Habari za Punde

Hutuba ya Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Ikiwasilishwa na Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Mhe.Dkt. Khalid Salum Mohammed . P


Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Mhe.Dkt. Khalid Salum Mohammed akiwasilisha Hutuba ya Mapato na Matumizi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi katika Mkutano wa Kumi wa Baraza la Tisa la Wawakilishi Chukwani Zanzibar.Kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019.
YALIYOMO                    

 MAPENDEKEZO YA MAKADIRIO YA BAJETI (MAPATO NA MATUMIZI) YA SERIKALI KWA MWAKA WA FEDHA 2018/19 KATIKA BARAZA LA WAWAKILISHI

I.        UTANGULIZI

1.          Mheshimiwa Spika, natanguliza shukran kwa Mola wetu muumba na muweza kwa kutujaalia sote uhai, uzima na neema nyengine zilizotuwezesha kukutana tena alasiri hii ili kutimiza wajibu wetu muhimu kwa jamii tunayoitumikia na kuiongoza. Wajibu huu unatokana na matakwa ya Kifungu cha 106 cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 (kama ilivyorekebishwa) na Kifungu cha 41(3) cha Sheria ya Fedha za Umma namba 12 ya mwaka 2016.
2.          Mheshimiwa Spika, vifungu hivyo vinamtaka Waziri anayehusika na Fedha, kabla ya kumalizika mwaka wa Fedha, kutayarisha na kuyawasilisha Baraza la Wawakilishi Makadirio ya Bajeti ya mwaka unaofuata. Kwa kuwa mwaka wa Fedha wa 2017/18 unakaribia kumalizika, Mapendekezo haya ya makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa 2018/19 yanawasilishwa ili kutimiza matakwa hayo ya Kikatiba na Sheria.
3.          Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo, na kwa heshima kubwa, sasa naomba kutoa hoja kwamba Baraza lako tukufu likae kama Kamati Maalum ya kujadili Mapendekezo ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mwaka 2018/19.
4.          Mheshimiwa Spika, jamii inayorudi nyuma kwa maendeleo yake ya kiuchumi, au yenye migogoro miongoni mwake, au baina yake na Serikali inayoingoza, au iliyokata tamaa kwa maisha yake ya baadae ni chachu kwa kukosekana amani ya kudumu na maendeleo ya kweli. Wakati tukielekea kukamilisha mwaka mwengine wa fedha na wa utekelezaji wa Ilani yetu ya Uchaguzi ya mwaka 2015, nchi yetu imeendelea kupata mafanikio makubwa ya kiuchumi na kijamii; imeshuhudia utulivu mkubwa na mashirikiano ya wananchi na Serikali yao; na imeendelea kuleta matumaini mapya ya maisha bora zaidi kwa wananchi wake.
5.          Mheshimiwa Spika, kama ilivyo kwa nchi yoyote, mafanikio hayo kwa kiasi kikubwa yanatokana na Serikali iliopo madarakani na imani ya watu wa nchi kwa Serikali hiyo. Kwa hivyo mafanikio tunayoyaona kwetu hayana budi kunasibishwa na kiongozi wetu, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Naomba basi nitumie fursa hii kumpongeza sana Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, kwa mwaka mwengine wa uongozi thabiti, wenye hekima na subira na wa mfano. Bado tunamuombea maisha marefu na uongozi wenye uadilifu kwa kipindi chake chote cha kutuongoza.
6.          Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais ameendelea kufaidika na ushauri na usaidizi wa karibu wa Makamo wake wa Pili, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi. Nasi sote tulio katika dhamana mbalimbali pia tumefarijika sana na uongozi na maelekezo ya mara kwa mara ya Mheshimiwa Makamo wa Pili wa Rais. Nachukua fursa hii kutambua mchango mkubwa wa jasho na fikra zake katika mafanikio tunayoendelea kuyapata na kumpongeza kwa dhati kwa uongozi wake usioyumba.
7.          Mheshimiwa Spika, kwangu mimi binafsi bado naendelea kupata heshima kubwa kwa imani ya Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kunipa heshima ya kutumikia dhamana hii adhimu ya Waziri wa Fedha na Mipango kwa nchi yetu. Kwangu mimi hii ni heshima kubwa sana na nitaendelea kuithamini, kuishukuru na kuitumikia kwa uwezo wangu wote.
8.          Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa pili mfululizo tunasoma mapendekezo ya Bajeti Kuu ya Taifa wakati Wizara zote zikiwa zimeshawasilisha mapendekezo ya Bajeti zake. Kwa mara nyengine tena tumeshuhudia mijadala ya kina katika Baraza hili kwa mapendekezo ya Bajeti kutoka Wizara za Serikali. Ni dhahiri kuwa kama taasisi, Baraza la Wawakilishi chini ya uongozi wako Mheshimiwa Spika limezidi kuimarika.
9.          Mheshimiwa Spika, nakupongeza sana wewe, Naibu wako Mheshimiwa Mgeni Hassan Juma na Wenyeviti wa Baraza, Mhe. Shehe Hamad Mattar na Mhe. Mwanaasha Khamis Juma, kwa uimara na uweledi mkubwa mnaotumia katika kuliongoza Baraza hili. Kupitia uongozi wenu, Baraza hili tukufu na nguzo muhimu kwa mustakabali wa Zanzibar linaweza kutimiza wajibu wake wa Kikatiba wa kuisimamia Serikali kwa niaba ya Wananchi wote wa Pemba na Unguja.
10.      Mheshimiwa Spika, nawapongeza pia Waheshimiwa Wajumbe wote wa Baraza lako tukufu kwa umahiri na kujitolea kwao katika kuwakilisha Wananchi wa majimbo na, kwa ujumla wao, wananchi wote wa Zanzibar. Sisi tuliopo katika dhamana za Serikali tunathamini sana mchango mkubwa unaotolewa na Wajumbe wako katika kuimarisha utendaji wa Serikali na katika kukuza demokrasia na uwajibikaji nchini.
11.      Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo ya utangulizi na pongezi, naomba nianze kwa kupitia kwa mukhtasari hali ya uchumi wetu na utekelezaji wa Bajeti kwa miezi tisa ya awali kwa mwaka unaoendelea wa fedha wa 2017/18.

II.     HALI YA UCHUMI NA MAENDELEO

12.      Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina ya mwenendo wa uchumi na matokeo yake katika maendeleo yetu niliyatoa leo asubuhi wakati nilipowasilisha mapitio ya Hali ya Uchumi kwa mwaka 2017 na utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2017/18.
13.      Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza asubuhi, uchumi wetu umeendelea kuonesha mwenendo mzuri. Sikusudii kurejea maelezo yote niliyoyatoa asubuhi ya leo lakini niruhusu nigusie tena mambo muhimu ya uchumi wetu kwa mwaka uliopita, 2017, kama ifuatavyo:
i.              Pato letu halisi la Taifa limeongezeka kwa asilimia 7.5 mwaka jana ikilinganishwa na mwaka 2016 ambapo Uchumi ulikuwa kwa asilimia 6.8. Kasi hii ya ukuaji ni kubwa zaidi kuliko takriban nchi zote za ukanda wa Afrika ya Mashariki na ni ukuaji mkubwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita;
ii.             Kujitokeza kiwango cha Mfumko wa Bei cha asilimia 5.6 ambacho ni kidogo zaidi katika miaka minne iliyopita;
iii.          Kufanikiwa kupata mzao mkubwa zaidi wa Karafuu wa Tani 8,543.9 ambazo hazijawahi kufikiwa tokea mwaka 1996/97 ambapo Tani 11,368.3 za Karafuu zilipatikana;
iv.           Kuimarika kwa uzalishaji wa mazao ya chakula kutoka Tani 227,256 mwaka 2016 hadi Tani 304,800 mwaka 2017, sawa na ongezeko la asilimia 34.1; na
v.             Kuendelea kuimarika kwa Sekta ya Utalii ambapo Idadi ya watalii waliotembelea Zanzibar imeongezeka kwa asilimia 15.2 kutoka watalii 376,242 wa mwaka 2016 hadi 433,474 mwaka 2017.
14.      Mheshimiwa Spika, mwenendo wetu huu wa uchumi unapaswa kuendelezwa na kuimarishwa zaidi kwani ni chachu muhimu ya maendeleo yetu. Tayari tunashuhudia kuimarika kwa mapato yetu ya ndani, kama nitakavyoeleza baadae, kutokana na kuimarika kwa uchumi. Mafanikio haya ni matokeo ya hali njema ya amani na utulivu inayovutia uwekezaji na shughuli za biashara, Sera nzuri zilizopo, na uongozi thabiti na wa uadilifu wa Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein.

III.      MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI KWA KIPINDI CHA MIEZI TISA (JULAI 2017– MACHI 2018):

a.   Makadirio ya Mapato

15.      Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2017/18 Serikali ilikadiria kukusanya jumla ya TZS 1,087.4 bilioni ikijumuisha, mapato kutokana na vyanzo vya ndani jumla ya TZS 675.8 bilioni sawa na asilimia 21.8 ya Pato la Taifa. Kati ya fedha hizo, jumla ya TZS 627.0 bilioni zilipangwa zitokane na makusanyo ya vyanzo vya kodi. Kitaasisi, asilimia 55.4 ya mapato hayo yalitarajiwa kukusanywa na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), sawa TZS 347.3 bilioni.
16.      Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikadiriwa kukusanya TZS 258.7 bilioni sawa na asilimia 41.3 ya mapato yote ya kodi na TZS 21 bilioni, sawa na asilimia 3.3 ya mapato ya kodi, zilipangwa kukusanywa na Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali kutokana na Kodi ya Mapato kwa wafanyakazi wa SMT waliopo Zanzibar. Aidha, jumla ya TZS 48.8 bilioni zilitarajiwa kukusanywa kutoka vyanzo mbalimbali visivyo vya kodi.
17.      Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa Misaada kutoka nje, kwa mwaka 2017/18 ilikadiriwa kupokea Ruzuku ya TZS 82.2 bilioni na Mikopo ya TZS 298.3 bilioni. Hivyo, jumla ya fedha zote zilizotarajiwa kutoka nje ni TZS 380.5 bilioni.
18.      Mheshimiwa Spika, ili kuziba nakisi iliyojitokeza ya Bajeti, Baraza lako tukufu liliidhinishia Serikali kukopa jumla ya TZS 30.0 bilioni kutoka soko la ndani ili kukidhi upungufu huo wa Bajeti.

