

Wamesema suala la kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na Serikali za kutoa huduma  za tiba asili na tiba mbadala siyo tatizo kwani wanafahamu kila jambo linataratibu zake katika kuliendesha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.