HOTUBA YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR, MHE. BALOZI SEIF ALI
IDDI ALIYOITOA
KUAKHIRISHA MKUTANO WA KUMI NA MOJA WA BARAZA LA TISA LA WAWAKILISHI
TAREHE 04 OKTOBA, 2018
Mheshimiwa Spika, Awali
ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu, Mwingi wa Rehma kwa
kutujaalia uhai
na afya njema na kutuwezesha kufanikisha Mkutano huu wa Kumi na moja wa Baraza
la Tisa ulioanza tarehe 19 Septemba, 2018 hadi leo tarehe 4
Oktoba, 2018 tunapouhairisha. Mkutano
ambao tumeweza kujadili kwa kina taarifa za utekelezaji wa maagizo ya Kamati za
Kudumu za Baraza letu Tukufu, kadhalika tumejadili Miswaada mitatu
iliyowasilishwa Barazani pamoja na maswali yaliyoulizwa ambayo yaliweza
kujibiwa kwa ufasaha kabisa.
Kwa ujumla shughuli zote tulizojipangia katika Mkutano huu zimeweza
kukamilika kwa wakati muafaka na kwa ufanisi mkubwa.
Mheshimiwa Spika, Napenda kutoa pongezi
zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein kwa Uongozi wake mahiri na makini wa
kuisimamia vyema Ilani ya Chama cha Mapinduzi pamoja na Serikali yetu ya
Mapinduzi ya Zanzibar. Usimamizi wake huo umetuletea mafanikio makubwa ya
kupigiwa mfano na sote ni mashuhuda wa hayo.
Kadhalika, nampongeza kwa ziara yake ya kikazi nchini Indonesia ambayo
italeta manufaa makubwa ya kuinua uchumi wa nchi yetu katika Sekta ya Uvuvi,
Sekta ya Utalii, Sekta ya Kilimo, Biashara na Viwanda, Afya pamoja na masuala
ya Ushirikiano wa Kidiplomasia ambayo yameimarisha uhusiano wetu baina ya Zanzibar na Indonesia,
ushahidi wa hayo ni mapokezi mazuri aliyoweza kuyapata kutoka kwa ndugu zetu
hao.
Mheshimiwa Spika, Napenda kuchukuwa fursa hii kukupongeza wewe mwenyewe binafsi
Mheshimiwa Zubeir Ali Maulid, Spika wa Baraza letu Tukufu, Naibu Spika
Mheshimiwa Mgeni Hassan Juma pamoja na Wenyeviti wote wa Baraza kwa kuviendesha
vyema vikao vyetu kwa hekima, busara na weledi mkubwa na kukifanya kikao hiki
kumalizika kwa amani, salama na mafanikio makubwa.
Mheshimiwa Spika,
Katika kikao hiki jumla ya maswali ya msingi 154 na maswali ya nyongeza
........yaliulizwa na yalijibiwa na Waheshimiwa Mawaziri. Kadhalika katika mkutano huu jumla ya Miswada
mitatu (3) imejadiliwa na kupitishwa kuwa Sheria na Baraza lako Tukufu. Miswada
yenyewe ni:-
i Mswada wa Sheria ya Kuweka Masharti Bora ya Usimamizi wa Mahakama,
Kufafanua Utumishi wa Mahakama, Kuanzisha Ofisi za Mtendaji Mkuu wa Mahakama na
Mrajis, Kuanzisha Mfuko wa Mahakama na Kuweka Masharti Mengine Yanayohusiana na
Hayo.
ii Mswada wa Sheria ya
Kuanzisha Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Elimu na Kuweka Masharti ya Mkaguzi wa Elimu
Pamoja na Mambo Mengine Yanayohusiana na Hayo.
iii Mswada wa Sheria
wa Kuanzishwa Wakala wa Serikali wa Uchapaji Zanzibar na Kuweka Masharti Bora
Yanayohusiana Na Kazi, Uwezo, Uongozi na Mambo Mengine Yayohusiana na Hayo.