b.   Makadirio ya Matumizi

19.      Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2017/18 Serikali ilikadiria kutumia kiasi hicho cha TZS 1,087.4 bilioni kugharamia Bajeti yake. Jumla ya TZS 590.7 bilioni ziliidhinishwa kwa matumizi ya kazi za kawaida na TZS 496.6 bilioni kwa matumizi ya kazi za maendeleo. Aidha, kati ya fedha hizo za maendeleo, TZS 116.1 bilioni ni kutokana na mapato ya ndani na TZS 380.5 bilioni kutokana na mapato kutoka nje.

c.   Utekelezaji Halisi

20.      Mheshimiwa Spika, Kwa kipindi cha miezi tisa (Julai hadi Machi 2018), ukusanyaji wa mapato umekuwa wa kuridhisha. Kwa ujumla, Serikali imemudu kukusanya jumla ya TZS 677.6 bilioni. Kati ya kiasi hicho, TZS 506.6 bilioni, sawa na asilimia 74.7 ya mapato yote ni mapato ya ndani, TZS 151.0 bilioni, sawa na asilimia 22.3 ya mapato yote ni mapato kutoka nje na TZS 20.0 bilioni ni mikopo ya ndani, sawa na asilimia 3 ya mapato yote.
21.      Mheshimiwa Spika, Makusanyo halisi ya TZS 506.6 bilioni ni sawa na asilimia 98 ya makadirio ya kipindi hicho kati ya TZS 515.1 bilioni. Katika kipindi kama hicho kwa mwaka uliopita (2016/2017), mapato ya ndani yalifikia jumla ya TZS 389.8 bilioni. Utendaji huu unamaanisha ukuaji wa mapato kwa TZS 116.8 bilioni sawa na ongezeko la asilimia 30.
22.      Mheshimiwa Spika, Kati ya mapato ya ndani, mapato ya Kodi ni TZS 465.2 bilioni, sawa na asilimia 97 ya lengo la kukusanya TZS 478.5 bilioni. Mapato yasiyo ya kodi ni TZS 41.4 bilioni. Matokeo haya yanaashiria utendaji mzuri zaidi katika ukusanyaji wa mapato yasiyokuwa ya kodi kupitia Wizara zetu. Makusanyo hayo ni sawa na asilimia 113 ya makadirio ya TZS 36.6 bilioni. Aidha, mapato hayo yamekuwa kwa asilimia 75 ikilinganishwa na ukusanyaji wa TZS 23.7 bilioni kwa miezi tisa ya awali ya mwaka uliopita.

d.  Ukusanyaji wa Mapato Kitaasisi

23.      Mheshimiwa Spika, Kwa kipindi cha mapitio, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ilikusanya jumla ya TZS 190.5 bilioni sawa na asilimia 99 ya makadirio ya TZS 193.2 bilioni. Kwa kiwango hicho cha utendaji, makusanyo ya TRA yameongezeka kwa asilimia 25 ikilinganishwa na ukusanyaji wa kipindi kama hicho kwa mwaka 2016/2017 ambapo jumla ya TZS 152.5 bilioni zilikusanywa.
24.      Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), makusanyo halisi yamefikia TZS 258.9 bilioni sawa na asilimia 96 ya makadirio ya TZS 269.5 bilioni. Hata hivyo, ikilinganishwa na TZS 197.5 bilioni zilizokusanywa katika kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2016/17, ZRB imeonesha ukuaji mkubwa zaidi wa mapato wa asilimia 31.1.
25.      Mheshimiwa Spika, Makusanyo ya Kodi ya Mapato kutoka kwa wafanyakazi wa SMT waliopo Zanzibar yalifikia TZS 15.75 bilioni sawa na asilimia 100 ya makadirio ya kipindi hicho. Kwa mikopo katika soko la ndani, Serikali imekopa jumla ya TZS 20.0 bilioni kupitia Hati Fungani, sawa na asilimia 66.7 ya makadirio ya mwaka ya kukopa TZS 30.0 bilioni. 

e.   Mapato ya Nje

26.      Mheshimiwa Spika, Katika kipindi hiki cha mapitio (Julai – Machi 2018), Serikali imepokea, kutoka kwa nchi wahisani na Mashirika ya fedha ya Kimataifa, jumla ya TZS 151.0 bilioni ambazo takriban ni asilimia 40 ya makadirio ya mwaka. Kati ya kiasi hicho, Ruzuku ni TZS 34.1 bilioni na Mikopo ni TZS 116.9 bilioni. Aidha, jumla ya TZS 3.2 bilioni zilipatikana kutokana na Misaada ya Kibajeti (General Budget Support – GBS) na TZS 2.6 bilioni kutokana na Misamaha ya Madeni (MDRI). Fedha zote zilizopatikana kutokana na Misaada ya nje zimetumika kwa shughuli za utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo badala ya matumizi ya kawaida ya uendeshaji wa Serikali.

IV.       UTEKELEZAJI WA HATUA ZA KUIMARISHA MAPATO KWA MWAKA WA FEDHA 2017/18.

27.      Mheshimiwa Spika, kupitia Sheria ya Fedha ya mwaka 2017, Baraza lako liliidhinisha marekebisho katika Sheria mbalimbali kwa lengo la kuimarisha ukusanyaji na usimamizi wa Mapato ya Serikali. Mukhtasari wa utekelezaji wa hatua hizo ni kama ifuatavyo:
    i.        Sheria ya Mafunzo ya Amali (Vocational Training Act)
28.      Mheshimiwa Spika, Marekebisho ya kufungu cha 27 (4) cha Sheria ya Mafunzo ya Amali (Vocational Training Act No.8 ya 2006) yamefanywa kwa kutoa tafsiri ya “Gross Monthly Emolument” ambayo mwajiriwa hatakatwa gharama za mafunzo pamoja na mavazi (uniforms) anazopatiwa na mwajiri wake kwa mwezi tofauti na ilivyokuwa hapo awali. Kama ilivyotarajiwa, hatua hii haikuwa na athari yoyote katika ukusanyaji wa mapato bali imesaidia kuleta usawa katika mfumo wa kodi.
  ii.        Sheria ya Ajira (Employment Act.)
29.      Mheshimiwa Spika, Marekebisho yamefanywa kwenye Kifungu cha 100 (2) cha Sheria ya Ajira (Employment Act No.11 of 2005) kwa kuelekeza kuwa malipo yote ya mishahara kufanywa kupitia akaunti za benki za waajiriwa. Waajiri wengi tayari wameanza kulipa mishahara ya wafanyakazi wao kupitia benki. Hadi kufikia Machi 2018 jumla ya TZS 2.46 bilioni zimekusanywa kutokana na Kodi zitokanazo na mshahara, sawa na asilimia 410 ya makadirio kwa mwaka.
iii.        Kanuni za Ada ya Biashara (Trade Levy Regulations):
30.      Mheshimiwa Spika, tayari Serikali imeacha kutoza Ada ya Biashara (Trade Levy) kwa uingizaji wa pembejeo za viwandani na malighafi. Tunaamini kuwa utekelezaji wa hatua hii umeleta faraja kwa wazalishaji viwandani na utasaidia kuimarisha uendelezaji wa viwanda nchini.
 iv.        Kutungwa kwa Sheria ya Ushuru wa Bidhaa
31.      Mheshimiwa Spika, Kama ilivoahidi, Serikali imetunga Sheria hiyo ya Ushuru wa Bidhaa na utekelezaji wake umeanza rasmi mwezi wa Agosti mwaka 2017. Jumla ya TZS 1.2 bilioni zimekusanywa kutokana na hatua hii katika miezi tisa.
   v.        Kufutwa kwa Sheria ya Ushuru wa Stempu Nam. 6 Ya 1996 na Kutungwa Sheria ya Ushuru wa Stempu
32.      Mheshimiwa Spika, Sheria mpya ya Ushuru wa Stempu imetungwa na kuanza kutumika rasmi mwezi wa Julai 2017. Sheria hiyo imechukua nafasi ya Sheria ya Ushuru wa Stempu namba 6 ya mwaka 1996 ambayo imefutwa. Jumla ya TZS 0.96 bilioni zimekusanywa sawa na asilimia 240 ya makadirio ya bajeti ya TZS 0.4 bilioni;
 vi.        Kutoza VAT Kwenye Huduma za Fedha
33.      Mheshimiwa Spika, Utekelezaji wa hatua hii umeanza rasmi mwezi wa Julai 2017. Jumla ya TZS 1.6 bilioni zimekusanywa sawa na asilimia 45 ya makadirio ya mwaka ya TZS 3.5 bilioni.
vii.        Usajili wa Namba Binafsi za Magari (Private Number Registration)
34.      Mheshimiwa Spika, Utekelezaji wa hatua hii umeanza rasmi Desemba 2017 baada ya kusainiwa kwa Kanuni. Lengo la hatua hiyo linaelekea kufikiwa kwani kwa miezi tisa hiyo hakuna mwananchi yoyote aliyejitokeza kwa ajili ya usajili huo.  

a.   MATUMIZI:

        i.    Jumla ya Matumizi

35.      Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha miezi tisa (Julai - Machi 2018), kupitia Kamati ya Ukomo wa Matumizi, jumla ya TZS 695.0 bilioni zilikadiriwa kutumika. Kati ya matumizi hayo, TZS 461.6 bilioni ni kwa kazi za kawaida na TZS 233.4 bilioni ni kwa kazi za maendeleo. Hadi kufikia Machi 2018, matumizi halisi yalifikia TZS 681.6 bilioni sawa na asilimia 98 ya makadirio ya kipindi hicho. Kati ya matumizi hayo TZS 457.1 bilioni zilitumika kwa kazi za kawaida na TZS 224.5 bilioni kwa kazi za maendeleo.

