Habari za Punde

TTCL yalia na Taasisi za Serikali kutolipa madeni

Na Salmin Juma, Pemba

MWENYEKITI wa Bodi wa Kampuni ya simu za mkononi ya TTCL Omar Rashd Nundu ameitaka Serikali ya Mkoa wa Kaskazini Pemba kusaidia kuzihamasisha taasisi za Serikali na binafsi  zinazodaiwa na kampuni hiyo kulipa madeni yao .

Amesema Kampuni inategemea fedha kutoka kwa wateja wake ili kujiendesha ambapo uwepo wa madeni mengi unaweza kuzorotesha utendaji wa kazi zake.

Akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Nundu ameitaka serikali ya mkoa kulipa kipaumbele cha pekee suala la kuziomba taasisi za serikali ambazo zinadaiwa na kampuni hiyo   kulipa madeni yao.

“Tunaiomba Serikali ya Mkoa kupitia kwako Mkuu wa Mkoa kuzihamasisha taasisi ambazo zinadaiwa na Kampuni kulipa madeni yao ili kuifanya kampuni kuweza kutekeleza wajibu na majukumu yake ya kazi ”alisema.

Aidha Nundu amesema Kampuni ya TTCL ni chombo cha kimkakati cha kupunguza kero za Muungano , ambacho kwa sasa inakusudia kuboresha huduma zake Unguja na Pemba kwa kuhakikisha wanaweka kituo cha kupokelea taarifa Zanzibar.

Naye Waziri Waziri Mjumbe wa Bodi hiyo amesema bila ya ushirikiano kutoka Serikali kuu Kampuni pekee haiwezi kufanikisha malengo yake ya ukusanyaji wa mapato kutoka kwa wadeni wake .

Amefahamisha kuwa malengo ya Kampuni hiyo ni kuboresha huduma zake na kwamba mipango ni kuhakikisha ifikapo mwishoni mwa mwaka huu huduma ziwe zinapatikana katika ubora wa halia ya juu.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Omar Khamis Othman  ameishauri bodi hiyo kuandaa utaratibu wa kuwahamasisha viongozi wa taasisi kuanza kutumia huduma za kampuni hiyo .

Aidha amesema ni vyema kampuni hiyo kuwakutanisha viongozi wa serikali na kuwatala kurejesha utaratibu wa zamani wa kuunganisha huduma za ttcl kwenye ofisi zao .

“Ni vyema Kampuni kuwaandalia mazingira mazuri wakuu wa Taasisi za Serikali kurejea utaratibu wa zamani wa kutumia huduma za Kampuni ya TTCL kwenye Ofisi zao , hii itaisaidia kuweza kufikia malengo yake ”alisisitiza.

Amesema kuwa Kampuni inalo jukumu kubwa la kujitangaza ili iweze kuingia kwenye ushindani wa soko la biashara na kwamba wakuu wa Taasisi wanaouwezo wa kufanikisha kuirejesha kampuni hiyo kwenye makali yake 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.