Habari za Punde

Dk.Kigwangalla ateta na Mjukuu wa Malkia wa Uingereza, Prince William Dar

Mjukuu  wa Malkia wa Uingereza, Prince William (katikati) akiteta jambo na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla (kushoto) wakati  alipowasili kwenye ofisi ndogo ya wizara hiyo Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Waziri wa Sheria na Katiba, Mhe. Profesa Paramagamba Kabudi.
Waziri wa Maliasili Dkt. Hamisi Kigwangalla akiagana na Mjukuu  wa Malkia wa Uingereza, Prince William katika ofisi ndogo za Wizara hiyo Jijini Dar es Salaam.
Mjukuu  wa Malkia wa Uingereza, Prince William akifanya mazungumzo na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla katika ofisi ndogo za Wizara hiyo Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Balozi wa Uingereza Nchini Bi. Sarah Cooke.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla jana amekutana na kuzungumza na Mjukuu  wa Malkia wa Uingereza, Prince William ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku tatu.
Prince William ambaye aliwasili nchini Septemba 26, 2018 kwa ziara maalum ambapo awali alikutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ikulu ya Magogoni Jijini Dar es Salaam, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na baadae kupokelewa ofisini kwa Waziri w Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla, amesema kuwa amefurahia uwepo wake hapa nchini hali iliyopelekea kukaa kwa muda huo tofauti na Nchi zingine ambazo amekaa kwa siku moja.
Prince William ameweza kumtembelea Dk. Kigwangalla katika ofisi ndogo ya Wizara hiyo Jijijini Dar es Salaam,ambapo katika mazungumzo baina ya wawili hao, ikiwemo suala la kuomba msaada wa kusaidia Sekta ya Utalii.
“Kiukweli tokea kumpokea hapa Nchini alipoingia Septemba 26, Prince William amefurahia na nimeweza kumuomba  msaada wa masuala mbalimbali ya kusaidia Sekta ya Utalii na Uhifadhi wa Nchi yetu kutokana na yeye  kuwa na mapenzi ya kipekee kwenye uhifadhi na pia anakumbukumbu nzuri na Tanzania kiasi cha kukaa siku tatuhapa tofauti na nchi zingine alizokaa siku moja” ameeleza Dkt. Kigwangalla.
Miongoni mwa mambo Waziri Dkt. Kigwangalla aliomba asaidiwe na Prince William ni pamoja na suala la kukijengea uwezo kikosi kazi cha kudhibiti ujangili Nchini hii ni pamojana kusaidia kwenye masuala ya utalaam, zana za kisasa za kiintelijensia na mafunzo.
Pia Dkt. Kigwangalla alimuomba Prince William kusaidia kwenye mradi wa kujenga makumbusho tatu za kuhifadhi  meno ya tembo ambapo Wizara inakusudio la kujenga makumbusho hayo katika Mikoa ya Dodoma, Arusha na Dar es Salaam.
“lengo la kumuomba atusaidie katika kujenga makumbusho ya kuhifadhi meno ya tembo ni kutokana na Tanzania kuwa miongoni mwa nchi za awali tano za Afrika kusaini mpango wa kulinda tembo kule nchini uingereza mwaka 2008.
Ambapo katika progam hiyo, nchi zote ambazo zimesaini, zinajifunga kwa kufanya meno hayo ya tembo yasiweze kutumika tena kibiashara na kiuchumi kwa maana ya kwamba meno hayo hayawezi kuuzwa tena kwa faida za kiuchumi hivyo na sisi tumeamua kuyalinda na kuyahifadhi ili iwe ukumbusho vizazi na vizazi tofauti na nchi zingine ambazo wao waliamua kuziteketeza kwa kuzichoma moto” alieleza Dkt. Kigwangalla.
Aidha, Dkt. Kigwangalla alimuomba Prince William msaada mwingine wa ndege aina ya Helkopta Nne, ikiwemo mbili zitakazokuwa  kwa ajili ya dharura na mbili zingine kwa ajili ya doria kwenye baadhi ya maeneo  ya uhifadhi nchini.
Prince William na ujumbe wake huo umeweza kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi na pia Chuo cha Wanyamapori cha Mweka (College of African Wildlife Management, Mweka (CAWM), kilichopo Moshi, mkoani Kilimanjaro na baada ya hapo ataendelea na ziara yake Nchini Kenya.
Lengo kuu la ziara hiyo ya Prince William ni pamoja na kufuatilia juhudi za kukabiliana na ujangili na uhifadhi wa wanyama ikiwemo tembo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.