      ii.    Matumizi ya kazi za kawaida

36.      Mheshimiwa Spika, Matumizi ya kazi za kawaida kwa kipindi cha mapitio yalifikia jumla ya TZS 457.1 bilioni. Kiwango hicho cha matumizi kinaashiria kuongezeka kwa matumizi ya kawaida kwa asilimia 34.9 ikilinganishwa na matumizi ya kipindi kama hicho mwaka 2016/2017 ambapo jumla ya TZS 338.8 bilioni zilitumika. Kati ya matumizi hayo, matumizi ya mishahara yalifikia TZS 209.7 bilioni sawa na asilimia 100 ya makadirio ya kipindi hicho. Matumizi hayo ya mishahara ni sawa na asilimia 30.2 ya matumizi yote ya kipindi hicho na sawa na asilimia 45.8 ya matumizi yote ya kazi za kawaida. Aidha, kwa ujumla, Matumizi ya kazi za Kawaida yanamaanisha ukuaji wa asilimia 40.3 ikilinganishwa na TZS 149.5 bilioni zilizotumika kipindi kama hicho kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
37.      Mheshimiwa Spika, Mwenendo mzuri wa uwezo wetu wa kuhudumia Bajeti umejionesha pia katika matumizi ya kuendeshea Serikali (Other Charges). Matumizi haya yameongezeka kwa asilimia 23.8 kutoka TZS 66.5 bilioni zilizotumika katika miezi tisa ya awali ya mwaka 2016/17 hadi TZS 82.3 bilioni kwa miezi tisa ya mwaka huu. Aidha, ikilinganishwa na makadirio ya TZS 84.1 bilioni kwa kipindi hicho, kiwango hicho cha matumizi kinamaanisha kuwa Serikali imemudu kutoa Shilingi 98 kati ya kila Shilingi mia moja zilizopangwa kwa ajili ya uendeshaji wa kazi za kawaida. Haya ni mafanikio makubwa na ya kupongezwa na kupigiwa mfano.
38.      Mheshimiwa Spika, taswira hiyo hiyo ya kuongezeka uwezo wa kuhudumia mambo yetu imejitokeza katika utoaji wa Ruzuku kwa Taasisi zetu. Ikilinganishwa na mwaka uliopita, fedha zilizotolewa na Serikali kwa mwaka huu ni asilimia 68.7 zaidi. Kwa ujumla, TZS 71.2 bilioni zilitolewa sawa na asilimia 88 ya makadirio ya TZS 80.9 bilioni ya kipindi hichi. Katika kipindi kama hicho mwaka jana kiasi kilichotolewa kama Ruzku kwa Taasisi zetu kilifikia TZS 42.2 bilioni tu.
39.      Mheshimiwa Spika, eneo jengine muhimu katika matumizi ya kawaida ni matumizi kwa ajili ya huduma za Mfuko Mkuu wa Serikali. Matumizi hayo ni kwa ajili ya kulipia viinua mgongo, pencheni, ulipaji wa Mishahara kwa Viongozi Wakuu na waliotajwa katika Katiba, riba za mikopo ya ndani, malipo ya Wazabuni pamoja na matumizi maalum ya Serikali yanapojitokeza. Kwa miezi tisa ya awali ilikadiriwa kuwa tungetumia TZS 88.2 bilioni kwa huduma hizo kutoka TZS 80.6 bilioni zilizotumika katika kipindi kama hicho mwaka uliopita. Hata hivyo, matumizi halisi yalifikia TZS 93.9 bilioni sawa na asilimia 106 ya makadirio yakimaanisha pia ukuaji wa asilimia 16.5.

   iii.    Matumizi ya kazi za Maendeleo

40.      Mheshimiwa Spika, Katika kipindi cha mapitio, Kamati ya Ukomo wa Matumizi ilikadiria kuwa matumizi kwa kazi za maendeleo yangefikia TZS 233.4 bilioni. Matumizi halisi yamefikia TZS 224.5 bilioni sawa na asilimia 96 ya lengo. Matumizi kutokana na fedha zetu za ndani yameongezeka kwa asilimia 86 baada ya kufikia TZS 73.5 bilioni kutoka TZS 39.5 bilioni zilizotumika katika kipindi kama hicho mwaka 2016/17. Hata hivyo, makadirio kutokana na fedha za ndani yalikuwa kutumia TZS 82.4 bilioni, hivyo utendaji huo ni sawa na asilimia 89.2 ya makadirio. Matumizi kutokana na Misaada kutoka nje yalifikia ni TZS 151 bilioni, nayo yakionesha ongezeko la asilimia 224.7 kutoka TZS 46.5 bilioni za mwaka jana.
41.      Mheshimiwa Spika, Ongezeko hilo limetokana zaidi na kukwamuka kwa Mradi wa Ujenzi wa Jengo jipya la abiria katika Uwanja wa Ndege wa Zanzibar ambapo katika Kipindi hicho, Benki ya Exim ya China inayofadhili mradi huo kwa mkopo nafuu ilitoa Dola za Marekani 35.2 milioni sawa na takriban TZS 78.9 bilioni.

b.   Deni la Taifa

42.      Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa Deni la Taifa kwa dhamira ya kuhakikisha linaendelea kubaki katika kiwango kinachohimilika. Aidha, Serikali inaendelea kuheshimu misingi mikuu (Fiscal Responsibility Principles) kama ilivyotajwa katika Kifungu cha 5 cha Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma, namba 12 ya mwaka 2016.
43.      Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Deni, misingi hiyo inayosimamiwa na Serikali ni pamoja na hii ifuatayo:
i.            Kuhakikisha kuwa Deni la Taifa ni himilivu;
ii.           Kuhakikisha kuwa kwa Kipindi cha Muda wa Kati, Serikali inakopa kwa ajili ya matumizi ya Kazi za Maendeleo na sio kugharamia kazi za Kawaida;
iii.        Kusimamia rasilimali na deni la umma kwa kutowabebesha mzigo mkubwa kizazi kijacho; na
iv.         Kuwa na akiba inayotesheleza kuhudumia deni la nje.
44.      Mheshimiwa Spika, pamoja na kuzingatia misingi hiyo, hadi kufikia Machi 2018, Deni la Taifa limekuwa na kufikia TZS 519.7 bilioni kutoka TZS 377.1 bilioni mwezi Machi 2017, sawa na ukuaji wa asilimia 37.8. Katika kiasi hicho, deni la ndani ni TZS 158.3 bilioni na deni la nje ni TZS 361.4 bilioni.
45.      Mheshimiwa Spika, kuongezeka kwa deni kumechangiwa na sababu zifuatazo:
                i.    Kuanza tena kutolewa fedha za mkopo kwa ajili ya ujenzi wa jengo jipya la abiria ambapo jumla ya Dola 35.2 milioni (TZS 78.9 bilioni) zimelipwa;
              ii.    Mkopo mpya wa Hati Fungani wa TZS 20.0 bilioni kati ya TZS 30.0 bilioni zilizoidhinishwa kukopwa ndani;
            iii.    Kuongezeka kwa kiwango cha malipo ya Kiinua Mgongo kutokana na kuimarika kwa maslahi ya Wafanyakazi. Jumla ya TZS 17.7 bilioni zimelipwa kwa wastaafu 1075 kwa mwaka 2017/2018 ukilinganisha na TZS 15.3 bilioni zilizolipwa kwa wastaafu 1,604 kwa mwaka 2016/2017; na
             iv.    Kwa deni la nje, athari ya mabadiliko ya kiwango cha kubadilishia fedha.
46.      Mheshimiwa Spika, pamoja na ongezeko hilo, thamani ya deni letu (face value) ni sawa na asilimia 16.8 ya Pato letu la Taifa la mwaka 2017. Kigezo cha uhimilivu wa deni ni kuwa lisipindukie asilimia 50 ya Pato la Taifa kwa thamani za sasa za deni (Present Value). Hivyo, kwa kiwango cha asilimia 16.8 kwa Pato la Taifa, bado tuna kiwango kidogo cha kudaiwa, deni letu linahimilika na tuna fursa zaidi ya kukopa tukihitaji, kwa ajili ya kuharakisha maendeleo yetu. Hata hivyo, bado inakusudiwa kuendelea kutumia busara (prudence) kwa Serikali kuingia katika madeni.

        i.    Mapato na Matumizi ya Mfuko wa Miundombinu:

47.      Mheshimiwa Spika, Jumla ya mapato yaliyopokelewa kutokana na Mfuko wa Miundombinu kwa kipindi cha Julai hadi Machi 2018 yamefikia TZS 24.3 bilioni sawa na asilimia 89.0 ya lengo la TZS 27.3 bilioni kwa kipindi hicho. Mapato hayo yamejumuisha makusanyo kutoka ZRB ya TZS 17.4 bilioni sawa na asilimia 89.2 ya makadirio ya TZS 19.5 bilioni na ya TRA ya TZS 6.9 bilioni sawa na asilimia 88.5 ya makisio ya TZS 7.8 bilioni.
48.      Mheshimiwa Spika, kwa upande wa matumizi, jumla ya TZS 34.90 bilioni zilikadiriwa kutumika kwa miradi iliyoorodheshwa chini ya Mfuko wa Miundombinu kwa mwaka 2017/18. Kwa kipindi cha mapitio, TZS 20.4 bilioni zimetumika sawa na asilimia 58.5 ya makisio.

V.          MATARAJIO YA MAPATO NA MATUMIZI MWAKA 2017/18

a.   Matarajio ya Mapato Julai – Juni 2017/2018

49.      Mheshimiwa Spika, utekelezaji wetu wa Bajeti kwa kipindi kilichobakia cha robo mwaka unatarajiwa kuendelea kuchangiwa na sababu tofauti zikiwemo zifuatazo:
i.        Shughuli za kiuchumi katika kipindi hicho;
ii.      Utendaji wa TRA, ZRB na Wizara zetu katika kukusanya mapato;
iii.    Utekelezaji wa miradi na upatikanaji wa fedha kutoka kwa Washirika wa Maendeleo;
iv.     Mahitaji ya matumizi muhimu kama yatakavyojitokeza.
50.      Mheshimiwa Spika, kutokana na sababu hizo, matarajio ni kuwa tutaumaliza mwaka kwa kukusanya jumla ya TZS 881.4 bilioni, takriban sawa na asilimia 85 ya makadirio ya mwaka. Kati ya kiasi hicho, mapato ya ndani ni TZS 680.0 bilioni na mapato kutoka nje ni TZS 201.4 bilioni.
51.      Mheshimiwa Spika, kutofikiwa lengo la mapato kunatarajiwa kuchangiwa na kiwango cha upatikanaji wa misaada (Ruzuku na Mikopo) kutoka nje. Hali ya ukusanyaji wa mapato kutoka vyanzo vyetu vya ndani inatarajiwa kuwa nzuri ambapo jumla ya TZS 680.0 bilioni zinatarajiwa kukusanywa. Ikilinganishwa na lengo la kukusanya TZS 675.9 bilioni kwa mwaka huu wa fedha, matarajio ya utendaji ni sawa na asilimia 100.6 ya lengo hilo. Aidha, kwa utendaji huo kunajitokeza ukuaji wa mapato kwa asilimia 30.5 ikilinganishwa TZS 521 bilioni zilizokusanywa mwaka uliopita, 2016/17.
52.      Mheshimiwa Spika, Kati ya makusanyo hayo, mapato yatokanayo na kodi ni TZS 612.4 bilioni, sawa na asilimia 97.6 ya makadirio ya TZS 627.01 bilioni. Ikilinganishwa na makusanyo ya TZS 478.3 bilioni ya mwaka wa fedha uliopita 2016/17, kiasi hicho cha mapato kitapelekea ukuaji wa mapato ya kodi wa asilimia 28.04 baina ya miaka hiyo miwili.
53.      Mheshimiwa Spika, Kitaasisi, utendaji wa TRA unatarajiwa kufikia asilimia 96.3 kwa kukusanya TZS 249.2 bilioni. Ikilinganishwa na mwaka uliopita ambapo ilikusanya TZS 203.9 bilioni, mapato ya TRA yataongezeka kwa asilimia 22.2. Kwa upande wa ZRB, pia kunajitokeza ukusanyaji wa kuridhisha kwa kigezo cha kufikia lengo na ukuaji wa mapato. ZRB inatarajia kukusanya TZS 342.2 bilioni sawa na asilimia 98.5 na sawa na ukuaji wa asilimia 35.2 kutoka makusanyo ya TZS 253.5 bilioni yaliyopatikana mwaka uliopita 2016/17. Kodi ya Mapato kutoka Serikali ya Muungano inayosimamiwa na Mhasibu Mkuu wa Serikali inatarajiwa kufikia TZS 21.0 bilioni sawa na asilimia 100 ya lengo.
54.      Mheshimiwa Spika, kuhusu mapato yasiyokuwa ya kodi, utekelezaji umeendelea kuonesha mwendo mzuri na wa kutia matumaini. Mapato haya yanatarajiwa kufikia TZS 68.1 bilioni na hivyo kuwa asilimia 38.5 zaidi ya lengo la kukusanya TZS 48.8 bilioni. Makusanyo hayo yanapelekea ukuaji wa asilimia 54.5 ikilinganishwa na TZS 43.8 bilioni zilizokusanywa kutoka kianzio hiki kwa mwaka wa fedha uliopita.
55.      Mheshimiwa Spika, katika makusanyo hayo, Mapato ya Mawizara yanategemewa kufikia TZS 51.4 bilioni sawa na asilimia 122.9 ya makadirio ya mwaka ya TZS 41.84 bilioni; Gawio la Mashirika ya Serikali linatarajiwa kufika TZS 3.2 bilioni sawa na asilimia 106.7 ya makadirio ya mwaka ya TZS 3 bilioni na Gawio la Benki Kuu ya Tanzania, ni TZS 13.5 bilioni sawa na asilimia 337.5 ya makadirio ya mwaka ya TZS 4 bilioni.

b.   Mfuko wa Miundombinu

56.      Mheshimiwa Spika, Kwa mwaka wa fedha 2017/18, matarajio ya mapato ya Mfuko wa Miundombinu ni TZS 33.6 bilioni sawa na asilimia 92.5 ya makadirio kwa mwaka huo. Kati ya kiasi hicho, TRA inatarajiwa kukusanya TZS 10.0 bilioni sawa na asilimia 74.1 ya lengo la kukusanya TZS 13.5 bilioni na ZRB inatarajiwa kukusanya TZS 23.6 bilioni kati ya lengo la TZS 21.3 bilioni, sawa na asilimia 110.8

c.   Matarajio ya Matumizi, (Julai – Juni) 2017/2018

57.      Mheshimiwa Spika, Hadi kufikia Juni 2018, kwa ujumla, matumizi yanatarajiwa kufikia TZS 865.1 bilioni sawa na asilimia 80.0 ya Bajeti ya mwaka ya TZS 1,087.4 bilioni. Kati ya kiasi hicho, matumizi ya kazi za kawaida yanatarajiwa kufikia TZS 559.2 bilioni wakati Matumizi ya maendeleo yatafikia TZS 305.9 bilioni.

d.  Matarajio ya Mpango wa Maendeleo, 2017/18

58.      Mheshimiwa Spika, Kati ya TZS 305.9 bilioni zinazotarajiwa kutumiwa na Serikali kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa programu 27 na miradi 46 ya maendeleo, Serikali inatarajia kutumia jumla ya TZS 104.5 bilioni kutokana na mapato yake ya ndani na Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuchangia TZS 201.4 bilioni, zikihusisha Ruzuku ya TZS 45.5 bilioni na mikopo ya TZS 155.9 bilioni.
59.      Mheshimiwa Spika, katika Hotuba yangu ya mwaka jana nilielezea dhamira ya Serikali ya kusawazisha deni linalodaiwa Shirika la Umeme (ZECO) na Shirika kama hilo la Tanzania Bara (TANESCO). Deni hilo ni kutokana na ununuzi wa umeme unaofanywa na ZECO kutoka TANESCO kwa ajili ya matumizi ya visiwa vyetu, Pemba na Unguja. Nilieleza nia ya Serikali ya kuhakikisha kuwa ZECO inalipa kwa ukamilifu Ankara zake zote mpya kwa bei iliyokubalika na pande mbili ili kuzuia kurundikana zaidi kwa deni hilo. Nilieleza pia hatua ambazo Serikali na ZECO zitachukua kumaliza kiasi kilichokuwa kimebakia.
60.      Mheshimiwa Spika, naomba kuliarifu Baraza lako tukufu kuwa ZECO inaendelea kulipa kwa ukamilifu Ankara zote na hivyo kuepuka kuingiwa deni jipya. Kwa mwaka huu tunaoumalizia, ZECO imelipa jumla ya TZS 18.5 bilioni na hivyo kufanya jumla ya deni lililolipwa kufikia TZS 23.8 bilioni. Kwa upande wake, Serikali imelipa jumla ya TZS 2.0 bilioni na kwa hivyo kufanya jumla ya malipo kwa kipindi cha miaka miwili kufikia TZS 15.0 bilioni. Kwa mantiki hiyo, ZECO na Serikali kwa pamoja wameshalipa TZS 38.8 bilioni na kubakisha deni la TZS 26.8 bilioni. Itakumbukwa pia, ili kulimaliza haraka deni hilo, SMZ imependekeza kwa Wizara ya Fedha na Mipango (SMT) kuilipa TANESCO moja kwa moja TZS 18.0 bilioni inazoidai kupitia katika Kodi ya Mapato ya Wafanyakazi wa SMT wananaofanyakazi Zanzibar ambazo hazijalipwa hapo kabla. Kwa upande mwengine, Taasisi kadhaa za Serikali ya Muungano zinadaiwa na ZECO jumla ya TZS 1.7 bilioni ambapo itafanya jumla ya deni la SMT linalodaiwa kufikia 19,7 bilioni ambazo kama zitalipwa TANESCO itabakiza deni la TZS 7.1 bilioni tu.  Kwa nia njema ya kulimaliza deni hilo, katika mwezi wa Oktoba mwaka jana, Serikali ilipendekeza kwa Serikali ya Muungano kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kulimaliza deni hilo kupitia katika madeni ya marejesho ya Kodi ambayo Zanzibar inaidai SMT.
61.      Mheshimiwa Spika, mapendekezo hayo yakikubaliwa na SMT yatasaidia katika maeneo kadhaa, Mosi, utasaidia kulimaliza deni lote kwa mkupuo mmoja. Pili, utasaidia kupunguza athari za Kibajeti kwa SMZ; na tatu, utapelekea SMZ kulipwa pesa zote inazodai hadi sasa kutokana na marejesho ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na Ushuru wa Bidhaa. Tunaendelea kufuatilia ili kupata ridhaa ya SMT kwa nia ya kumaliza vyema suala la madeni hayo yanayodaiana pande mbili za Jamhuri ya Muungano.
62.      Mheshimiwa Spika, katika Hotuba ya mwaka jana pia nilieleza uamuzi wa Serikali wa kuanza na Ugatuzi wa madaraka kutoka Serikali Kuu kwenda Serikali za Mitaa (Mabaraza ya Manispaa, Mabaraza ya Miji na Halmashauri za Miji). Maeneo yaliyohusika na Ugatuzi huo ni pamoja na Elimu ya Maandalizi na Msingi, Afya ya Msingi na Huduma za Ugani na nyenginezo katika Kilimo. Nina furaha kulijuilisha Barza hili kuwa ugatuzi huo umeanzwa kama ilivyopangwa na kwa ujumla umeendelea vyema.
63.      Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo ya mapitio ya utekelezaji wa Bajeti ya mwaka tunaokaribia kumalizika wa 2017/18, naomba sasa niwasilishe mapendekezo ya Bajeti kwa mwaka 2018/19 kama ninavyotakiwa na Katiba yetu ya mwaka 1984 kama ilivyorekebishwa.
64.      Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya fedha namba 12 ya mwaka 2016 na Kanuni za Baraza la Wawakilishi, maandalizi ya Bajeti ya mwaka 2018/2019, yalitanguliwa na uwasilishwaji wa Mwelekeo wa Bajeti katika Baraza la Wawakilishi mwezi Februari mwaka huu. Mwelekeo huo umekuwa Dira ya utayarishaji wa Bajeti hii ambayo leo ninaiwasilisha mbele ya Baraza lako. Mapendekezo ya Makadirio haya ya Mapato na Matumizi ya mwaka ujao (2018/2019) ninayowasilisha leo hii yameongozwa na Mwelekeo huo ulioidhinishwa wa Bajeti   na mazingatio ya Vipaumbele vya Taifa.
65.      Mheshimiwa Spika, makadirio haya ya Bajeti yametokana na matarajio ya ukuaji mzuri wa uchumi kama nilivyoeleza kwa kina katika hotuba yangu leo asubuhi. Kwa ufupi, tunatarajia ukuaji mzuri zaidi wa uchumi kwa mwaka 2018 ambao utakua kwa kasi ya asilimia 7.7 itayotokana na kukua kwa sekta za Huduma, Kilimo na Viwanda, utakaochangiwa zaidi na ukuaji rasilimali utaotokana na ujenzi wa miundombinu.

