Habari za Punde

Rais wa Zanzibar Dk Shein Ajumuika na Wageni Wake Ujumbe Kutoka Oman Katika Chakula cha Usiku.

STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar                                                                                                                16.10.2017
---
KIKUNDI cha Taarab cha Taifa kimekonga nyoyo za hadhira iliyohudhuria katika hafla ya Chakula maalum cha usiku kilichoandaliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kwa ajili ya wageni kutoka Serikali ya Oman ambao walikuwepo nchini kwa ziara maalum ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano.

Hafla hiyo ambayo mgeni rasmi alikuwa Rais Dk. Shein, ilifanyika hapo jana katika ukumbi wa zamani wa Baraza la Wawakilishi, Kikwajuni mjini Zanzibar ambapo Makamo wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd na Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mwanamwema Shein nao walihudhuria.

Viongozi mbali mbali wa Serikali ya Oman pamoja Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar walihudhuria ambapo kwa upande wa Serikali ya Oman Waziri wa Mafuta na Gesi wa nchi hiyo Dk. Mohammed bin Hemed Al Ruhmi aliongoza ujumbe wa Oman.

Taarab hiyo ilienda sambamba na chakula hicho maalum cha usiku kilichoandaliwa na Rais kwa ajili ya wageni hao na kuweza kutoa burudani murua ambayo iliweza kuwafurahisha wageni pamoja na wenyeji wa hafla hiyo.

Waimbaji wa kikundi hicho cha Taifa cha taarab waliimba nyimbo mbali mbali za taarab zikiwemo zile za asili ambazo hadi hivi leo bado zinaendelea kupendwa kutokana na muziki na ala zake sambamba na ujumbe uliomo kwenye nyimbo hizo.

Waimbaji mahiri kutoka katika kikundi hicho waliweza kutoa burudani safi ya nyimbo zao akiwemo Sabina Bint Hassan aliyoimba nyimbo isemayo ‘Kama yalivyonipata’ nyimbo iliyotungwa na Mzee Haji na kutiwa sauti na Abass Machano.

Professa Mohammed Ilyas naye hakuwa nyuma katika kutoa burudani kwenye usiku huo maalum kwa kuimba nyimbo isemayo ’Nipepee’, ambapo naye Saada Nassor  aliimba wimbo uitwao ‘Kibali’, wimbo uliotungwa na Chimbeni Kheir na kutiwa sauti na yeye mwenye Chimbeni Kheir ambaye hivi sasa ni Mshauri wa Rais katika masuala ya utamaduni, utalii na michezo.

Makame Faki na nyimbo yake ‘Tumependana wenyewe’ nyimbo iliyotungwa na Nasma Khamis na kutiwa sauti na yeye mwenyewe Makame Faki almaarufu Sauti ya Zege, nayo iliweza kukonga nyoyo za hadhira hiyo iliyofika katika hafla hiyo sambamba na nyimbo ‘Nnae’ iliyoimbwa na Idd Suwed.

Makofi, hoihoi, nderemo na vigeregere vilisikika katika ukumbi huo pale wageni kutoka Serikali ya Oman walipoomba wimbo wa ‘Kama yalivyonipata’ uimbwe tena na bila ya ajizi Sabiha Bint Hassan na kikundi chake hicho cha Taifa uliirejea nyimbo hiyo.

Akitoa neno la shukurani katika hafla hiyo kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, Waziri wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Issa Haji Gavu alisisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendeleza uhusiano kati yake na Serikali ya Oman kwa mafanikio ya pande zote mbili.

Waziri Gavu aliongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande wake  itaendeleza uhusiano, ushirikiano pamoja na umoja uliopo kati yake na Oman huku akipongeza juhudi zinazochukuliwa kwa kila upande katika kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa.

Aidha, Waziri Gavu alieleza kuwa kuwepo kwa uhusiano na kukuza ushirikiano uliopo ni mbegu ya kuimarisha umoja na mshikamano kati ya Oman na Zanzibar.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.