Habari za Punde

DKT. MWIGULU NCHEMBA AHIMIZA UFUGAJI WA KISASA ILI KUSISIMUA UCHUMI NA MAISHA YA WATU

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akieleza kuhusu umuhimu wa kupanua wigo wa vyanzo vya kodi katika Sekta ya Mifugo, Uvuvi na Utalii, alipofanya mkutano kati yake na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Mashimba Ndaki (Mb) na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) (hawapo pichani), ambao pia uliwakutanisha wataalamu wa Wizara hizo, jijini Dodoma.


Na Benny Mwaipaja, Dodoma

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameishauri Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kusimamia kikamilifu sekta ya mifugo kwa kubuni njia mbalimbali zitakazoongeza tija katika sekta hiyo.

Dkt. Nchemba ametoa ushauri huo Jijini Dodoma, alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Wizara hiyo pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii, kujadili masuala mbalimbali yanayohusu namna ya kuboresha sekta ya mifugo ili iweze kuongeza mchango katika ukuaji wa uchumi wa nchi na maendeleo ya watu.

“Tutakavyo weka mipango ya kisasa ya kukuza uzalishaji katika eneo hili la mifugo, tutatengeza wigo mkubwa wa walipakodi, tutabadilisha maisha ya watu wetu, tutakuza uchumi na ajira” alisema Dkt. Nchemba

Alisema kuwa maendeleo ya sekta ya viwanda yanayokwenda kwa kasi hapa nchini yanahitaji malighafi za kulisha viwanda hivyo na kwamba fursa zilizopo kwenye sekta ya mifugo ni kubwa na kushauri mbinu za kisasa za kuendeleza ufugaji ziwekwe bayana na kufanyiwa kazi ipasavyo.

Alisema utaratibu wa sasa wa wafugaji kuhamahama na mifugo kwa ajili ya kutafuta malisho na maji umepitwa na wakati na kuahidi kuwa Wizara yake iko tayari kutoa ushirikiano ili kufanikisha mipango ya kuendeleza sekta ya mifugo nchini.

Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki, alimshukuru Mhe. Waziri wa Fedha na Mipango kwa kukutana na vingozi wa Wizara hizo mbili na kuahidi kuwa ushauri uliotolewa utafanyiwa kazi kikamilifu ambapo ameunda timu ya wataalamu kwa ajili ya kuchambua mapendekezo mbalimbali yaliyotolewa katika kikao hicho alichosema kilikuwa ni cha muhimu.

“Tutaangalia namna ya kupanua na kuwa na  maeneo maalum ya malisho ya mifugo yetu pamoja na kuboresha ufugaji ili ubadilike kutoka ufugaji wa kiasili kwenda ufugaji wa kisasa ili kuongeza tija” alifafanua Mhe. Ndaki

Alisema kuwa wafugaji watakaokuwa tayari kubadilisha namna ya ufugaji wao watapelekwa kwenye maeneo hayo yatakayowekewa miundombinu yote muhimu ya ufugaji ikiwemo maji, majani ya malisho na maji.

Wakizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba, aliishauri Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuanzisha maeneo ya ufugaji (Runch) kila mkoa na kujenga miundombinu itakayowasaidia wafugaji kufuga mifugo yao kisasa ili waweze kuongeza kipato chao, kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi na kuondokana na umasikini.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Elisante Ole-Gabriel aliiomba Wizara ya Fedha na Mipango kuiwezesha Wizara yake kifedha kwa ajili kufanya utafiti katika sekta ya mifugo ili kuongeza mbinu za kisasa za kuongeza uzalishaji.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Allan Kijazi, alishauri kuwa ili sekta ya mifugo iweze kupiga hatua kubwa, suala la utafutaji masoko kwa ajili ya bidhaa za mifugo, kuongeza elimu kwa wafugaji, pamoja na kuwa na maeneo ya kimkakati ya viwanda vya kuchakata bidhaa za mifugo ni muhimu likafanyiwa kazi.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), kwenye kikao hicho Prof. Elisante Ole-Gabriel, Tanzania ni ya pili kwa kuwa na mifugo mingi barani Afrika kwa kuwa na ng’ombe milioni 33.4, mbuzi milioni 21.29, Kondoo milioni 5.65, Punda 657,380, lakini tija yake bado ni ndogo.

Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) akiongoza Mkutano kati yake na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Mashimba Ndaki (Mb) na  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb), ambao pia uliwakutanisha Wataalamu kutoka Wizara hizo, jijini Dodoma.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Mashimba Ndaki (Mb) (kulia), akieleza kuhusu Sekta ya Mifugo inavyoweza kuongeza fursa za uwekezaji na kuinua uchumi wa nchi, katika Mkutano na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) (hawapo pichani), kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb), akifafanua jambo wakati wa Mkutano kati yake na Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Mashimba Ndaki (Mb) (hawapo pichani), katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia), akieleza umuhimu wa kuwa na mbegu bora za mifugo, wakati wa mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe Mashimba Ndaki (Mb) na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb), jijini Dodoma, kushoto ni Katibu Mkuu wa Maliasili na Utalii, Bw. Dkt. Allan Kijazi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba, akifafanua jambo wakati wa Mkutano kati ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Mashimba Ndaki (Mb) (kulia) na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) (hawapo pichani), jijini Dodoma.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.