Habari za Punde

WANAOPANDISHA BEI YA CEMENT KUPOKONYWA LESENI

Na Hamida Kamchalla, TANGA.

MKUU wa mkoa wa Tanga Martin Shigela amewaagiza viongozi na watendaji wa wilaya za mkoa huo kufanya msako na kubaini wafanyabiashara wanaopandisha bei za cement (saruji) kwakuwa bei ya bidhaa hiyo haijapanda viwandani.

Shigela aliyasema hayo jana alipotembelea kiwanda cha cement cha Kilimanjaro jijini Tanga baada ya tetesi za kupanda kwa bidhaa hiyo katika baadhi ya maduka.

Alisema kuwa lengo la msako huo ni kuwabaini na kuwachukulia hatua wale wote watakaokutwa wamepandisha bei baada ya kugundua kuna upungufu wa bidhaa ambao umetokana na hali ya kiwanda kupata hitilafu za kiufundi.

"Agizo langu kwa wakuu wote wa wilaya, wakurugenzi, maafisa tarafa na wengineo kuhakikisha mnafanya msako kwenye maeneo yenu na kuwabaini wafanyabiashara wa cement wanaopandisha bei, mtakapowabini muwachukulie hatua pamoja na kuwanyang'anya leseni zao" alisisitiza. 

Aidha ametoa onyo kwa wafanyabiashara kuacha kujipandishia bei bila tamko maalumu la makubaliano ambapo alieleza kwamba wafanyabiashara wana tabia ya kurundika bidhaa kwenye magodauni yao kisha kunapotoke tafizo la uzalishaji wanapandisha bei.

"Cement ipo kiwandani na haijapandishwa bei, hivyo ni marufuku kwa wafanyabiashara kufanya ujanja ujanja kupandisha bei, kwa sababu bei za viwandani ziko palepale, wanarundika cement kwenye magodauni na kuiuza kwa bei ghali wanapoona kuna tatizo la uzalishaji" alisema.

Sambamba na hilo Shigela ameahidi kutoa ushirikiano kwa viwanda vya cement jijini Tanga ili kuweza kufanya uzalishaji wa kutosha kutokana na ongezeko la uhitaji wa bidhaa hiyo.

Naye Msimamizi mkuu wa fedha katika kiwanda hicho Filbert Nshange alieleza kwamba wao kiwandani hawajapandisha bei ya bidhaa kama inavyodaiwa isipikuwa ndani ya mwezi mmoja uliopita uzalishaji ulisimama kutokana na mitambo yao ya kuzalishia kuharibika.

"Bei ya cement hatujapandisha isipokuwa mwezi mmoja uliopita kuna mashine iliharibika hivyo kupelekea uzalishaji kusimama, lakini tumeshafanya matengenezo na sasa uzalishaji umeanza na tumeanza rasmi wiki iliyopita" alisema.

Hata hivyo Nahange alieleza kwamba wana bei mbili kiwandani hapo ambapo kwa wanunuzi wa ndani ya jiji la Tanga wananunua kwa shilingi 11,600 kwa mfuko wakati wanunuzi wa nje ya Tanga wananunua kwa shilingi 10,600.

Nshange aliongeza kuwa kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha mifuko 7000 ambayo ni sawa na tani 300 kwa siku.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.