Habari za Punde

Waziri Mkuu Mhe.Kassim Majaliwa Akagua Ujenzi wa Hospital ya Wilaya ya Geita na Kuzungumza na Wananchi.

Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi baada ya kukagua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Geita katika kijiji cha Nzela
Vijana wa kijiji cha Nzela katika jimbo la Geita Vijijini wakimshangilia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  wakati alipozungumza na wananchi baada ya kuakagua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Geita,
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama baadhi ya vifaa tiba vilivyopatikana kutokana na juhudi za  mbunge wa Geita vijijini, Joseph Msukuma (kulia) kwa ajili ya  hospitali ya wilaya ya Geita iliyopo katika kijiji cha Nzela, wakati alipokagua ujenzi wa hospitali hiyo na kuzungumza na wananchi Septemba 21, 2019. Wa pili kulia ni Mganga Mkuu wa wilya ya Geita, Deo Kisaka.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Mamlaka  ya Usajili wa Vitambulisho vya Taifa  (NIDA) ihakikishe wananchi  hasa walioko vijijini wanapata angalau  namba za utambulisho wa usajili wao kabla ya muda wa usajili wa laini za simu haujamalizika. 

Ametoa agizo hilo jana (Jumamosi, Septemba 21, 2019) wakati alizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa hospitali ya wilaya ya Geita iliyopo kwenye Kijiji cha Nzela.

Alisema kitendo cha kuwapatia namba za utambulisho wa usajili wananchi ambao hawajapata vitambulisho vya uraia kitawezesha kuingia kwenye orodha ya wale wanosubiri kusajiliwa hata kama muda wa usajili utakuwa umeisha. Mwisho wa muda wa usajili ni Desemba mwaka huu.

Waziri Mkuu alisema Serikali imewapatia NIDA vifaa vya kisasa vya kielektroniki ili wafanye kazi zao kwa haraka na ufanisi, lakini hali hairidhishi kwa sababu wananchi wengo bado hawajapata vitambulisho na kasi ya usajili wa laini za simu inalalamikiwa katika meneo mengi. 

“NIDA mnalalamikiwa, nimeenda Morogoro Vijijini NIDA mnalalamikiwa hivi utendaji wenu uko je? Kwanini mnachelewa ?” Waziri Mkuu alimuuliza Afisa Msajili wa NIDA wa wilaya ya Geita, Paschal Saro ambaye  alijitetea kwamba wamesajili laini za simu 340 na tayari namba za usajili 330 zimeshatolewa.

Saro alimwambia Waziri Mkuu kuwa suala la utata wa uraia kwa baadhi ya wananachi wanaoomba vitambulisho vya NIDA ni moja ya sababu zinazochelewesha  usajili wa vitambulisho vya uraia.

Waziri Mkuu aliwasihi wananchi wote kuwa walinzi wa nchi yao kwa kutoa taarifa za watu ambao wanaomba viutambulisho vya uraia wa Tanzania wakati si raia na aliwataka watoe taarifa mara moja kwenye vyombo vya dola pale wanapogundua kuwa kuna raia wa nje anafanya mchakato wa kuapata vitambulisho hivyo.

Alisema katika baadhi ya mikoa ya mipakani ambayo ina wakimbizi Serikali imekamata silaha ambazo raia hawasurusiwi kuzimiliki na zinasadikiwa kuwa zimepenyezwa nchini na raia wa nje wasiowaaminifu.

Awali,Waziri Mkuu, alikagua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Geita iliyopo katika kijiji cha Nzera mkoani Geita na kufurahishwa na hatua ya Mbunge wa jimbo wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma ambaye amewezesha upatikanaji wa vifaa tiba vya kisasa kwa ajili ya hospitali hiyo.

Waziri Mkuu alimpongeza Musukuma kwa moyo wa upendo alionao kwa  wapiga kura wake.  Vifaa hivyo ni vya kisasa na vinastahili kuwa katika hospitali za rufaa za mikoa lakini mbunge huyo ameamua kuwapelekea wapiga kura wake kwenye hospitali ya wilaya lengo likiwa ni kuboresha huduma.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, SEPTEMBA 22, 2019.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.