Habari za Punde

Balozi Seif ziarani Shinyanga

 Mke wa Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga Kichama Mama Asha Suleiman Iddi akimkabidhi Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Halmashauri ya  Kahama Mji Dr. George Masasi Baskeli ya kubebea Wagonjwa kwa ajili ya Hospitali hiyo.
Wa Kwanza Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Zainab Rajab Telak.
 Mama Asha Kushoto akimkabidhi Dr. George Masasi Mashuka kwa ajili ya Vitanda vya Wagonjwa wanaolazwa katika Hospitali hiyo ya Halmashauri ya Kahama Mji.
 Mama Asha akiwakabidhi akina Mama waliojifungua kwenye Hospitali ya Halmashauri ya Kahama Mji Doti za Kanga kwa ajili ya kuwahifadhi na Baridi Watoto wao.
 Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga Balozi Seif Ali Iddi akiweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Jengop Jipya la Tawi la CCM la Kijiji cha Buganzo ndani ya Jimbo la Msalala Wilaya ya Kahama
 Balozi Seif akielekea kwenye Mkutano wa Mbunge wa Jimbo la Msalala Mh. Ezekiel Magolyo Maige kushuhudia uwasilishwaji wa Utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa Mwaka 2015 – 2020.
 Balozi Seif akimpokea aliyekuwa Mwenyekiti waTawi la Chama cha Demokrasia ya Maendeleo {CHADEMA} Bibi Getrude aliyeamua kurudi CCM yeye pamoja na Uongozi wake mzima wa uliokuwa Chadema.
Uongozi Mzima wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo       { Chadema} katika Kijiji cha Buganzo ukikabidhiwa sare za CCM Mara baada ya kupokelewa kurudi katika Chama chao cha asili ccm.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Balozi Seif Ali Iddi alisema ushindi mnono wa CCM kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mwaka huu ni ishara njema kwa Chama hicho kuendelea kuongoza Dola ya Tanzania kwa miaka mingi ijayo.
Alisema kinachohitajika kwa sasa ni ushirikiano zaidi kati ya Viongozi na Wanachama wa Chama hicho licha ya kazi kubwa iliyofanywa na Serikali za CCM katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015 -2020 ndani ya Kipindi cha Miaka Minne.
Balozi Seif Ali Iddi ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na Mlezi wa Mkoa wa Shinyanga Kichama alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Wana CCM na Wananchi wa Jimbo la Msalala Baada ya kuweka Jiwe la Msingi la Jengo Jipya la Tawi la CCM Buganzo kwenye Mkutano wa Mbunge wa Jimbo hilo Mh. Ezekiel Magolyo Maige wa kuwasilisha kwa Wananchi Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Jimbo hilo.
Alisema Chama cha Mapinduzi kimefanya mambo mengi makubwa ya kupigiwa mfano katika kuwaletea maendeleo Wananchi wake Chini ya usimamizi wa Mwenyekiti wa Chama hicho ambae pia ni Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John  Pombe Magufuli.
Balozi Seif aliwaeleza Wananchi hao wa Jimbo la Msalala kwamba katika azma Kuu ya ushindi wa lazima wa CCM kwenye chaguzi zake zote Viongozi wa Chama hicho hasa ngazi ya Wilaya ambayo ndio inayopendekeza Majina ya Wagombea wa Chama hicho katika chaguzi hizo lazima waendelee kutumia hekima na busara za kutenda haki katika kupitisha majina yanayostahiki.
Alisema wapo baadhi ya Viongozi wa ngazi hiyo wenye tabia ya kupendekeza majina ya Watu kwa kuzingatia zaidi urafiki, udugu na uhisani hali inayoleta vurugu na migongano baadae na hatimae kuanza kujitokeza cheche za mgawanyiko unaozaa makundi yanayodhoofisha nguvu za Chama.
“ Migogoro baina ya Wanachama wenyewe kwa kwenyewe ndani ya Chama kamwe haileti Afya wala tija”. Alitahadharisha Mlezi huyo wa Mkoa wa Shinyanga.
Alisema Viongozi wa Wilaya kazi yao kubwa ni kusimamia haki ya kila Mwanachama, na yule atakayebahatika kuibuka kuwa mgombea wa nafasi yoyote amefanikiwa kutokana na jitihada zake za kukitumikia Chama katika harakazi zake akiwa Mwanachama.
Alisisitiza kwamba katika kupata Viongozi safi na makini, wanaopendekezwa  lazima wapimwe katika vigezo bora vinavyokubalika ndani ya Chama katika ngazi zote za uteuzi.
Akigusia suala la Amani Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM alisema utulivu na Amani iliyopo Nchini lazima ilindwe kwa gharama yoyote ile ili Taifa liendelee kupata mafanikio makubwa kimaendeleo katika sekta ya Uchumi na Ustawi wa Jamii.
