Habari za Punde

UEFA: Bao la Mchezaji Cristiano Ronaldo Kushindania Tuzo ya Bao Bora la Msimu Ulaya

Bao lililofungwa na mchezaji wa sasa wa Juventus ya Italia Cristiano Ronaldo limeteuliwa kushindania tuzo ya bao bora la msimu uliopita Ulaya.
Ronaldo alifunga bao hilo la kushangaza la 'bicycle-kick' na kuwasaidia Real Madrid kuwalaza Juventus 3-0 katika mechi ya mkondo wa kwanza ya robofainali katika Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.
Alikuwa pia amefunga bao la kwanza kwenye mechi hiyo na kwa mabao yote mawili aliandika historia.
Kwanza, alifikia krosi ya Isco na kufunga bao la Real la kwanza dakika ya 3 ambapo aliweka historia kwa kuwa mchezaji wa kwanza kufunga mabao katika mechi 10 mtawalia Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Ronaldo alifungaje bao lake?

Dani Carvajal alituma krosi eneo la hatari na Ronaldo akapaa juu angani na kutoa kiki kali ambayo ilimwacha kipa stadi wa Juve Gianluigi Buffon akiwa ameduwaa dakika ya 64.
Bao hilo lilikuwa la ustadi mkubwa kiasi kwamba mashabiki wa Juventus ya Italia, ambao bila shaka walivunjiwa matumaini ya kufika nusufainali na bao hilo, walisimama na kumshangilia Ronaldo.
Meneja wa Real Madrid Zinedine Zidane alivyolipokea bao hilo la pili la Ronaldo ilitosha kufahamu ustadi uliotumiwa.
Alitingisha kichwa chake na kuonekana kupigwa na butwaa usoni, alipindua kichwa upande na kisha kuonekana kulikubali.
Katika maisha yake ya uchezaji alifunga mabao mengi ya kushangaza akiwa Turin mwenyewe, lakini alichokiona kutoka kwa Cristiano Ronaldo kilikuwa cha kipekee.
Ronaldo, 33, alikuwa ameruka juu kana kwamba ni kawaida yake tu na kuutuma mpira kimiani.
Baada ya mpira kutulia kwenye wavu, mashabiki wa Juve walimfuata Zidane na kusimama kumshangilia Ronaldo.
Winga wa zamani wa Scotland ambaye alikuwa akitangazia BBC Radio 5 live alishangazwa pia na Ronaldo.
"Unapoona mpira unaelekea kwake, unafikiria 'Oh, hautajaribu kuupiga mpira huyo kwa kuupitisha juu cha kichwa chako.' Kisha, pa! Unajionea mwenyewe, unatazama."
"Si jambo la kawaida. Watu wanazungumzia jinsi Ronaldo anazeeka sasa - lakini hakuna kasoro yoyote kwenye mwili wake iwapo anaweza kufanya jambo kama hilo. Alipima vyema kabisa, na ubunifu wa kufanya hivyo ni wa kushangaza."

Wengine wanaoshindania tuzo

Kwa jumla, kuna mabao 11 ambayo yanashindania tuzo hiyo, ambapo kuna pia bao alilolifunga Mwingereza Lucy Bronze wa timu ya kinadada ya Lyon ya Ufaransa dhidi ya kina dada wa Manchester City.
Mabao yanayoshindania tuzo hiyo yalifungwa katika kipindi cha miezi 12 iliyopita na yanashirikisha michuano yote ambayo huratibiwa na Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa).
Mchezaji mwingine wa Uingereza Elliot Embleton ameteuliwa kutokana na bao lake alilolifunga hatua ya makundi michuano ya ubingwa wa wachezaji wa chini ya miaka 19 didi ya Uturuki.

Bao la kiungo wa Tottenham Christian Eriksen wakati wa mechi ya muondoano wa kufuzu kwa Kombe la Dunia baada ya hatua ya makundi dhidi ya Jamhuri ya Ireland pia limeorodheshwa kushindania tuzo hiyo.
Lucy Bronze akifunga dhidi ya kina dada wa Manchester City
Bao la Ronaldo limeteuliwa badala ya bao karibu sawa na lake alilolifunga mshambuliaji wa Real Madrid nyota wa Wales Gareth Bale wakati wa ushindi wao Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya dhidi ya Liverpool.

Orodha kamili ya mabao yanayoshindania tuzo

Lucy Bronze (LYON 1-0 Manchester City)

Nusufainali Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya ya Wanawake 29/04/18
Olga Carmona (Uswizi 0-2 UHISPANIA)
Hatua ya makundi ubingwa wa wachezaji wa chini ya miaka 19 ligi ya wanawake 21/07/18

Elisandro (Sporting CP 2-5 INTER FS)

Fainali ya Kombe la Futsal Cup, 22/04/18
Elliot Embleton (Uturuki 2-3 ENGLAND)
Ubingwa wa wachezaji wa chini ya miaka 19 ligi ya wanaume, 17/07/18
Christian Eriksen (Jamhuri ya Ireland 1-5 DENMARK)
Mechi za muondoano Ulaya za kufuzu kwa Kombe la Dunia baada ya hatua ya makundi, 14/11/17

Paulo Estrela (PORTO 5 -1 Beşiktaş)

Ligi ya Vijana hatua ya makundi, 13/09/17

Eva Navarro (Ujerumani 0-2 SPAIN)

Ubingwa wa wachezaji wa chini ya miaka 17 ligi ya wanawake, 21/05/18

Dimitri Payet (MARSEILLE 5-2 Leipzig)

Robo fainali Europa League, 12/04/18

Gonçalo Ramos (Slovenia 0-4 URENO)

Ubingwa wa wachezaji wa chini ya miaka 17 ligi ya wanawake hatua ya makundi, 07/05/18

Ricardinho (URENO 4-1 Romania)

Mechi za Futsal EURO hatua ya makundi, 31/01/18

Cristiano Ronaldo (Juventus 0-3 REAL MADRID)

Robofainali Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya, 03/04/18

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.