VI.       MWELEKEO WA MAPATO:

a.   Mapato ya Ndani

66.      Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kuwa wakati akizindua Baraza la 9 la Wawakilishi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, alieleza nia ya Serikali ya kuimarisha zaidi usimamizi wa mapato yetu na kuelekea zaidi kujitegemea katika kuendesha mambo yetu badala ya kutegemea Wafadhili. Kuhusu mapato, Mheshimiwa Rais alikumbusha kuwa ahadi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa wananchi, kama ilivyobainishwa katika Ilani yake ya Uchaguzi ya mwaka 2015, ni kukusanya kiasi cha TZS 800.0 bilioni ifikapo mwaka wa 2020.
67.      Mheshimiwa Spika, wazee wetu walishatuambia kuwa ahadi ni deni na dawa ya deni ni kulipa. Na kwa deni hili, kulilipa kwake ni kwa Serikali hii ya CCM kukusanya angalau TZS 800.0 bilioni kutokana na vyanzo vya ndani ifikapo mwaka 2020.
68.      Mheshimiwa Spika, nina fakhari kubwa kulijuilisha Baraza lako tukufu kuwa Serikali imedhamiria kutimiza ahadi hiyo na hivyo kulipa deni lake kwa wananchi.  Serikali inakusudia kutimiza ahadi hiyo katika mwaka ujao wa fedha, 2018/19, mwaka mmoja kabla, badala ya kusubiri mwaka 2020 kama ilivyoahidi.
69.      Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2018/19, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, katika awamu yake ya saba inayoongozwa na Dkt. Ali Mohamed Shein, inatarajia kukusanya jumla ya TSZ 807.5 bilioni kutokana na vyanzo vya ndani. Makadirio haya ni sawa na ongezeko la asilimia 18.7 kutoka mapato ya TZS 680.0 bilioni yanayotarajiwa kukusanywa kwa mwaka wa fedha 2017/18 kama nilivyoeleza awali.
70.      Mheshimiwa Spika, mchanganuo wa mapato hayo ni kama ifuatavyo:
i.              Mapato yatokanayo na kodi ni TZS 727.5 bilioni;
ii.            Mapato ya Mawizara ni TZS 71.0 bilioni;
iii.          Gawio la Mashirika ya Serikali ni TZS bilioni 5; na
iv.           Gawio kutoka Benki Kuu (BoT) ni TZS 4 bilioni.
71.      Mheshimiwa Spika, Kitaasisi, mgawanyo wa jukumu la kukusanya kiasi hicho cha mapato ni kama ifuatavyo:
i.          Mamlaka ya Mapato (TRA) imekadiriwa kukusanya jumla ya TZS 301.1 bilioni ambapo Idara ya Forodha na Ushuru imekadiriwa kukusanya TZS 165.9 bilioni na Idara ya Kodi za Ndani TZS 135.2 bilioni;
ii.         Bodi ya Mapato inatarajiwa kukusanya TZS 485.4 bilioni ikiwemo TZS 405.4 bilioni za Mapato ya kodi, TZS 71.0 bilioni Mapato ya Mawizara na TZS 9.0 bilioni za Gawio la Benki Kuu na Mashirika ya SMZ;
iii.      Ofisi ya Mhasibu Mkuu wa Serikali inatarajiwa kusimamia upatikanaji wa TZS 21.0 bilioni zitokanazo na Kodi ya PAYE kwa wafanyakazi wa Muungano waliopo Zanzibar.

b.   Mapato ya Nje

72.      Mheshimiwa Spika, pamoja na nia yetu ya dhati ya kuharakisha kujitegemea, bado tutaendelea kushirikiana na Mataifa rafiki na Mashirika ya Kifedha na ya Kibinaadamu ya Kimataifa katika kughramia Maendeleo yetu. Kwa mwaka wa fedha 2018/19, Serikali inatarajia kupokea jumla ya TZS 464.2 bilioni kutokana na Mikopo na Ruzuku kutoka nje ya nchi. Kati ya kiasi hicho, TZS 388.6 bilioni kinatarajiwa kutokana na Mikopo na TZS 75.6 bilioni ni Ruzuku. Bado Serikali haitaingiza moja kwa moja Misaada ya Kibajeti (GBS) katika mipango yake ya matumizi. Tutaendelea kutumia utaratibu wa Kibajeti wa “100T” ili kukidhi haja ya matumizi pindi Misaada hiyo ikipokelewa katikati ya mwaka.

VII.    MAPENDEKEZO YA HATUA ZA KUIMARISHA MAPATO

73.      Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikuchukua hatua maalum za kuweka utulivu wa mfumo wa kodi nchini kama njia mojawapo ya kushajiisha uwekezaji na ulipaji wa Kodi kwa hiari. Kwa mara nyengine tena, Serikali haipendekezi kupandisha kodi katika mwaka ujao wa fedha. Badala yake, Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha usimamizi na ukusanyaji wa mapato. Kwa mustakabali huo, hatua zinazopendekezwa ni hizi zifuatazo:
i.    Sheria ya Ushuru wa Stempu namba 7 ya mwaka 2017
74.      Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitoza Ushuru wa Stempu kwa bidhaa ambazo zimesamehewa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT). Miongoni mwa bidhaa hizo ni za vyakula muhimu kwa jamii yetu kama vile mchele na unga wa ngano. Bidhaa hizo zilisamehewa VAT kwa dhamira ya kupunguza gharama za maisha. Kwa lengo hilo hilo, Serikali inapendekeza kurekebisha Sheria ya ushuru wa Stempu kwa kufuta Ushuru huo kwa uingizaji, usambazaji na uuzaji wa bidhaa za mchele na unga wa ngano nchini ili kutoa unafuu zaidi kwa bei za chakula.
75.      Mheshimiwa Spika, marekebisho mengine yanayopendekezwa katika Sheria hii ni kufutwa kwa Ushuru wa Stempu kwenye tiketi za ndege zinazotolewa na mashirika ya Kimataifa hapa Zanzibar kwa safari za nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lengo ni kuleta usawa wa kodi na Tanzania Bara ambayo kwa sasa haitozi ushuru huo hivyo kuendelea kuutoza hapa Zanzibar kunaathiri biashara hiyo.
ii.  Kufanya mapitio ya mfumo wa misamaha ya ushuru wa stempu katika kuhaulisha mali (Transfer of property)
76.      Mheshimiwa Spika, Sheria ya Ushuru wa Stempu inataka Ushuru huo utozwe hata pale ambapo mali inahama kutoka kwa mmiliki wake kwenda kwa mtu mwengine kwa njia ya mirathi au kutoa kwa hiba bila ya kuwepo malipo kutoka kwa anaepokea. Inapendekezwa kufuta Ushuru wa Stempu wakati wa uhaulishaji mali (transfer of Property) bila ya malipo pale mali hizo zinapohaulishwa kwa utaratibu wa urithi na baina ya mzazi au mlezi wa kisheria na mtoto au mume au mke wa ndoa anapompa mwenza wake kwa hiba;
iii. Kuongeza Muda wa Kuwasilisha Ritani na Malipo ya Kodi
77.      Mheshimiwa Spika, muda unaohitajika kuwasilisha Ritani ya mauzo kila mwezi na muda wa kuwasilisha malipo ya Kodi Serikalini ni muhimu kwa Walipakodi kutimiza matakwa ya Sheria na athari katika gharama za kuwajibika kisheria. Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Kodi (TAPA) namba 7 ya mwaka 2009, kwa sasa walipakodi wanapaswa kuwasilisha Ritani kwa Kodi mbalimbali si zaidi ya siku ya 10 ya mwezi unaofuatia mwezi wa mauzo. Aidha, siku ya mwisho kufanya malipo ni tarehe 15 ya mwezi huo unaofuatia mwezi wa mauzo. Baada ya mashauriano na Sekta binafsi, Serikali inapendekeza kubadilisha tarehe hizo na kuzichanganya kuwa siku moja, tarehe 20 ya mwezi unaofuatia mauzo kwa kuwasilisha Ritani na kufanya malipo.
78.      Mheshimiwa Spika, zaidi ya hatua hizo za kisheria, Serikali pia itachukua hatua za kiutawala zenye lengo la kuimarisha ukusanyaji wa mapato. Miongoni mwa hatua hizo ni hizi zifuatazo:
iv. Kutoa Muongozo wa Kodi ya Zuio (Withholding Tax)
79.      Mheshimiwa Spika, Wizara na Taasisi za Serikali zimekuwa zikizuia Kodi za VAT na ya Mapato mbambali wakati wa malipo kwa wazabuni. Imebainika kuwa bado si malipo yote yanayopaswa kuzuiliwa na kuwasilishwa ZRB na TRA yanafanywa hivyo. Ili kurekebisha kazoro zilizopo, kwa mwaka ujao wa fedha, Serikali itatayarisha na kutoa Muongozo wa Usimamizi na Ukusanyaji wa Kodi ya Zuio (Withholding Tax Guideline) kwa Wizara, Idara na Taasisi mbali mbali za Serikali. Hatua hii itaongeza mapato ya Serikali ya TZS 8.5 bilioni;
v.   Kuimarisha Usimamizi wa Utoaji wa Leseni
80.      Mheshimiwa Spika, bado tuna tatizo la baadhi ya watu kufanya biashara bila ya kusajiliwa na TRA na ZRB na hivyo kuikosesha Serikali mapato yake. Serikali itasimamia mamlaka zote za utoaji wa leseni za biashara, ikiwemo Serikali za Mitaa, kuhakikisha kuwa hakuna leseni zinazotolewa bila ya Mfanyabiashara kusajiliwa na TRA na ZRB na kuonesha Hati ya kutodaiwa kodi (Tax Clearance Certificate) kutoka TRA na ZRB. Matarajio ni kwua hatua hii itaiingizia Serikali jumla ya TZS 4.5 bilioni;
vi. Kodi ya Majengo (Property Tax)
81.      Mheshimiwa Spika, matayarisho ya ukusanyaji wa Kodi ya Majengo (Property Tax) yamefikia hatua kubwa. Serikali itaanza rasmi kutoza kodi hiyo katika mwaka ujao wa Fedha (2018/19) kwa majengo ya biashara. Jumla ya TZS 5.0 bilioni zinatarajiwa kukusanywa na kuhaulishwa kwenda Serikali za Mitaa kwa kutumia vigezo maalum vya mgao vinavyokaribia kukamilishwa.  
vii.               Kufanya mapitio ya viwango vya Ada
82.      Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikifanya mapitio ya viwango vya ada zinazotozwa katika huduma mbalimbali kwa lengo vya kuvifanya viendane na mahitaji ya wakati. Serikali itaendelea na mapitio hayo katika mwaka ujao wa Fedha, hatua ambayo inatarajiwa kuingiza jumla ya TZS 0.4 bilioni.
viii.             Kupunguza unafuu wa Kodi ili kulinda Viwanda vya Ndani
83.      Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitoa unafuu wa Ushuru wa Forodha na Kodi nyengine kwa uingizaji wa bidhaa muhimu za chakula kama vile mchele, unga wa ngano na sukari. Hata hivyo, kufuatia kuimarika kwa uzalishaji nchini kupitia kiwanda cha Unga wa Ngano cha “Zanzibar Milling Corporation” na kufufuliwa Kiwanda cha Sukari cha Mahonda, inajitokeza haja ya kupunguza unafuu unaotolewa kwa uingizaji wa bidhaa hizo muhimu ili viwanda vyetu viweze kuhimili ushindani wa haki. Serikali inakusudia kupunguza unafuu unaotolewa sasa wa ushuru wa uingizaji kwa dhamira ya kuupunguza au kuuondoa kabisa.

