Habari za Punde

Wazazi watakiwa kuwaendeleza watoto wao kielimu - Wito

 Mjumbe wa NEC na Mbunge wa jimbo la Chwaka Bhagwanji M.Meisura (aliyesimama) akitoa nasaha zake kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Wazazi CCM huko katika Ukumbi wa Jamhuri Hall Wete
 Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Wazazi Mkoa wa Kaskazini Pemba wakimsikiliza mgeni rasmi Mbunge wa jimbo la Chwaka Bhagwanji M.Meisuria  wakati wa uchaguzi wa kuchagua viongozi ambao wataiongoza jumuia hiyo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo 2017/2022 huko katika ukumbi wa Jamhuri Hall Wete.  (PICHA NA SAID ABDULRAHMAN  PEMBA)
 Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Wazazi Mkoa wa Kaskazini Pemba wakimsikiliza mgeni rasmi Mbunge wa jimbo la Chwaka Bhagwanji M.Meisuria  wakati wa uchaguzi wa kuchagua viongozi ambao wataiongoza jumuia hiyo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo 2017/2022 huko katika ukumbi wa Jamhuri Hall Wete.  (PICHA NA SAID ABDULRAHMAN  PEMBA)

Msimamizi Mkuu wa uchaguzi wa viongozi wa jumuia ya Wazazi Mkoa wa Kaskazini Pemba Simba  Haji Mcha  Katibu Msaidizi Organization kutoka Makao Makuu ya CCM akitangaza matokeo ya washindi katika uchaguzi huo
uliofanyika katika ukumbi wa Jamhuri Hall Wete  ( PICHA NA SAID ABDULRAHMAN  PEMBA)

NA / SAID ABDULRAHMAN—PEMBA.

MJUMBE wa Mkutano Mkuu wa CCM (NEC) Zanzibar na Mbunge wa jimbo la Chwaka, Bhagwanji M.Meisuria, amewataka wazazi kuendeleza kielimu watoto wao  ili waweze kuja kuwa viongozi bora wa hapo baadae.

Bhagwanji, aliyasema hayo huko katika Ukumbi wa Mikutano Jamhuri Hall Wete, wakati akifungua Mkutano wa jumuia ya wazazi wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Mjumbe huyo wa CCM, aliwahakikishia wazazi hao kuwa yeye binafsi yuko tayari kushirikiana na Jumuia hiyo katika kuwaendeleza vijana katika sekta ya elimu pamoja kuiipa msukumo Skuli ya Sekondari Dodeani ambayo
inamilikiwa na jumuia hiyo.

Bhagwanji, aliwasisitiza wajumbe wa Mkutano huo kushikiana kwa pamoja katika kuhakikisha malezi ya vijana wao yanakwenda sambamba na matakwa ya Chama chao pamoja na kuwahamasisha vijana kujiunga na chama hicho.

“Niwaombe wazazi wenzangu tusimamieni malezi ya watoto wetu kwani kwa siku za hivi sasa kumezuka wimbi kubwa la vitendo vya udhalilishaji pamoja ubakaji kwa watoto wadogo wakike na wakiume jambo ambalo linatia aibu nchi yetu”,alifahamisha Mbunge huyo.

Akizungumzia suala la madawa ya kulevya ambalo limekuwa tishio kwa Vijana,alisema   Zanzibar imeonekana kuwa ni kituo kikuu cha kupitishia madawa hayo, hivyo alitanabahisha kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa kushirikiana na Serkali ya Zanzibar zinafanya juhudi kubwa kutokomeza janga hili.

“Madawa ya kulevya yamekuwa yakiwaathiri vijana wetu ambao ndio tunao wategemea kuwa viongozi wetu  hapo baadae, hivyo ninachowataka wazazi tushiriane kwa pamoja ili tuweze kuliondosha balaa hili na wala tusiwafumbie macho wale wote ambao wanashiriki kwa njia moja ama nyengine”,alisema Bhagwanji.

Akisoma taarifa ya miaka 5, Katibu wa wazazi Mkoa wa Kaskazini Pemba, Hamad Issa Hamad, alisema   jumuia hiyo imepata mafanikio makubwa katika kipindi chote hicho kutokana na mashirikiano mazuri waliyokuwa nayo wanachama pamoja na viongozi wa jumuia hiyo.

“Katika kipindi cha miaka mitano inayomalizika leo,jumuia yetu iliweza kupata mafanikio mengi ambayo ni makubwa kutokana mashirikiano yaliyokuwepo baina ya viongozi wa jumuia hiyo na wanachama wake”,alisema Katibu Hamad.

Katika uchaguzi huo ambao ulikuwa na utulivu sana, Msimamizi wa uchaguzi huo Simba Haji Mcha, alimtangaza Khamis Shaame Hamad kuwa Mwenyekiti mpya wa Jumuia hiyo kwa Mkoa wa Kaskazini baada ya kupata kura 47 sawa na asilimia 54% na kuwashinda wapinzani wake Saleh Ali Faki aliepata kura 11 na Hamad Khamis aliepata kura 26.

Wengine walichaguliwa katika uchaguzi huo ni pamoja na Mwanaidi Omar Khamis kuwa mjumbe atakaeiwakilisha Jumuia hiyo UWT ya Wazazi ,Yussuf Mbwana Ali pamoja na Juma Hija Khatib wajumbe wa Baraza la Mkoa , Ramadhan Issa Kipaya mjumbe wa Baraza kuu na Mkutano Mkuu wa Taifa CCM na Assa Ali Hussein , Rashid Khalfan Suleiman pamoja na Makame Faki Ali hawa wameteuliwa kuiwakilisha Jumuia ya wazazi katika baraza kuu.

Akitoa neno la shukrani kwa wajumbe wa mkutano huo,Mwenyekiti mpya ya jumuiya ya Wazazi , aliwataka wajumbe wote kushirikiana kwa pamoja katika kuujenga umoja huo bila ya kujali sehemu wanazotoka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.