Habari za Punde

Wananchi wa Zanzibar Watakiwa Kuimarisha Amani na Umoja Walionao Ili Kuiletea Nchi Yao Maendeleo.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akiwasalimia na kuzungumza na Wananchi wa Kijiji cha Bweleo Wilaya ya Magharibi “B” Unguja baada ya kumalizika kwa  Sala ya Ijumaa iliofanyika katika Msikiti Mkuu wa Ijumaa Bweleo


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka wananchi wa Zanzibar kuimarisha amani na umoja walionao ili kuiletea nchi yao maendeleo.

Alhaj Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo huko katika Msikiti wa Ijumaa Bweleo, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi wakati akitoa salamukwa Waislamu mara baada ya kukamilisha Sala ya Ijumaa.

Katika salamu zake hizo Alhaj Dk. Mwinyi alisema wananchi wote wa Zanzibar wana kila sababu kuungana pamoja katika kuendeleza amani na umoja uliopo kwani bila ya kuwepo mambo hayo ya msingi maendeleo hayawezi kupatikana.

Alisema kuwa kukosekana kwa amani hupelekea kutokufanyika mambo muhimu katika maisha ya wananchi ikiwemo kushindwa kutekeleza ibada hivyo,Alhaj Dk. Mwinyi alieleza kwamba kila mmoja ana wajibu wa kuendeleza na kuimarisha amani iliyopo.

Alieleza kuwa wananchi wana matumaini makubwa ya kupiga hatua za uchumi hapa nchini sambamba na kubadilika kwa maisha yao kwa sababu ya kuwepo kwa amani, hivyo, ni jukumu la kila mtu kuidumisha na kuihubiri amani na umoja uliopo.

Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa upo umuhimu mkubwa wa kuimarisha umoja, kwani ni muhimu katika kujiletea maendeleo kwani kuwepo kwa mifarakano hakuna tija na wala hakutaleta maendeleo.

Alieleza jukumu la wananchi la kuidumisha na kuihubiri amani na kusisitiza kwamba umoja ni jambo la msingi na ndio maana kwa upande wao viongozi wa siasa wameweza kuhubiri amani na umoja kwa vitendo kwa kuungana na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kuweza kuwaunganisha watu.

Hivyo, aliwataka wananchi kuweka tofauti zao za kisiasa na kiitikadi pembeni na badala yake wawe kitu kimoja katika kuendeleza amani, umoja na mshikamano.

Alhaj Dk. Mwinyi alieleza kwamba kwa upande wake ana jukumu kubwa la kuwahudumia wananchi pamoja na kutekeleza ahadi alizoziahidi wakati wa kampeni sambamba na kuhakikisha kwamba nchi inapata maendeleo ya haraka na maisha ya wananchi yanaimarika.

Kwa kutekeleza hayo, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kwamba kuna hitaji msaada wa wamawazo, dua sambamba na watu kuwajibika katika kufanya kazi.

Kutokana na hayo, Rais Dk. Mwinyi aliwataka waumini hao kumuombea dua ili atimize majukumu yake na atende haki kwa kila mmoja kutokana na dhima aliyonayo mbele ya MwenyeziMungu na wananchi ya kutenda haki.“Ombi langu kwenu ni kuendelea kuniombea”,alisisitiza Alhaj Dk. Mwinyi.

Alhaj Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba amegombea nafasi hiyo kwa nia moja ya  kuwatumikia wananchi wa Zanzibar ambapo kitu kilicho mbele yake hivi sasa ni utekelezaji.

Alieleza kwamba katika utekekezaji kuna mamabo yatawakusa watu ambapo pale atakaposema watu wawajibike na kwamba hawatowajibika basi watawajibishwa hivyo, na hatua zinazochukuliwa ni kujenga na wala sio visasi.

Aliongeza kwamba watu wote wakiwajibika hasa watumishi wa umma katika maeneo yao maendeleo ya haraka yatapatikana.

Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Mwinyi alieleza kwamba kuna mapambano dhidi ya rushwa, ubadhirifu, wizi, uzembe ambapo hayo yakiwachwa kuendelea hakuna maendeleo yatakayopatikana kwani wapo ambao wanabomoa wakati serikali inajenga.

Hivyo, alisisitiza kwamba kuna haja ya kupigwa vita vitendo hivyo kwa nguvu zote hasa kwa kutambua kwamba kupambana na vitendo hivyo kutagusa watu ambao ndani yake wamo jamaa, ndugu lakini lengo ni kutafuta maendeleo ya haraka na wala si kumkomoa mtu.

Mapema akisoma hotuba ya sala  ya Ijumaa, Khatibu wa msikiti huo Sheikh Mussa Ali Kirobo alieleza haja kwa waumini kushikamana na maamrisho ya Allah na wala wasifarakiane na kuwataka kuwa kitu kimoja.

Aliongeza kwamba katika dini ya Kiislamu watu wote ni sawa na hakuna aliyebora hata mmoja na badala yake mbora ni yule anayemcha MwenyeziMungu zaidi.

Nae Katibu wa Mufti Sheikh Khalid Ali Mfaume alisisitiza haja kwa wananchi kumuombea dua Alhaj Dk. Mwinyi kutokana na mambo makubwa anayoyafanya na kuwataka wananchi kuithamini neema hiyo ya kupata kiongozi huyo bora.

Wakati huo huo,mara baada ya kumaliza Sala hiyo ya Ijumaa huko Bweleo Alhaj Dk. Mwinyi alikwenda kumtembelea Rais Mstaafu wa Awamu ya Saba  Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein huko nyumbani kwake Kibele, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.