Mheshimiwa Spika, Ni imani yangu kwamba
Miswada hiyo mitatu (3) tuliyoipitisha kwa kauli moja itasaidia kuimarisha
Utawala bora ikiwemo uwajibikaji kwa watendaji wetu ili kukuza uchumi wa nchi
yetu. Waheshimiwa Wajumbe wenzangu, Serikali inaahidi kuwa itaifanyia kazi
michango yenu yote mliyoitoa wakati wa kujadili Miswada hii. Nawaomba wananchi mtoe ushirikiano wenu wa
karibu wakati Miswada hii itakapoanza kuwa Sheria. Tutambue kuwa Sheria siku zote zinatungwa kwa
ajili ya kusimamia haki za wananchi wake kwa maendeleo yao na Taifa lao kwa
ujumla.
Mheshimiwa Spika, Katika mkutano huu, Serikali
iliwasilisha taarifa za Wizara zote za Serikali kuhusu utekelezaji wa maagizo
ya Kamati Saba za Kudumu za Baraza lako Tukufu. Taarifa zenyewe ni kutoka:-
i. Kamati ya Kusimamia Ofisi
za Viongozi Wakuu wa Kitaifa;
ii.
Kamati ya Sheria, Utawala Bora na
Idara Maalum;
iii. Kamati ya Maendeleo ya Wanawake, Habari na
Utalii;
iv. Kamati ya Fedha, Biashara
na Kilimo;
v.
Kamati ya Ardhi na Mawasiliano;
vi.
Kamati ya Ustawi wa Jamii;
vii.
Kamati ya Kuchunguza na Kudhibiti Hesabu za Serikali na Mashirika (PAC);
na
viii.
Kamati ya Bajeti;
Mheshimiwa Spika,
Ninazishukuru Kamati zote
kwa kuzipokea taarifa hizo na Waheshimiwa Wajumbe kupata fursa ya kuzichangia
kwa umakini na uweledi ili kuleta ufanisi wa majukumu yetu. Pia, nawaomba Waheshimiwa Mawazii kuzichukua
hoja zote pamoja na mapendekezo yaliyotolewa na Wajumbe wa Baraza na kuzifanyia
kazi ipasavyo.
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Wawakilishi wenzangu na wananchi wote wa Zanzibar, kwa
mara nyengine tena tunatoa mkono wa pole kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, wanafamilia na Watanzania wote kwa msiba mkubwa wa kuwapoteza
Watanzania wenzetu wapatao 230 kutokana na ajali ya kupinduka kwa kivuko cha
M.V. Nyerere huko Kisiwa cha Ukara, Mkoani Mwanza. Tunamuomba Mwenyezi Mungu aziweke roho za
Marehemu mahala pema peponi na wale wote walioumia wapate nafuu haraka.
Mheshimiwa Spika, uzoefu unaonyesha kuwa ajali nyingi zinazotokea nchini zinatokana na
uzembe na ukiukwaji wa makusudi wa Sheria za Usalama wa vyombo vya usafiri.
Nikiwa Msimamizi Mkuu wa Maafa hapa nchini natoa wito kwa watu wote wenye
kumiliki vyombo vya usafiri kufuata sheria zote za usalama wa abiria ili
kunusuru maisha ya wananchi wetu na mali zao.
Mheshimiwa Spika, Kama tunavyotambua kuwa mvua za Vuli kwa mwaka huu zinategemewa kuanza
kunyesha mwezi wa Oktoba hadi Disemba. Hii ni kwa mujibu wa taarifa kutoka
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Kanda ya Zanzibar. Aidha, mvua tutakazozipata
zinatarajiwa kuwa na kiwango cha wastani hadi juu ya wastani. Kwa hivyo,
tunaomba wananchi kuchukua
tahadhari za hali ya juu ikiwa ni pamoja na kuhama maeneo yote hatarishi,
kuyatunza mazingira yetu, kushirikiana katika usafishaji wa mitaro ya maji
machafu, kufunika karo kwa mifuniko madhubuti, kufuata maelekezo na kanuni zote
za afya kama zinavyoendelea kutolewa na wataalamu wetu. Kadhalika, tunapaswa pia kuwa karibu na
watoto wetu wakati mvua zikiendelea ili kuwanusuru na maafa ya kuzama kwenye
madimbwi au karo na hatimaye kupoteza maisha yao. Hivyo, tukumbuke wahenga
walivyosema “tahadhari kabla l-athari.
