Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akijumuika na Wananchi wa Zanzibar katika dua ya Hitma ya kumuombea Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, iliofanyika katika ukumbi wa Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar leo.
RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein
leo ameongoza hitma ya kumuombea dua Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee
Abeid Amani Karume, iliyofanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui mjini Zanzibar.
Hitma hiyo, ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Rais mstaafu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Pili Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu
wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Sita, Amani Abeid Karume na
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd.
Viongozi wengine waliohudhuria katika hitma hiyo ni Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar
Kabhi, Naibu Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Hassan Othman Ngwali, viongozi wa
serikali zote mbili na viongozi wastaafu, viongozi wa vyama vya siasa, Masheikh
kutoka Zanzibar na Tanzania Bara, Wabunge na Wawakilishi, wananchi kutoka maeneo
mbali mbali pamoja na Mabalozi wadogo waliopo hapa Zanzibar.
Hitma hiyo ya kumuombea dua Marehemu Mzee Abeid Amani
Karume ambapo pia, ni miongoni mwa
maadhimisho ya Siku ya Mashujaa ilitanguliwa na Qur-an tukufu, iliyosomwa na
Ustadh Sharif Muhidin pamoja na hitma iliyohitimishwa na Sheikh Jafar Abdallah kutoka
Masjid Noor Muhammad.
Mara baada ya hitma hiyo, Sheikh Fadhil Suleiman Soraga alitoa
mawaidha na kumuelezea marehemu Mzee Abeid Amani Karume kuwa ni kiongozi
aliyepigania maendeleo ya wananchi wa Zanzibar na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu
ampe makaazi mema Peponi.
Katika mawaidha hayo, Sheikh Soraga alisisitiza haja ya
kuendeleza na kudumisha amani na utulivu uliopo ikiwa ni miongoni mwa misingi
madhubuti iliyoachwa na muasisi wa Mapinduzi Marehemu Sheikh Abeid Amani
Karume.
Aliongeza kuwa hadhara hiyo iliyohudhuria katika kisomo
hicho huko katika Ofisi za CCM Kisiwandui mjini Zanzibar ni udhibitisho wa wazi kuwa Wazanzibari na
Watanzania wote kwa jumla wanathamini na wanatambua yale yoteyaliyofanywa na
Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume.
“Yeye ndio mkombozi wetu kwani amefanya mambo mengi na
sote tuko tayari kushuhudia mema yote
aliyoyafanya hapo siku ya kiama itakapofika mbele ya Mwenyezi Mungu (S.W)”alisisitiza
Sheikh Soraga.
Baada ya kisomo hicho cha hitma ambacho hufanyika kila
mwaka inapofika tarehe 7, Aprili, viongozi hao na wananchi waliohudhuria katika
hitma hiyo walimuombea dua, marehemu mzee Abeid Karume katika kaburi lake
lililopo pembezoni mwa afisi Kuu ya CCM Kisiwandui.
Dua hiyo iliongozwa na viongozi wa dini tofauti akiwemo
Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Omar Kabhi kwa upande wa dini ya Kiislamu pamoja
na Askofu Charles Lundu kutoka Kanisa la
Anglikana Zanzibar.
Viongozi na wanafamilia waliweka mashada ya maua katika
kaburi la marehemu mzee Abeid Amani Karume akiwemo Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Mzee Hamad Ussi Haji aliyeweka
shada la maua akiwawakilisha wazee wa CCM.
Wengine walioweka mashada ya maua ni Meja Jenerali Sharif
Sheikh Othman aliyeweka shada la maua kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya
Tanzania Jenerali Venance Salvatory Mabeyo, Balozi Ali Karume aliyeweka kwa
niaba ya familia ya Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume na Balozi mdogo wa Msumbiji
anayefanya kazi zake hapa Zanzibar Jorge Augusto Menezes aliyewawakilisha Mabalozi wenzake wa
hapa nchini.
Aidha, Mama Mwanamwema Shein aliungana na akina mama
wengine katika hitma hiyo iliyofanyika katika Afisi ya CCM Kisiwandui, akiwemo mjane
wa marehemu mzee Abeid Karume, Mama Fatma Karume, Mama Shadya Karume na viongozi wengine
wanawake wa kitaifa wakiwemo Mawaziri, Wabunge, Wawakilishi, viongozi wakuu wa
vyama vya siasa na wananchi kutoka maeneo mbali mbali ya Zanzibar na Tanzania
Bara.
April 7, 1972 ndiyo siku aliyouawa Rais wa Kwanza wa
Zanzibar marehemu Mzee Abeid Amani Karume na wapinga maendeleo nchini ambapo hivi
leo imetimia miaka 47 tokea utokee msiba huo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment