Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia wakati wa hafla ya Ufungaji wa Maonesho ya Kimataifa ya Utalii Zanzibar yaliofanyika katika Viwanja vya Hoteli ya Kitalii ya Verde Mtoni Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameridhia Maonyesho ya Utalii Zanzibar
yaendelee kufanyika kila mwaka kwa lengo la kuendelea kuitangaza Zanzibar katika
sekta ya utalii.
Dk. Shein alitoa kauli
hiyo huko katika ukumbi wa Hoteli ya Verde, Mtoni, Mjini Zanzibar katika hafla
ya utoaji wa zawadi kwa washindi walioshiriki vyema katika sekta ya utalii
ikiwa ni hatua za kukamilisha Maonyesho ya Utalii Zanzibar ya mwaka 2018
yaliaoza tarehe 17 mwezi huu.
Hafla hiyo iliyokwenda
sambamba na chakula maalum cha usiku ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo
Makamo wa Pili wa rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Mama Mwanamwema Shein, viongozi
mbali mbali wa vyama vya siasa na Serikali pamoja na wadau wa utalii wa ndani
na nje ya Zanzibar.
Katika maelezo yake Rais
Dk. Shein alitamka kuwa ameridhia kuendelea kufanyika kwa Maoyesho ya Utalii
Zanzibar kila mwaka kwani yana umuhimu mkubwa katika kuitangaza sekta ya Utalii
hapa Zanzibar.
Rais Dk. Shein pia,
alisisitiza haja kwa Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale kufanya usajili
katika Maonyesho hayo kwa kutumia njia za kisasa ili kurahisiha zoezi la
shughuli zao hizo.
Aidha, Rais Dk. Shein
alikichangia kikundi cha “City Band” ambacho kilitumbuiza katika hafla hiyo kwa
kukipa TZS Milioni sita 6 ambapo na Mama Mwanamwema Shein kwa upande wake alikichangia
TZS Milioni 4 na kufanya idadi ya TZS Milioni Kumi 10.
Pia, wageni wengine
waalikwa walikichangia kikundi hicho kwa fedha taslim pamoja na huduma mbali
mbali ikiwa ni pamoja na kutoa nafasi kutumbuiza katika hoteli mbali mbali hapa
Zanzibar kwa lengo la kukipa moyo sambamba na kuweza kujiendeleza zaidi.
Akielezea kufurahishwa
na Kikundi hicho, Rais Dk. Shein alitoa pongezo zake kutokana na uwezo mkubwa
wa wanakikundi wa kuimba vizuri pamoja na kupiga ala kwa ustadi.
Pamoja na hayo, Rais Dk.
Shein alitua fursa hiyo kutoa pongezi zake kwa Wizara ya Habari, Utalii na
Mambao ya Kale kwa kufanikisha vyema Maonyesho ya Utalii hapa Zanzibar mwaka
huu sambamba na wale wote waliosaidia kufanikisha hafla hiyo adhimu.
Dk. Shein pia, alitoa
pongezi kwa mmiliki wa Hoteli ya Verde, Said Salim Bakhresa ambaye amejitolea
kufanyika kwa maonyesho katika eneo lake hilo pamoja na hafla hiyo sambamba na
uwamuzi wake wa pekee wa kujenga Hoteli hiyo ya kisasa katika eneo hilo ambalo
hakuna aliyefikiria kuwa eneo hilo inaweza kuejngwa hoteli kama hiyo ya kisasa.
Alisema kuwa jitihada za
mfanya biashara huyo ni kubwa sana na wananchi wa Zanzibar wanafurahishwa na
juhudi zake hizo huku akitoa pongezi kwa wageni waliotoka sehemu mbali mbali za
dunia ambao wamekuja kwa shughuli hiyo maalum ya maonyesho ya mwaka huu hapa
Zanzibar.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein aliwapongeza Washindi wote waliopata zawadi katika hafla hiyo na kuwaeleza
wale ambao mwaka huu wamekosa wasivunjike moyo wajiandae kwa mwakani hasa
ikizingatiwa kuwa tayari amesharidhia kuendelea kufanyika kwa maonyesho hayo na
miaka ijayo.
