Habari za Punde

Marudio ya Mitihani ya kidato cha Pili kuanza tarehe 13/01/19

TAARIFA KUHUSU KUFANYIKA MITIHANI YA KIDATO CHA PILI YA MARUDIO MWAKA 2018

Ndugu Viongozi wa Wizara
Ndugu Waandishi wa Habari,
Ndugu Wananchi, 
Ndugu Walimu na Wanafunzi,
Assalamu Aleykum.

Itakumbukwa kwamba siku ya Jumatatu tarehe 3 Disemba 2018, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ilifuta Mitihani ya Kidato cha Pili kwa wanafunzi wa skuli 189 za Serikali na skuli 60 za binafsi baada ya kugundulika kuwa baadhi ya watu wasiohusika wameipata baadhi ya mitihani kabla ya wakati uliopangwa kufanyika kwa mitihani husika.

Baada ya kufanyika kwa marekebisho yaliyohitajika, Wizara inatangaza rasmi kwamba mitihani ya marudio ya Kidato cha Pili itafanyika kuanzia Jumatatu tarehe 14 Januari, 2019 na kumalizika tarehe 22 Januari, 2019 kwa wanafunzi wa skuli zote za Serikali na Binafsi za Unguja na Pemba.

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali inawataka Walimu wakuu wa Skuli zote husika kufanya maandalizi husika ili kuwezesha kufanyika kwa mitihani hiyo katika hali ya utulivu na usalama.

Wizara inatoa shukurani za dhati kwa walimu kwa kuendelea kuwafundisha na kuwashauri wanafunzi wao katika kipindi hiki cha mpito. Aidha, inawashukuru wazazi na jamii kwa jumla kwa kuwa watulivu na kushirikiana na Serikali katika kuona kwamba haki inatendeka kwa wanafunzi wote wa nchi hii.

Wizara inatoa indhari kwamba katika kipindi cha mitihani ya marudio wanafunzi wasiofanya mitihani na wananchi wasipite katika maeneo ya skuli wakati mitihani inaendelea. Aidha Wizara inazuwia kambi za aina yoyote zinazohusiana na mitihani kuanzia Jumatatu ya tarehe 07/01/2019.

Wizara inawatakia kila la kheri wanafunzi wote waliokutwa na kadhia hii na kuwaombea mafanikio katika mitihani hii ya marudio.

Ahsanteni.

Imetolewa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.