Alisema Tanzania inaendelea kubega sifa ya kudumisha Amani ndani ya Bara la Afrika kitendo ambacho hadi sasa kinaheshimiwa na Mataifa mbali mbali ya Bara hili kutokana na mchango wake mkubwa wa kusaidia Ukombozi kwa Mataifa mengi ya Bara hili.
Katika kuunga mkono jitihada kubwa zinazoendelea kuchukuliwa na Wana CCM na Wananchi wa Kijiji cha Buganzo katika kujiletea Maendeleo Balozi Seif alichangia Shilingi Milioni Moja {1,000,000/-} ili kuwapa nguvu zaidi za kufikia malengo waliyojipangia.
Mapema Mbunge wa Jimbo la Msalala Mheshimiwa Ezekiel Magolyo Maige Akiwasilisha Taarifa ya Utakelezaji wa Uilani ya CCM ya Jimbo hilo ndani ya Kipindi cha Miaka Minne alisema hadi ifikapo Mwaka 2020 Utekelezaji huo wa Ilani utakuwa ushafikia asilimia 90%.
Mh. Maige alisema juhudi kubwa imefanywa na Uongozi wa Jimbo la Msalala katika kusimamia seka za Kilimo, Afya, Ufugaji pamoja na uimarishaji wa Sekta ya Elimu kwa kuwajengea mazingira bora Watoto wa Jimbo hilo mambo yanayokwenda sambamba na uhamasishaji wa Vikundi vya ujasiri amali vya Wananchi.
Alisema mafanikio hayo yametokana na uwezeshaji wa fedha za Mfuko wa Jimbo, zilizojumuisha na zile za Washirika wa Maendeleo kwa kuungwa mkono zaidi na Serikali Kuu nguvu zilizopelekea kujengwa kwa Vituo vipya vya Afya vinavyofaidisha Wananchi wa Vijiji 92, Matawi 108 na Vitongoji 389 ndani ya Jimbo hilo.
Mbunge huyo wa Jimbo la Msalala ameishukuru na kuipongeza Serikali Kuu kwa mchango wake mkubwa uliowezesha kupunguza kero mbali mbali zilizokuwa zikiwakabili Wananchi wake.
Hata hivyo Mh. Maige alisema bado zipo changamoto zinazokwaza harakati za Kiuchumi za Wananchi wa Jimbo hilo, Wilaya ya Kahama na Wilaya zilizojirani na Mkoa wa Shinyanga akizitaja kuwa ni pamoja na Bara bara inayounganisha na Mikoa mengine pamoja na Huduma za Maji Safi na salama.
Naye kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa wa Shinyanga Mheshimiwa Aza Hamad  Hilal alisema katika kuunga mkono utekelezaji wa Ilani ndani ya Mkoa huo amejitahidi kuongeza nguvu katika uimarishaji wa Sekta ya Afya.
Mh. Aza alisema Sekta ya Afya ni muhimu kwa nguvu kazi za Wananchi hasa akina mama wanaohitaji kuimarishiwa huduma hizo ili waendelee kuwa walezi bora wa Familia yenye nguvu na Afya.
Mapema Mchana Balozi Seif ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alikabidhi msaada wa vifaa mbali mbali vya Tiba kwa Uongozi wa Hospitali ya Hospitali ya Kahama Mji.
Akikabidhi vifaa hivyo Balozi Seif alisema Serikali Kuu muda wote imekuwa ikitilia mkazo Suala zima la uimarishaji wa huduma za Afya kwa Wanachi wake na ndio maana hutenga fedha nyingi kwa kugharamia huduma hizo muhimu kwa ustawi wa Jamii.
Balozi Seif  aliwanasihi watendaji wa Hospitali na Vituo vya Afya hasa  Wauguzi kuacha maneno ya mkato dhidi ya Wagonjwa wao hasa akina Mama wanapokwenda Hospitali na Vituo vya Afya Kujifungua.
Alisema si vyema kwa Mwananchi anapopatwa na changamoto ya maradhi akaanza kubughudhiwa kwani mjazito anahitaji kufanyiwa huruma kubwa  kwa vile yuko katika maandalizi ya kuleta kizazi kipya.
Akitoa shukrani kwa niaba ya Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga Mkuu wa Mkoa huo Mh. Zainab Rajab Telak alisema kitendo alichofanya cha Balozi Seif  cha kuipatia Hospitali hiyo vifaa vya Tiba kimeonyesha upendo wake mkubwa kwa Wananchi hao.
Mh. Zainab alisema msaada huo wa Balozi Seif  ni faraja iliyolenga kuimarisha Sekta ya Afya kwa Wananchi wa Shinyanga wanaotumia Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kahama ambayo pekee huwa inazalisha Watoto kati ya 40 hadi 50 kwa siku kiwango ambacho inapaswa ziwepo nguvu za msaada kwa wahisani.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.