Habari za Punde

Uwekaji wa Jiwe la Msingi Mradi wa Ujenzi Mabweni Ya Wanafunzi Kampasi ya Karume Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed akipata maelezo ya mradi wa ujenzi wa Mabweni ya Wanafunzi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kampasi ya Karume Zanzibar kutoka kwa Mkurugenzi wa Huduma za ushauri wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Msanifu Majengo Wencelause P. Kizaba
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akiweka jiwe la Msingi la ujenzi wa Mabweni ya wanafunzi wa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kampasi ya Karume Zanzibar.
Mkuu wa chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Shadrack Mwakalila akimueleza Mgeni Rasmi changamoto zinazokikabili chuo hicho ikiwemo uvamizi wa eneo la chuo katika hafla ya uwekaji wa jiwe la Msingi la ujenzi wa Mabweni ya wanafunzi kampasi ya karume Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na kuhutubia katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la mradi wa ujenzi wa mabweni ya wanafunzi  wa chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere – Kampasi ya Karume Zanzibar.



Na.Kassim Abdi. OMPR.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema uwepo wa Chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu  Nyerere visiwani Zanzibar  ni kielelezo Chanya katika kuenzi na kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa Vitendo.

Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alieleza hayo kupitia hotuba alioisoma kwa niaba ya Rais Dk. Hussein Mwinyi  katika hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la mradi wa ujenzi wa mabweni ya wanafunzi  wa chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere – Kampasi ya Karume Zanzibar.

Alieleza kuwa, Bodi pamoja na uongozi wa chuo hicho wamekuwa wakifanya kazi nzuri kwani tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mnamo mwaka 1961 mpaka sasa chuo kimekuwa kinaishi kwa mawazo ya waasisi wa Taifa la Tanzania Hayati Mwalimu J.K Nyerere na Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume .

Makamu wa Pili Rais alisema kutokana na jitihada mbali mbali zinazochukuliwa na uongozi wa Chuo hicho serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikitambua mchango unatolewa na chuo hicho katika kutoa mafunzo mbali mbali kwa Astashishahada, Stashahada, Shahada na Shahada ya Uzamili.

Pamoja na utoaji huo wa Mafunzo Mhe. Hemed alieleza chuo kimekuwa na mchango mkubwa katika kutoa mafunzo ya uongozi , maadili na uzalendo kwa wanafunzi na watumishi mbali mbali ambao kwa namna moja au nyengine wanasaidia katika kutekeleza majukumu yao kupitia serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Alifafanua kuwa, Ni ukweli usiopingika wahitimu wanaotoka katika chuo hicho baada ya kumaliza mafunzo yao hutoka wakiwa wameiva , wenye uwadilifu na uweledi wa hali ya juu jambo ambalo lina umuhimu kwa watu ambao hupewa dhamana katika nafasi za utumishi wa Umma.

“Tangu kuanzishwa kwa chuo hiki kimewanufaisha watanzania wengi na serikali kwa ujumla, kupitia chuo hichi kimepata kimepata wahitimu wengi wenye ari na bidii ya kulitumikia taifa hili kwa uweledi na kuchangia katika maendeleo ya taifa” Alieleza Makamu wa Pili wa Rais

Alisema kitendo cha chuo hicho kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Mabweni ya wanafunzi kinaashiria kutekeleza kwa vitendo mipango ya serikali ya awamu ya sita kwa kuzingatia maelekezo mbali mbali  ya serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia ikiwemo suala kuongeza udahili wa wanafunzi na ujenzi wa miundombinu mbali mbali katika taasisi za Kielimu.

Mhe. Hemed alieleza hatua ya chuo kuweka jiwe hilo la msingi ni kubwa sana katika kufikia mafanikio kwani chuo kupitia mapato yake ya ndani kimeweza kuanzisha mradi mkubwa ambao utanufaisha kizazi cha sasa na cha baadae.

“Niwasihi Wadau wote wa maendeleo mliopo hapa mtuunge mkono katika ujenzi wa Mabweni haya ambayo yatagharimu Shillingi Bilioni Kumi na Tano nukta Mbili (15.2) ambao ukikamilika utasaidia sana wanafunzi kupata malazi bora na salama na hatimaye kuwapatia ari ya kusoma ili kupata maarifa bora yatakayoongeza maendeleo kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Alisema Mhe. Hemed

Pamoja na mambo mengine, Makamu wa Pili wa Rais alimuomba mkandarasi wa mradi huo ambae ni SUMA JKT kukamilisha mradi huo kwa wakati uliopangwa kwani mradi huo unalenga kutatua changamoto kubwa iliopo kwa wanafunzi ya kukosa makaazi.

Katika Hatua nyengine, Aliwahisi watekelezaji wa mradi huo kufuata sheria na taratibu zote za utekelezaji wa mradi kwa lengo la kuondoa migogoro na hasara zisizokuwa za lazima na kuokoa fedha za serikali zinazotumia katika ujenzi wa mradi huo.

Kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi Waziri wa Elimu na Mafunzo ya amali Zanzibar Mhe. Simai Mohamed Said aliupongeza uongozi wa Chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kwa kuhakikisha yale malengo waliojiwekea ya kutoa mafunzo ya uongozi na uzalendo kwa jamii yanafikiwa.

Aidha, Mhe. Simai aliukumbusha uongozi wa Chuo hicho mbali na mafunzo ya uongozi na uzalendo wanayoyatoa lakini pia ipo haya yua kuangalia upya uwezekano wa kuwafanya wanafunzi wawe na uwezo wa kufanya vitu vingi kwa pamoja kwa kuzingatia masuala ya Ubunifu na Uvumbuzi kama zinavyofanya nchi nyengine Duniani.

Aliwahakikishia kwamba Wizara ya Elimu na mafunzo ya Amali Zanzibar itahakikisha inaendelea kushirikiana na chuo hicho huku ikizingatiwa kuwa Wizara anayoingoza ipo katika mchakato wa kufanya marekebisho kupitia kitengo chake kinachosimamia elimu ya juu ili kiweze kwenda sambamba na Wadau wa Elimu Nchini.

Kwa upande wake Mkuu wa chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Prof. Shadrack Mwakalila alitumia fursa hiyo kumshukuru na kumpongeza Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa jitihada anazoendelea katika kukuza uchumi wa Zanzibar.

Alieleza kuwa jitihada hizo zinapaswa kuungwa mkono na kila mmoja katika jamii kwani zinalenga kuinua hali za maisha ya watu wa hali ya chini ikizingatiwa kwa sasa Rais Dk. Mwinyi amedhamiria kuukuza uchumi wa Zanzibar kupitia uchumi wa bahari (BLUE ECONOMY).

Prof. Shadrack alisema chuo hicho kimeamua kuingiza somo la uongozi na uzalendo katika kila kozi ili kuwajenga wanafunzi wanapomaliza mafunzo yao ili kuwajenga vijana kuwa viongozi bora na wenye uweledi.

Alieleza kuwa, Kampasi ya Karume imefanikiwa kutenga fedha kupitia bajeti yake ikiwa na adhmna ya kutekeleza miradi mbali mbali ikiwemo ujenzi wa Mabwni ya wanafunzi, Ujenzi wa madarasa ya kusomea, Ujenzi wa Ofisi kwa upande wa Pemba pamoja na ujenzi wa nyumba za walimu.

Akizungumzia Mradi huo wa ujenzi wa Mabweni ya wanafunzi Prof. Shadrack alimueleza Makamu wa Pili wa Rais kuwa ni jambo la kujivunia katika utekelezaji wa mradi huo kutokana na kutekelezwa na wataalamu wazalendo huku akiwaomba wadau wa maendeleo waliopo Zanzibar kujitokeza kuunga mkono mradi wa ujenzi huo.

Akigusia changamoto zinazokikabili chuo hicho kwa kampasi ya Karume Zanzibar alisema kumekuwepo kwa changamoto ya baadhi ya watu kuvamia eneo la chuo tangu mwaka 2018 na kumuomba mgeni rasmi kulipatia ufumbuzi suala hilo kutokana na kurejesha nyuma jitihada za chuo hicho.

Akisoma Taarifa ya utekelezaji wa mradi huo  Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la uzalishaji Mali la jeshi la kujenga Taifa (SUMA-JKT) Kanali Absolonon Lyanga Shausi alisema wanaishukuru serikali ya mapinduzi Zanzibar kupitia wakala wa majengo Zanzibar kwa kuisajili SUMA-JKT kuweza kufanya kazi zake Zanzibar na kuahidi kuwa mradi huo utakamilika ndani ya wakati uliopangwa wa kipindi cha miezi 18 huku ikizingatia weledi katika utekelezaji wake.

Katika kuunga mkono jitihada za kukamilisha mradi wa ujenzi huo Mbunge wa Jimbo la Mpendae kwa niaba ya Turky Foundation amechangia jumla ya Shilingi Millioni Ishirini (20,000,000/=) ikiwa ni kuitikia wito wa wadau wa maendeleo waliopo Zanzibar kujitokeza kusaidia kufanikisha mradi huo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.