Katika kuwatia moyo wale
ambao mwaka huu hawakupata nafasi, Rais Dk. Shein alisema kuwa “Mshindi hakati
tamaa, na wale wanaokata tama kamwe hawashindi”, mkahawa bora kwa vyakula vya
asili ambao ni Lukmaan, Mpishi bora ambaye ni Alankalee Mayaven kutoka Hoteli
ya Melia Zanzibar.
Washindi wengine ni
mshindi wa Shirika la ndege la ndani ambapo Coastal Aviation alifanikiwa
kushinda, Shirika la Ndege la Kimataifa ambalo ni Oman Air, Kampuni bora ya
kutembeleza watalii ambayo ni Fishermen
Tours and Travel, Melia Zanzibar iliibuka Hoteli yenye ukumbi bora wa mikutano,
Best Western Plus Zanzibar iliibuka Hoteli inayotoa huduma ya makaaze nei
nafuu.
Aidha, Hoteli bora
katika maeneo ya Mji Mkongwe ni Park Hyatt Zanzibar na Hoteli ya Jaffeji House
& Spa iliibuka mshindi wa Hoteli yenye urembo, Gold Zanzibar Beach House
& Spa iliibuka Hoteli bora yenye fukwe huru na Park Hyatt Zanzibar iliibuka
mshindi wa Hoteli bora yenye kutambulika zaidi, na sehemu yenye urithi ni kisiwa
cha Prison Island na Kampuni bora katika kuiunganisha Zanzibar kama kituo cha
Utalii ni Costal Aviation.
Nae Waziri wa Habari,
Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo alitoa pongezi na shukurani wa
Rais Dk. Shein kwa kuendelea kuipa kipaumbe sekta ya utalii sambamba na juhudi
kubwa anazozichukua katika kuhakikisha sekta hiyo inaimarika hapa nchini.
Alisema kuwa tukio
Maonyesho ya Utalii Zanzibarla mwaka 2018 ni la kwanza kufanyika hapa nchini
ambalo limeweza kuwashirikisha washiriki 152 na kuahidi kuwa endapo litaendelea
washiriki zaidi wataongezeka ambao ni kutoka ndani na nje ya Zanzibar.
Waziri Kombo alitaja idadi
ya waliotembelea katika maonyesho hayo ambao walifikia watu 4020 ambao wengi
wao ni wananchi wa Zanzibar huku akitumia fursa hiyo kumpogeza mfanya biashara
Said Salim Bakhresa kwa ushirikiano wake mkubwa alioonesha katika kufanikisha
maonyesho hayo ya mwaka huu wa 2018 na fursa ya pekee aliyopewa.
Katika maelezo yake,
Waziri Kombo alieleza jinsi ya mambo mbali mbali yaliyofanyika katika maonyesho
hayo zikiwemo semina mbali mbali zilizowashirikisha wadau huku akitoa pongezi
kwa wahisiriki wote wa ndani na nje ya Zanzibar ambapo pia, alipata fursa ya
kutoa zawadi kwa washidi wa pili.
Katika hafla hiyo
kikundi cha “City Band” kilitumbuiza na kuonesha umahiri wake mkubwa wa kuimba
na kupiga ala hali ambayo iliifanya hadhira kushindwa kujizuia kutokana na
nyimbo mwanana na zenye mvuto wa pekee.
Hafla hiyo ilihitimishwa
kwa urushwaji wa fashfash maalum zilizoandaliwa kwa ajili ya shughuli hiyo katika
viwanja vya Hoteli ya Verde ambapo Rais Dk. Shein na viongozi wengine alioambatana
nao walijionea mapambo mbalimbali yaliooneshwa huku waalikwa wengi wakifurahia
tukio hilo.
Rajab Mkasaba,
Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment