Habari za Punde

Wazazi waendelea kuwahimiza watoto wao kuokota mpetaNA HAJI NASSOR, PEMBA

WAZAZI na walezi ambao watoto wao wanaendelea kuokota karafuu zinazoanguka chini “mpeta” wamesema kwa kipindi hichi cha msimu wa zao la karafuu, waalimu wa vyuo vya Qur-an wataendelea kuwakosa watoto, hasa siku za mwisho mwa wiki.

Walisema kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa watawalazimishe wabakie kwenye madrassa na skulini, lakini siku mbili za mwisho wa wiki, wawasamehe maana hufuatana nao katika kazi ya kuokota mpeta.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu wananchi hao wa  vijiji vya Ngomeni, Chambani, Mtambile, Mtuhaliwa, Wambaa, Mwambe, Kiwani, Pujini na Mgelema  walisema lazima wawashajishe watoto kuokota karafuu.

Mmoja katia ya wazazi hao Hamida Issa Ussi wa Bwegeza Mwambe, alisema kwa vile wanapokuwa na watoto wake wanne, hujipatia kati ya shilingi 32,000 hadi shilingi 40,000 kwa siku, hafikirii wanawe kuwakatisha kuokota mpeta kwa siku mbili kwa wiki.

“Mimi wanangu siku zote tano huwataka na kuwalazimisha kushiriki kwenye masomo, lakini kwa siku za Jumamosi na Jumapili, waalimu wa madrassa au skuli kwa masomo ya ziada hawapatikani”,alisema.

Asha Mselemu Habibu wa Pujini, alisema kutokana na hali yake ya maisha ya watoto sita ambao baba yao ameshafariki miaka imnne sasa, lazima watoto wake wamsaidie huduma za siku.

“Maisha kwa sasa ni magumu na hasa ambao ni sisi wajane hatuna mtu wa kumtegemea, kipindi kuna riziki ya karafuu na keshokutwa yaondoka, lazima watoto tutoke pamoja”,alieleza.

Aidha mzazi huyo alisema mwanawe mmoja anasoma darasa la kumi akitarajiwa kufanya mitihani miezi michache ijayo, lakini suala la huduma za ndani kwa kipindi hichi nae linamgusa.

Kwa upande wake Mwanaisha Kassim Ussi, alisema hata vyuo vya Qur-an wapo baadhi ya waalimu wamekubali kuvifunga kwa wanafunzi wanaookota mpeta, maana wamekuwa wahazuiliki.

“Alfjairi swala swala kwa siku za Jumamosi na Jumapili watoto wote wakiwemo wangu watano, huwa tunatoka kwenda Ngomeni kuokota karafuu, na mimi wala siwazuii maana siku tano za wiki zawatosha kusoma”,alifafanua.

Mwalimu mmoja wa madrasaa Mwambe wilaya ya Mkoani, Mcha Hassan Jaku, alisema ana idadi ya wanafunzi 45 kwenye madrassa yake, ingawa kwa siku za mwishoni mwa wiki huopungua mara tatu.

“Wanafunzi ninaobaki nao kuhudhuria madrassa kwa siku za Jumamosi na Jumapili, ni wale ambao wazazi wao wanafanyakazi serikali pekee, lakini wengine wote huwenda Ngomeni na Mtambile kuokota mpeta”,alifafanua.

Hata hivyo alisema, wapo baadhi ya wazazi waliotaka madrassa hizo kwa kipindi hichi kufungwa hasa mwishoni wa mwiki, ingawa yeye na kamati yake ilikataa.

Msaidi mwalimu mwalimu wa madrsaa Hassan Haji Hassan wa Chambani, alisema wamefika pahala wamechoka kuvutana na baadhi ya wazazi na sasa wamewaachia watoto ili kushiriki uokotaji mpeta.

“Tokea tunawapiga, kisha tukamua kuwafukuza madrssa lakini wameendelea kuwazuia watoto wao, na sisi wanaokuja kwa siku mbili hizo za mwisho wa wiki tunawasomesha, lakini naamini msimu wa uvunaji wa karafuu ukimalizika watakuja kama kawaida”,alisema.

Mkuu wa wilaya ya Mkoani Hemed Suleiman Abdulla, ameendelea kutoa tamko lake la kuwataka wazazi na walezi kutowaruhusu watoto wao na wao wenyewe wasiokote mpeta.

Alisema kwanza watoto hao wanatakiwa kuhudhuria kwenye mdarassa na skulini ili kukabiliana na mitihani ya taifa, ambayo inatarajiwa kufanyika mwezi ujao.


Serikali za wilaya na mikoa kisiwani Pemba, zilishapiga marufuku tokea mwanzoni mwa msimu, kwamba hakuna mwanamke wala mtoto anaeruhusiwa kuokota mpeta, kwa mdai ya kuongozeka vitendo vya udhalilishaji katika kipindi kama hiki.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.