Mheshimiwa Spika, Tutambue
kuwa jamii inayowadhalilisha na kuwanyanyasa wanawake na watoto haiwezi kupata
maendeleo endelevu. Hivyo, unyanyasaji na ukatili wa wanawake na watoto
unaoendelea nchini unaweza kutishia amani, kuwakosesha uhuru wanawake na watoto
na kuwapunguzia uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli zao za kijamii na
kimaendeleo.
Mheshimiwa Spika,
Vitendo hivi ni vya kinyama na aibu kwa jamii yetu yenye kufuata mila, silka,
desturi, na utamaduni wa watu wastaarabu. Hivyo, tunaviomba vyombo vyote
vinavyohusika na jamii nzima kuondoa muhali na kuchukua hatua kali za kisheria
bila ya kujali dini, rangi, kabila au cheo cha mtu kwani tukumbuke Zanzibar
bila ya unyanyasaji na udhalilishaji wa wanawake na watoto inawezekana iwapo
kila mmoja wetu atatimiza wajibu wake kwa mujibu wa dhamana aliyopewa.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mara nyengine tena ninawasihi wananchi waachane na kujihusisha katika
Uingizaji, Usambazaji, Uuzaji na Utumiaji wa dawa za kulevya. Sote ni mashahidi wa athari kubwa
zinazosababishwa na dawa za kulevya ambapo kundi kubwa la vijana ambao ndio
nguvu kazi inayotegemewa na Taifa imeathirika na dawa hizo. Serikali inaendelea na jitihada za mapambano
dhidi ya dawa hizo na haitomuonea muhali au aibu mtu yeyote atakayeshindwa
kutekeleza wajibu wake. Zanzibar bila
ya dawa za kulevya inawezekana, tutimize wajibu wetu.
Mheshimiwa Spika, Serikali
inasikitishwa kuona kwamba kuna baadhi ya Watendaji wasiokuwa waaminifu katika
Taasisi zinazoshughulikia masuala ya ardhi ambao hukiuka taratibu za kiutumishi
na maadili ya kazi zao na kuwa ni chanzo cha kusababisha migogoro. Tunashuhudia kuwa kiwanja kimoja kuwa na
nyaraka zaidi ya moja, na baadhi ya watendaji huchelewesha kwa makusudi utoaji
wa hati za viwanja na kuwapa wasiostahiki na kutaka rushwa. Vitendo hivi vinaisikitisha sana Serikali na
kuitia aibu na lawama kwa wananchi wake.
Hivyo, ninawaagiza na kuwakumbusha Viongozi wenye dhamana wasijihusishe
na kadhia hiyo watekeleze na kuwasimamia watendaji walio chini ya dhamana zao,
ili kuwaondolea wananchi usumbufu na kuhakikisha kila mtu anapata haki yake kwa
mujibu wa sheria na taratibu za ardhi.
Mheshimiwa Spika,
Maadili bora kwa
Viongozi wa Umma ni jambo lisiloepukika, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
haitakuwa tayari kuwavumilia viongozi wasio na maadili na kuwajibika ipasavyo
kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.
Nina imani kuwa Serikali iliyopo madarakani inatekeleza Ilani ya Chama
cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020, ukurasa 234 (185) c kimeeleza:-
“ Lengo ni kurejesha dhamira ya kuwa na
Viongozi wanaotumikia umma kwa maslahi ya umma na si viongozi wanaotumikia
ofisi za umma kwa maslahi yao binafsi”
Tunawaomba Viongozi
na Watendaji wote wa Umma wenye kutumia rasilimali za Ofisi za Umma kwa maslahi
yao binafsi waache mara moja na pia naviomba vyombo vinavyohusika, Tume ya
Maadili, ZAECA, Jeshi la Polisi na Vyombo vyengine vyote wasisite kuchukua
hatua kwa watendaji hao ili kulinda na kutetea maslahi ya Taifa.
Mheshimiwa Spika, Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu 11(2) kimeandikwa “Kila mtu anastahiki heshima ya kutambuliwa
na kuthaminiwa utu wake”. Pia Baraza lako Tukufu linaendeshwa
kwa kuzingatia misingi ya utawala bora ikiwemo uwazi, uwajibikaji pamoja na
uhuru wa kuchagua au kuchaguliwa. Naomba nizungumzie kidogo kuhusu uhuru huu wa
kuchagua na kuchaguliwa katika Kamati au mambo mengine ya Baraza, tunategemea
kila mmoja akimthamini na kumuheshimu mwenziwe hivi ndivyo inavyotakiwa na
ndivyo demokrasia ambayo wengi wetu huwa tunaihubiri katika Majimbo yetu.
Mheshimiwa
Spika,
ni jambo lisilopendeza na halikubaliki kidemokrasia kuwekeana chuki miongoni
mwetu kwa sababu ya utekelezaji wa demokrasia hiyo. Nasaha zangu kwenu tuachane na tabia hii ya
kuchukiana na badala yake tujenge mshikamano miongoni mwetu Waswahili wanasema:
“Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu”.
Mafanikio ya Baraza letu na Taifa letu yanategemea umoja na mshikamano
wetu, Waheshimiwa Wajumbe.
Mheshimiwa Spika, siku za hivi karibuni katika Baraza
letu umezuka mtindo wa kuzungumzia mambo binafsi yanayotokea mitaani na
kuyageuza kuwa mambo ya kitaifa. Hali hii hatuwezi tukaichia kuendelea kwani
inawanyima wananchi fursa ya kuzungumziwa mambo yao ya kimaendeleo
yanayowahusu; ambayo yameainishwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Hivyo,
tabia hii itakapoachiwa kuendelea tuelewe kuwa Baraza hili litakosa heshima
machoni mwa wananchi tunaowawakilisha. Nikiwa Kiongozi wa Shughuli za Serikali
ndani ya Baraza hili nasema sitokubali hata kidogo na ni lazima sheria na
taratibu zifuate mkondo wake.
Mheshimiwa Spika, matatizo yote ya nchi yetu au watendaji
wetu tunaweza kuyazungumza kwa kutumia lugha ya kawaida yenye hekma na busara
na ujumbe uliokusudiwa ukafika Serikalini na kuchukuliwa hatua kwa ufanisi
mkubwa. Naomba ieleweke kuwa kuzungumzia jambo lolote lile kwa kutumia lugha
kali na wakati mwengine iliyobeba matusi haimaanishi hata kidogo
unalolizungumzia una uchungu nalo. Na pale unapomtetea mtu kwa kutumia lugha
hii ya ukali au matusi pia haionyeshi hata kidogo unayemtetea unampenda
sana.
Mheshimiwa Spika, ni vyema tukakumbuka mafunzo ya dini
yetu ambapo Mwenyezi Mungu alimwambia Mtume wetu (SAW) katika Suratul Al –
Imran, nanukuu:
“Na
kama ungekuwa mkali na mwenye moyo
mgumu
bila ya shaka (watu) wangekukimbia”
Waheshimiwa
Mawaziri, Wawakilishi Wapendwa na Watendaji wote wa Serikali tutumie lugha
njema yenye busara na hekma katika utoaji huduma kwa wananchi au katika
kukosoa, kushauri au kutekeleza jambo lolote ikiwa Serikalini au katika jamii,
maneno mazuri humtoa nyoka pangoni na pia huleta upendo mapenzi na mshikamano
na kufikia malengo tuliyojiwekea.
Mheshimiwa Spika, Wataalamu wanasema: “A civil servant
isn’t accountable to the legislature and is not in a position to answer
questions. Ministers are responsible and accountable for the affairs of their
Department”. Kwa tafsiri isiyokuwa rasmi mtumishi wa serikali hawajibiki kwa
Baraza hili na hawezi kujibu chochote endapo kutakuwa na maswali. Badala yake
ni Mawaziri ambao wanawajibika kwa matendo yanayofanywa ndani ya Idara
zao. Waheshimiwa Wajumbe wajibu wetu ni
kwenda kwa Waziri husika au vyombo vinavyohusika kisheria na kuelezea matatizo
na kasoro zilizopo pamoja na ushahidi wake katika utoaji wa huduma au utendaji
katika eneo hilo. Naamini Waheshimiwa Wawakilishi, Mawaziri wetu au watendaji
wetu watakusikilizeni, na jambo au tatizo litachukuliwa hatua kwa mujibu wa
sheria na taratibu za nchi zilizopo.