VIII.  MWELEKEO WA MATUMIZI

84.      Mheshimiwa Spika, Serikali inakadiria kutumia jumla ya TZS 1,315.1 bilioni katika mwaka wa fedha 2018/19. Matumizi haya yanajumuisha matumizi ya kazi za kawaida ya TZS 702.2 bilioni na matumizi ya kazi za maendeleo ya TZS 613.0 bilioni. Matumizi ya kazi za kawaida yamezingatia matakwa ya misingi ya usimamizi wa fedha kama ilivyo katika Kifungu cha 5(1)(b) cha Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma namba 12 ya mwaka 2016. Kifungu hiki kinaelekeza kuwa katika kipindi cha muda wa kati, matumizi ya kazi za kawaida yasipindukie mapato ya ndani.
85.      Mheshimiwa Spika, katika matumizi ya kawaida, jumla ya TZS 337.1 bilioni zinahitajika kwa ajili ya kulipa mishahara, posho zinazoendana na mishahara pamoja na michango ya lazima, kwa ajili ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF). Katika mwaka huo, kiasi cha TZS 15 bilioni zimetengwa kwa ajili ya nyongeza za mwaka, upandishaji vyeo na ajira mpya. Kiasi hicho ni sawa na asilimia 41.7 ya mapato ya ndani na hivyo kimezingatia matakwa ya Kifungu cha 5(1)(d) cha Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma kinachokataza matumizi ya mishahara na maslahi kwa wafanyakazi wa umma kuwa makubwa kwa kuzingatia uwezo wa kuchumi.
86.      Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mapato ya ndani yanayotarajiwa ya jumla ya TZS 807.5 bilioni, matumizi hayo kwa ajili ya mishahara yataacha salio la TZS 470.6 bilioni kwa ajili ya matumizi mengine. Aidha, kati ya jumla ya mapato hayo yanayotarajiwa kutokana na vyanzo vya ndani, yamo mapato yaliyokasimiwa matumizi maalum na hivyo kutoweza kugawanywa kwenye matumizi mengine.
87.      Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2018/19, mapato hayo yenye matumizi maalum yanatarajiwa kufikia TZS 97.5 bilioni kama ifuatavyo:
i.                   Fedha maalum zilizotengwa kwa ajili ya Mfuko wa Miundombinu, TZS 39.4 bilioni;
ii.                 Asilimia 5 ya makusanyo inayobaki ZRB sawa na TZS 20.3 bilioni;
iii.              Makusanyo kwa ajili ya Mfuko wa Barabara TZS 15.8 bilioni;
iv.              Ada ya Bandari kwa mchango wa madawati inatarajiwa kuwa ni TZS 1.0 bilioni;
v.                 Ada ya Kuendeleza Ujuzi (SDL), TZS 13.8 bilioni;
vi.              Marejesho kwa Idara ya Uhamiaji Zanzibar ya TZS 6.5 bilioni sawa na asilimia 25 ya makusanyo yao; na
vii.            Ada ya Usalama ya Uwanja wa Ndege kwa ajili ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege TZS 650 milioni.
88.      Mheshimiwa Spika, baada ya kuondoa kiasi hicho cha TZS 97.5 bilioni zinabaki jumla ya TZS 373.1 bilioni ambazo ndio zinagaiwa kwa ajili ya matumizi ya kuendeshea Serikali (Other Charges), Ruzuku kwa Taasisi mbalimbali na kazi za maendeleo. Ugawaji wa fedha hizo umezingatia mambo ya ziada yafuatayo:
                  i.    Kuendeleza utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015;
            ii.        Maeneo ya vipaumbele vya Taifa kwa mwaka 2018/19 kama nilivyovibainisha wakati nikiwasilisha Mpango wa Maendeleo leo asubuhi; na
          iii.        Maagizo Maalum ya Serikali kwa mujibu wa vipaumbele vya Taifa yakiwemo ya kutoa Elimu bure hadi Sekondari na kuongeza Bajeti ya Dawa na Vifaa tiba kama nitakavyoeleza baadae.
89.      Mheshimiwa Spika, zaidi ya vigezo nilivyovitaja, ugawaji wa fedha za maendeleo kwa mwaka 2018/19 umezingatia mambo ya ziada yafuatayo:
               iv.    Programu na miradi ya kimkakati (Flagship Projects) iliyotajwa katika MKUZA III;
                 v.    Programu na miradi yote ambayo Serikali ina dhima (Commitment) kutoka kwa Washirika wa Maendeleo;
               vi.    Programu na miradi yote iliyokuwa haijakamilika utekelezaji wa shughuli zake kwa bajeti ya mwaka 2017/18;
             vii.    Miradi inayogharamiwa kupitia Mfuko wa Miundombinu.

a.   Matumizi ya Mfuko wa Miundombinu

90.      Mheshimiwa Spika, kwa upande wa matumizi, jumla ya TZS 39.4 bilioni zimekadiriwa kutumika katika kugharamia Miradi maalum ya maendeleo hususan miradi ya kuimarisha Miundombinu. Miradi inayotarajiwa kugharamiwa na Mfuko huo kwa mwaka 2018/19 ni kama ifuatavyo:
91.      Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia jumla ya matumizi ya TZS 1,315.1 bilioni, mapato ya ndani ya TZS 807.5 bilioni na Misaada kutoka nje ya TZS 464.2 bilioni pamoja na Mfuko wa Wafadhili (Basket Fund) wa TZS 3.4 bilioni, kunajitokeza matumizi kuzidi mapato kwa TZS 40 bilioni. Nakisi hiyo inaombwa kuzibwa kupitia Mikopo ya ndani.

IX.       MAENEO MENGINE MUHIMU YALIYOZINGATIWA

92.      Mheshimiwa Spika, katika mgawanyo wa rasilimali, maeneno mengine muhimu yaliyozingatiwa ni pamoja na haya yafuatayo:

a.   Maendeleo ya Kiuchumi

93.      Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio yetu makubwa katika kukuza uchumi wetu na hatimae ukuaji huo kupelekea maendeleo ya watu wetu, bado tuna kazi kubwa sana mbele yetu kufikia katika maisha bora ya wananchi ambayo Serikali ya CCM ingependa kuyaona. Tunaendelea kushuhudia Sekta za kisasa zikichukua nafasi ya Sekta za asili kama vile Kilimo lakini bado kasi ya mageuzi hayo inahitaji kuimarishwa zaidi. Mchango wa Sekta ya Kilimo katika Pato letu la Taifa kwa mwaka 2017 ni asilimia 27. Pamoja na dhamira ya kukiimarisha Kilimo ili kiwe cha kisasa na chenye tija, Sekta ya Viwanda na Huduma zinapaswa kuimarishwa ili zitoe mchango mkubwa zaidi katika uchumi wetu.
94.      Mheshimiwa Spika, kwa mwaka ujao wa Fedha, sambamba na kuendeleza jitihada za kushajiisha uwekezaji zaidi binafsi katika uzalishaji viwandani, Serikali inatarajia kuanza ujenzi wa Eneo moja la Viwanda (Industrial Park) na eneo la kuimarisha wazalishaji wadogo wadogo. Aidha, hatua maalum za kuyaimarisha maeneo ya kusarifu mazao ya Kilimo ya Kizimbani (Unguja) na Pujini (Pemba) zitachukuliwa.
95.      Mheshimiwa Spika, Nia ya Serikali ni kuwa maeneo hayo yatumiwe na Wananchi pale wanapohitaji kusarifu na kuongeza thamani kwenye mazao yao. Utaratibu huu unatarajiwa kuharakisha usarifu wa mazao kwa kuondoa kikwazo cha gharama kubwa za kuwekezwa katika ujenzi wa viwanda. Kila mwenye kuhitaji kusarifu mazao yake atakuwa na fursa ya kuyapelekea kwa ajili ya kusarifiwa.

b.   Ajira

96.      Mheshimiwa Spika, eneo jengine linalopewa mkazo maalum na Serikali ni upatikanaji wa ajira kwa vijana wetu. Sio siri kuwa nchi nyingi zinazoendelea hasa za kusini mwa Jangwa la Sahara, ikiwemo Zanzibar, zina changamoto kubwa ya kushajiisha upatikanaji wa ajira kwa nguvu kazi yake, hususan vijana. Matokeo ya Utafiti wa Nguvu kazi wa mwaka 2014 yalionesha kuwa kiwango cha ukosefu wa ajira Zanzibar ni asilimia 14.3, na tatizo likijokeza zaidi kwa Vijana.
97.      Mheshimiwa Spika, kwa Vijana wa umri wa miaka 15 hadi 24, ukosefu wa ajira umepanda kutoka asilimia 17.9 mwaka 2006 hadi asilimia 27. Hata hivyo, kwa kundi la vijana wa miaka 15 hadi 35, mafanikio yamepatikana kwa kupungua ukosefu wa ajira kutoka asilimia 31.3 mwaka 2006 hadi asilimia 21.3 mwaka 2014. Pamoja na mafanikio hayo, kiwango hicho bado ni kikubwa na kinahitaji juhudi maalum za kurekebisha.
98.      Mheshimiwa Spika, tatizo hili linachangiwa zaidi na uchache wa nafasi za ajira zinazojitokeza kila mwaka ikilinganishwa na mahitaji kutokana na wahitimu wanaomaliza masomo katika ngazi mbalimbali. Ili kurekebisha hali hiyo, Serikali itachukua jitihada mbalimbali zikiwemo hizi zifuatazo:
a)         Kuendeleza juhudi za kushajiisha uwekezaji binafsi nchini;
b)        Kuendelea kukuza ujuzi wa vijana wetu na kuwapatia elimu bora ili waweze kuajirika;
c)         Kuimarisha mafunzo ya Ujasiriamali na amali ili vijana wengi zaidi waweze kujiajiri na kuajiri wenzao;
d)        Kupitia upya utaratibu wa utoaji wa vibali vya Kazi ili kuimarisha udhibiti kwa kuhakikisha kuwa wanaopatiwa vibali hivyo ni wale tu wanastahiki na kwa nafasi ambazo vijana wa Kizanzibari hawana ujuzi wa kuzifanya; na
e)         Kuendelea kuajiri vijana kwa kujaza nafasi Serikalini zinazojitokeza kwa wengine kustaafu au mahitaji mapya.
99.      Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada hizo, kuanzia mwaka ujao wa Fedha, Serikali imeamua kuanzisha Programu Maalum ya Ajira kwa Vijana. Lengo la Programu hiyo ni kuwasaidia vijana kuweza kujiajiri wenyewe kwa kuwapatia mitaji kwa mapendekezo yao ya miradi katika sekta tofauti. Kwa kuanzia, Serikali imetenga TZS 3.0 bilioni kwa ajili ya Programu hiyo. Mazungumzo yanaendelea na Benki ya Dunia kuangalia uwezekano wa kupatikana fedha zaidi kwa Programu hiyo. Programu hiyo inatarajiwa pia kunufaika na matokeo ya mazungumzo yanayoendelea na nchi ya Abu Dhabi kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu ambayo imeahidi kusaidia jitihada za Serikali za kuleta ajira kwa vijana kupitia Mfuko wake wa Khalifa (Khalifa Fund). Ahadi hiyo ni matokeo ya ziara ya kufana na kidugu ya Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein katika Falme hizo za Kiarabu.

c.   Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia

100.  Mheshimiwa Spika, kama tunavyofahamu, nchi yetu ipo katika harakati za utafutaji wa maliasili za Mafuta na Gesi. Maelezo ya kina yametolewa na Mheshimiwa Waziri anaesimamia Sekta hiyo muhimu. Miongoni mwa mambo yaliyokwishafanyika ni pamoja na haya yafuatayo:
a)           Kutungwa kwa Sheria ya Mafuta na Gesi namba 6 ya mwaka 2016;
b)            Kuanzishwa kwa Mamlaka ya Kusimamia Shughuli za utafutaji na undelezaji wa Mafuta na Gesi (ZPRA);
c)           Kuanza kazi za utafutaji wa rasilimali hiyo kwa kutumia ndege, meli na vifaa vya nchi kavu katika Kitalu cha Pemba/Zanzibar kwa mashirikiano na Kampuni ya Rak Gas kutoka Ras Al Khaimah. Tayari kazi hizo zimekamilika isipokuwa utafutaji wa mafuta katika nchi kavu kwa kisiwa cha Pemba ndio unaendelea; na
d)          Kutenga eneo la Mangapwani kwa ajili ya ujenzi wa Bandari ya Mafuta na Gesi na Huduma nyengine muhimu.
101.  Mheshimiwa Spika, kwa mwaka ujao wa fedha jitihada hizo zitaimarishwa zaidi kwa kuendeleza kazi ya utafutaji wa mafuta katika Kitalu hicho na kutafsiri taarifa zilizokwishakusanywa. Aidha, Serikali imetenga TZS 5.0 bilioni kwa ajili ya kuanza kazi ya uwekaji wa miundombinu ya msingi katika eneo la Mangapwani. Kazi hizo ni pamoja na ujenzi wa barabara, usogezaji wa umeme na maji.
102.   Mheshimiwa Spika, kwa upande mwengine, eneo hili la kiuchumi ni jipya kwa hapa kwetu na lina mahitaji maalum ya utaalamu na uzoefu katika fani mbalimbali zinazohusiana na mambo hayo. Kwa kuzingatia uhaba mkubwa wa utaalamu, hatua ambazo Serikali inachukua kujenga haraka utaalamu ni pamoja na hizi zifuatazo:                
a)           Kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, imetoa kipaumbele katika kudhamini wataalamu wanaosomea fani mbalimbali zinazohusiana na Mafuta na Gesi;
b)            Katika mikataba ya Ubia wa Mafuta (Petroleum Sharing Agreements – PSA), kunatarajiwa kuwa na kiwango maalum kwa ajili ya Kampuni hizo kutoa fedha za mafunzo ya wataalamu wazalendo; na
c)           Kwa mwaka 2018/19, Serikali pia imetenga TZS 1.0 bilioni kwa madhumuni ya kuharakisha ujenzi wa utaalamu huo.

d.  Miundombinu na Huduma za Jamii

103.  Mheshimiwa Spika, mara nyingi nimekuwa nikieleza umuhimu ambao Serikali inaweka katika kuendeleza miundombinu na huduma muhimu za Elimu na Afya. Kwa mwaka ujao wa fedha, Sekta hizi tatu zimetengewa jumla ya TZS 487.5 bilioni ambapo Afya ni TZS 93.3 bilioni, Elimu na mafunzo ya Amali TZS 179.6 bilioni na ujenzi, Miundombinu na Usafirishaji TZS 214.6 bilioni.
104.  Mheshimiwa Spika, kuhusu Elimu, baada ya mafanikio yaliyopatikana kwa kusajili wanafunzi wengi zaidi katika Skuli za Maandalizi na Msingi baada ya Serikali kufuta michango ya wazazi katika elimu ya ngazi hizo, kuanzia mwaka ujao wa Fedha Serikali itafuta rasmi michango katika elimu ya Sekondari. Hatua hii inaendana na dhamira ya Mapinduzi yetu matukufu ya Januari 1964 yaliyopelekea huduma ya elimu nchini kutangazwa kutolewa bila ya malipo, bila ya ubaguzi kwa watoto wote.
105.  Mheshimiwa Spika, Uwekezaji huu muhimu katika kukuza watoto wetu utanufaisha watoto 256,048 wa elimu ya msingi na watoto 122,163 wa elimu ya Sekondari kwa Takwimu za mwaka 2017. Serikali pia itaelekeza jitihada zake katika kuimarisha ubora wa elimu na matokeo ya wanafunzi. Jitihada hizi zitapata msukumo zaidi kutokana na mashirikiano na Washirika wa Maendeleo hususan Benki ya Dunia na mashirika mengine ya Kimataifa.
106.  Mheshimiwa Spika, eneo jengine muhimu kwa maisha ya kila mwanaadamu ni siha, inayotokana na lishe bora, upatikanaji wa maji safi na salama, kuishi katika mazingira mazuri na kwa kuzingatia tabia njema kama vile kufanya mazoezi, na upatikanaji wa huduma bora za afya. Serikali inachukua hatua mbalimbali katika kuimarisha mambo yote hayo kama zilivyoelezwa kwa kina na Waheshimiwa Mawaziri wanaosimamia Sekta hizo.
107.  Mheshimiwa Spika, kuhusu huduma za afya, kama nilivyotangulia kusema Sekta hii imetengewa jumla ya TZS 93.3 bilioni mwaka ujao wa fedha. Moja ya eneo muhimu lililopewa mazingatio maalum ni upatikanaji wa dawa za lazima na vifaa tiba. Itakumbukwa kuwa hadi kwenye mwaka 2014, tulikuwa tukitegemea sana wafadhili hasa ndugu zetu wa Denmark kupitia Shirika lao la DANIDA na wa Marekani kupitia Shrika la USAID. Serikali ilifanya uamuzi makhsusi wa kupunguza kutegemea washirika wa maendeleo kwa upatikanaji wa dawa za lazima kwa Wananchi na hatua kwa hatua kuchukua yenyewe jukumu hili muhimu.
108.  Mheshimiwa Spika, Sambamba na uamuzi huo, Bajeti ya dawa muhimu na vifaa tiba kutokana na fedha za ndani za SMZ imeongezeka awamu kwa awamu kutoka TZS 500 milioni mwaka 2014/2015 hadi kufikia TZS 8.0 bilioni mwaka huu unaomalizika. Serikali kupitia Wizara ya Afya imefanya uchambuzi wa kina wa mahitaji ya dawa za lazima na vifaa tiba na kubainisha kuwa jumla ya TZS 12.7 bilioni zinahitajika kila mwaka kwa kukidhi mahitaji hayo.
109.  Mheshimiwa Spika, nina furaha kulijuilisha Baraza lako tukufu kuwa kwa mwaka ujao wa fedha, Serikali imeongeza tena bajeti ya dawa na vifaa tiba na kutenga kiasi hicho cha TZS 12.7 bilioni katika Bajeti ya Wizara ya Afya ili kukidhi mahitaji ya dawa za lazima kwa wananchi katika hospitali zetu. Ni jukumu letu sote sasa kuhakikisha kuwa dawa hizo zinanunuliwa kwa wakati, zinapatikana kwa wenye mahitaji na zinatumiwa vyema na wanaopatiwa. Kinyume cha hayo, fedha nyingi zinazotumiwa na Serikali zitakuwa zinapotea bila ya malengo yaliyokusudiwa.
110.  Mheshimiwa Spika, katika Hotuba yangu ya Bajeti ya mwaka jana nilieleza juu ya Mpango wa Serikali wa kuanza kutekeleza mageuzi ya Serikali za Mitaa kwa lengo la kuongeza uwajibikaji wa umma kwa wananchi na kusogeza huduma muhimu karibu yao. Nilibainisha kuwa majukumu yatakayohamishwa kutoka Serikali Kuu kwenda Serikali za Mitaa (ugatuzi) ni pamoja na Huduma za msingi za afya, elimu ya maandalizi na msingi na huduma za ugani na usimamizi wa madiko katika Sekta ya Kilimo na Uvuvi.
111.  Mheshimiwa Spika, mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa mageuzi hayo umeonesha matumaini mazuri na pia kubainisha kazi kubwa iliyo mbele yetu katika kuhakikisha kuwa lengo la mageuzi hayo linafikiwa. Kwa mwaka ujao wa fedha hatua zaidi zitachukuliwa katika kuimarisha mageuzi hayo kwa maeneo ya kuanzia. Hatua hizo ni pamoja na kuhamisha wafanyakazi wa maeneo hayo kutoka Serikali Kuu na kuhamishia Serikali za Mitaa sambamba na kuhamisha gharama zao za mishahara, maposho na likizo. Serikali itaimarisha pia uratibu wa mageuzi haya na kukabiliana na changamoto zozote zitakazojitokeza.

X.          SURA YA BAJETI

112.  Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia hali ya mapato na matumizi niliyokwisha yaeleza hapo juu, Bajeti ya mwaka 2018/19 inatarajiwa kuhusisha mapato ya jumla ya TZS 1,275.1 bilioni. Kati ya fedha hizo:
a.   Mapato ya ndani ni TZS 807.5 bilioni; na
b.  Ruzuku na Mikopo kutoka nje ni TZS 464.2 bilioni
c.   Ruzuku ya TZS 3.4 bilioni ya Mfuko wa Wafadhili (BF).
113.  Mheshimiwa Spika, kwa upande wa matumizi, jumla ya TZS 1,315.1 bilioni zinatarajiwa kutumika kama ifuatavyo:
i.       Matumizi ya Kazi za Kawaida TZS 702.1 bilioni, na
ii.     TZS 613.0 bilioni kwa kazi za Maendeleo.
114.  Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia mapato ya TZS 1,275.1 bilioni na matumizi ya TZS 1,315.1 bilioni, kunajitokeza nakisi ya TZS 40.0 bilioni. Inapendekezwa kuwa nakisi hiyo izibwe kwa kukopa kiasi hicho cha fedha kutoka soko la ndani.
115.  Mheshimiwa Spika, kwa sura hii ya Bajeti, kunajitokeza taswira ifuatayo:
i.            Mapato yetu ya ndani ya TZS 807.5 bilioni yatakidhi haja ya kugharamia matumizi yetu yote ya kazi za kawaida ya jumla ya TZS 702.1 bilioni;
ii.          Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo utagharamiwa na vyanzo vifuatavyo vya fedha:
a)   Mapato ya Ndani ya TZS 69.4 bilioni;
b)  Mfuko wa Miundombinu TZS 39.4 bilioni;
c)   Mikopo kutoka nje TZS 388.6 bilioni;
d)  Ruzuku kutoka nje TZS 75.6 bilioni, na
e)   Mikopo ya Ndani ni TZS 40.0 bilioni.
Sura kamili ya Bajeti kwa mwaka 2018/2019 inaonekana katika jadweli hapa chini.
Chanzo: Wizara ya Fedha na Mipango, Zanzibar
116.  Mheshimiwa Spika, itakumbukwa kwamba katika Bajeti tunayoendelea nayo, tulitoa taarifa ya kupungua kwa utegemezi wa Bajeti kwa ruzuku kutoka nje kutoka asilimia 11.1 mwaka 2016/17 hadi asilimia 7.3 mwaka 2017/18. Kutokana na mchango wa Ruzuku ya TZS 75.6 bilioni katika Bajeti ya TZS 1,315.1bilioni ya mwaka 2018/19, utegemezi wa Bajeti unatarajiwa kushuka zaidi na kufikia asilimia 5.7 tu. Haya ni mafanikio mengine makubwa tunayoendelea kuyapata ambayo yanapaswa kudumishwa.

XI.       SHUKRANI

117.  Mheshimiwa Spika, nna deni kubwa kwa viongozi na watendaji wote walioshiriki katika uandaaji wa Makadirio haya ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2018/19. Uwasilishaji huu usingewezekana leo hii bila ya mchango mkubwa wa maelekezo, miongozo na mawazo ya watu mbalimbali, Serikalini na katika Sekta binafsi. Kwa ujumla wao, naomba uniruhusu niwashukuru sana wote kwa namna walivosaidia na kufanikisha mimi leo hii kutimiza wajibu wangu wa Kikatiba kwa dhamana niliyopewa ya Uwaziri wa fedha na Mipango. Naomba uniruhusu niwataje wachache.
118.  Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nishukuru sana maelekezo na miongozo ya Mheshimwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Dira na upeo wa kuona mbali kwa Mheshimiwa Rais, na utayari wake wa kutuongoza bila ya kinyongo na khiana na uzoefu wake mkubwa katika uongozi wa Serikali ni faraja kubwa kwetu sote na kwangu mimi binafsi.
119.  Mheshimiwa Spika, kwa kauli hiyo hiyo, namshukuru sana msaidizi wake mkuu, makamu wa pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi nae kwa kutusimamia na kutuelekeza bila ya kuchoka. Tunajifunza mengi kutoka kwao, muda wote. Shukran hizi pia ni kwa Baraza la Mapinduzi na Wajumbe wake wote. Utulivu tunaoupata Wizarani na msaada mkubwa wakati wa maandalizi ya Makadirio haya hauwezi kwenda bila ya kutambua na kuthamini mashirikiano ya Waheshimiwa Mawaziri, Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu na Manaibu Waziri wote.
120.  Pili, Mheshimiwa Spika, ni wewe binafsi Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid, Naibu wako Mheshimiwa Mgeni Hassan Juma na Wenyeviti Mheshimiwa Shehe Hamad Mattar na Mheshimiwa Mwanaasha Hassan Juma. Tunaelewa kazi ngumu ya kuliongoza Baraza hili. Uweledi wenu umesaidia sana kuleta utulivu wa Baraza kwa kusimamia wananchi wakiwakilishwa vyema na Wawakilishi wao, Waheshimiwa Wawakilishi wakiiisimamia vyema Serikali na Serikali ikiwajibika kwa Wananchi kupitia chombo hichi adhimu. Hakika hii si kazi nyepesi lakini mnaimudu na kuitekeleza vyema.
121.  Mheshimiwa Spika, tatu, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Mohammed Said (Dimwa) na Waheshimiwa Wajumbe wote wa Kamati ya Kudumu ya Bajeti ya Baraza lako hili. Tunapata na kuthamini sana mashirikiano makubwa kutoka Kamati na Mwenyekiti wake. Miongozo na michango yao siku zote inaibua fikra mpya na za kimaendeleo na tumekuwa tukiipokea na kuifanyia kazi kwa dhati. Kwa uzito huo huo tunashukuru msaada na uelewa mkubwa wa Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo na Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC). Tunafanya kazi na Kamati zote hizi, na nyengine zote, kwa maelewano yasioathiri majukumu ya kila upande.
122.  Mheshimiwa Spika, wapishi wa chakula chetu hiki kizuri cha Makadirio ya Bajeti ni Watendaji. Naomba kumshukuru kwa dhati Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Abdulhamid Yahya Mzee, Makatibu Wakuu na watendaji wote walioshiriki katika maandalizi ya bajeti hii. Michango na upeo wao umesaidia sana kuyaweka sawa makadirio haya na hivyo kuwezesha kuwasilishwa Barazani leo hii.
123.  Mheshimiwa Spika, pamoja na wote hao, bado kazi kubwa ya uandaaji wa Makadirio haya imefanywa na Watendaji wa Wizara yangu, ya Fedha na Mipango wakiwemo wa Tume ya Mipango. Nathamini na kushukuru sana uongozi na msaada mkubwa wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bwana Khamis Mussa Omar, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango - Bwana Juma Hassan Reli, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango - Bwana Iddi Haji Makame, Mhasibu Mkuu wa Serikali- Bi Mwanahija Almas Ali, na Kamishna wa Bajeti – Bwana Mwita Mgeni Mwita. Kupitia kwao, nawashukuru sana watendaji wote wa Wizara, Tume ya Mipango na Taasisi zilizo chini ya Wizara hususan, kwa mnasaba wa Mapendekezo haya, Mamlaka ya Mapato (TRA) na Bodi ya Mapato (ZRB).
124.  Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kushirikiana na Mataifa na Mashirika mbalimbali. Kwa namna moja au nyengine, mashirikiano hayo yamesaidia sana katika kuharakisha maendeleo yetu. Kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi, natoa shukran za dhati kwa nchi za Canada, China, Cuba, Denmark, Falme za Kiarabu, Finland, India, Ireland, Japan, Korea ya Kusini, Kuwait, Marekani, Misri, Norway, Oman, Saudi Arabia, Sweden, Ubelgiji, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani na Uturuki.
125.  Mheshimiwa Spika, aidha, nashukuru sana msaada na mashirikiano na mashirika ya: ACBF, ACCRA, AfDB, AGRA, BADEA, CARE INTERNATIONAL, CDC, CHAI, CIDA, DANIDA, DFID, EGH, EU, EXIM Bank ya China, EXIM Bank ya Korea, FAO, FHI, GAVI, GEF, GLOBAL FUND, IAEA, ICAP, IDB, IFAD, ILO, IMF, IPEC, JICA, JSDF, KOICA, MCC, NORAD, OFID, ORIO-Netherlands, PRAP, SAUDI FUND, Save the Children, SIDA, UN AIDS, UN, UNDP, UNESCO, UNFPA, UN-HABITAT, UNICEF, UNIDO, USAID, WB, WHO na WSPA.
126.  Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie kwa kutoa shukran maalum. Kwanza, kwa wananchi wote wa Jimbo la Donge. Wakati nipo hapa nikitumikia wananchi wote wa Zanzibar, sitosahau Imani kubwa ya Wananchi wa Donge kwangu. Kwa Imani na ridhaa yao ndio walinichagua kuwawakilisha katika Baraza hili tukufu. Pili, ni shukran kwa familia yangu yote. Kutumikia wananchi mara nyengine kunamaanisha sio tu kujitolea kwa muhusika, bali pia kunahitaji ustahamilivu, ufahamu na kujitolea kwa familia nzima. Nashkuru sana uelewa na ustahamilivu mkubwa wa familia yangu na kuniunga mkono muda wote.

XII.    HITIMISHO:

127.  Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema awali, kwa mujibu wa Katiba yetu ya mwaka 1984 na marekebisho yake, jukumu langu kama Waziri mwenye dhamana ya Fedha ni kutayarisha na kuwasilisha makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa mwaka ujao wa Fedha. Kwa sasa, mwaka huo ni mwaka 2018/19. Jukumu la kuidhinisha Makadirio hayo ya Serikali ni la Baraza lako hili la Wananchi.
128.  Mheshimiwa Spika, kwa mnasaba huo, na kwa heshima kubwa, sasa naliomba Baraza lako tukufu liidhinishe Mapendekezo ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2018/19. Serikali inapendekeza kukusanya jumla ya Shilingi Trilioni Moja, Bilioni Mia Tatu na Kumi na Tano na Milioni Mia Moja (TZS 1.3151 Trilioni). Kati ya mapato hayo, mapato ya ndani ni Shilingi bilioni mianane na saba na milioni Mia Tano (TZS 807.5 bilioni) na Ruzuku na Mikopo kutoka Nje ni shilingi bilioni mia nne na sitini na saba na milioni mia sita (TZS 467.6 bilioni) na shilingi bilioni arubaini (TZS 40.0 bilioni) ni mikopo ya ndani.
129.  Mheshimiwa Spika, kwa upande wa matumizi, kwa mwaka huo wa 2018/19, nina heshima ya kuliomba Baraza lako liidhinishe matumizi ya Shilingi Trilioni Moja, Bilioni Mia Tatu na Kumi na Tano na Milioni Mia Moja (TZS 1.3151 Trilioni). Matumizi hayo ni TZS 702.1 bilioni kwa ajili ya kazi za kawaida na TZS 613.0 bilioni kwa utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo.
130.  Mheshimiwa Spika, Naomba kutoa hoja.


Dkt. Khalid S. Mohamed,
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO,
ZANZIBAR.

20 JUNI 2018.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.