Mheshimiwa Spika,
kabla ya kumalizia hotuba
yangu, napenda kuliweka jambo moja bayana ambapo ni hili la kuwaita baadhi yetu
kuwa ni Wawakilishi wa Jimbo la Ikulu kama alivyoeleza Mhe. Mohamed Said Dimwa
kuwa Ikulu hakuna Jimbo yuko Rais, kwa hiyo, wako Wawakilishi Wateule wa Rais
tu. Waheshimiwa Wawakilishi wa nafasi za Rais kuendelea kusema Jimbo la Ikulu
tunaweza kuwababaisha wananchi.
Mheshimiwa Spika,
kwa mara nyengine
tena, nawashukuru Waheshimiwa Wajumbe
kwa kutumia nafasi yao ya Kidemokrasia ya kuisimamia, kuishauri na kuihoji
Serikali, jambo ambalo limeonesha nia thabiti mliyonayo ya kuitaka Serikali
yenu kuwajibika ipasavyo kwa wananchi wake.
Kadhalika, napenda kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri
kwa kujibu maswali yote mliyoulizwa,
mliweza kuyatolea ufafanuzi ambao uliwanufaisha Waheshimiwa Wajumbe pamoja na
wananchi kwa ujumla. Nawaomba Waheshimiwa Wajumbe tuendelee kupendana,
kuvumiliana na kushirikiana katika kuijenga nchi yetu kiuchumi na kijamii kwani
mshikamano na umoja wetu ndio utakaoivusha nchi yetu kuelekea kwenye maendeleo
endelevu. Aidha, napenda pia kumpongeza
Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ufafanuzi wake alioutoa katika
mambo mbali mbali yaliyohitaji ufafanuzi wa kisheria.
Mheshimiwa Spika, Napenda kuwashukuru wale wote waliotuwezesha kukamilisha shughuli
zilizopangwa kwenye Mkutano huu wa Kumi na Moja wa Baraza la Tisa la
Wawakilishi kwa ufanisi. Pongezi hizo
zaidi ziwafikie Watendaji wote wa Baraza hili la Wawakilishi wakiongozwa na
Katibu, Ndugu Raya Issa Msellem. Ni
ukweli usiofichika kwamba tumeanza vizuri na ninaamini tutaendelea vizuri. Mungu libariki Baraza hili, Mungu zibariki
Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Pia nawapongeza Wakalimani wetu wa lugha ya
alama ambao wamewawezesha Waheshimiwa Wawakilishi wenye ulemavu wa kusikia
kufuatilia yote yaliyokuwa yakiendelea ndani ya Baraza. Vile vile, nawashukuru Wanahabari kwa kufanya
kazi nzuri ya kuwapatia habari wananchi wetu kwa shughuli zote ambazo zilikuwa
zikiendelea kufanyika Barazani hapa.
Mheshimiwa Spika, Mwisho
kabisa kwa mara nyengine tena nikupongeze wewe binafsi, Mhe. Naibu Spika na
Wenyeviti wa Baraza kwa kuliongoza vizuri na kwa ufanisi mkubwa Baraza
hili. Hekima na busara zenu zimesaidia
sana katika kuumaliza mkutano huu kwa salama na amani. Mungu libariki Baraza letu la Wawakilishi,
Mungu Ibariki Zanzibar na watu wake, Mungu Ibariki Tanzania.
Mheshimiwa Spika, Baada ya
maelezo hayo, naomba sasa kwa heshima na taadhima kutoa hoja kwamba Baraza lako
Tukufu liakhirishwe hadi siku ya Jumatano tarehe 28 Novemba, 2018, saa 3.00
barabara za asubuhi panapo majaaliwa.
Mheshimiwa Spika, Naomba
kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment