Habari za Punde

Waziri wa Maji Mhe.Jumaa Aweso Ataka Miradi Kichefuchefu kumaliziwa ili Kuleta Taswira Mpya ya Wizara.

Na Hamida Kamchalla, TANGA.

WAZIRI wa Maji Jumaa Aweso ameitaka Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) mkoani Tanga kuhakikisha kwamba mpaka ifikapo mwezi Disema wanamaliza miradi yote kichefuchefu iliyobaki ili kuleta raswira mpya katika Wizara hiyo.

Waziri Aweso alitoa agizo hilo jana kwenye hafla ya kuanza kwa Mradi wa Kuboresha Huduma ya Maji Tanga Awamu ya Pili iliyoandaliwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (Tanga UWASA) katika mji wa Pande, jijini Tanga.

Alisema wakati wanakabidhiwa Wizara hiyo ikiwa na miradi mingi kichefuchefu lakini katika kutekeleza ilani ya imepambana na kufanikisha kuiondoa baadhi kwa kumaliza utekelezaji wake huku akisisitiza kumalizika kwa miradi iliyobaki ili kuendelea na Wizara yenye miradi yenye tija ambayo itatumia gharama kulingana na utekelezaji.

"Wizara yetu ya maji inapitia mageuzi makubwa sana, hapo mwanzo Wizara hii ilikuwa ni Wizara ya kero, sisi tukakubaliana badala ya kuwa kero tunakwenda kuifanya Wizara ya utatuzi, tunatambua tumekabidhiwa Wizara hii miaka ya nyuma ikiwa na miradi ya WSDP ambayo mingi ilikuwa kichefuchefu" alisema.

"Tumeidhinisha jumla ya miradi 177 kichefuchefu na tayari tuneshakamua miradi zaidi ya 85 mpaka sasa na watu wanapata maji, niwaombe ndugu zangu wa RUWASA, katika maeneo haya ya Tanga, miradi ile yote kichefuchefu ambayo imebaki, mpaka ikifika mwezi Disemba mwaka huu miwe mmeikamilisha ili twende na taswira mpya ya kujenga Wizara yetu ya maji" alisisitiza Aweso. 

Aidha Aweso alimtaka Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kuharakisha upelekaji wa mradi wa maji wilayani Mkinga ili wananchi wapate huduma hiyo ambayo kwa Wilaya hiyo ni kilio chao cha muda mrefu huku akifafanua kwamba tayari fedha zimeshaidhinishwa kilichobaki ni taarifa ya kuanza kwa mradi huo.

Alibainisha kwamba Wizara imeidhinishiwa kiasi cha sh bilioni 680 na Bunge ambapo mbali na hilo Rais Samia Sulluhu Hassan ameongeza kiasi cha sh bilioni 207 kwa ajili ya kuongeza nguvu ya utekelezaji, lakini pia aliongeza kuwa kwa upande wa vijijini RUWASA tayari wana fedha kwa ajili ya kutatua kero za maji katika maeneo yao.

"Mradi wa kuyatoa maji hapa na kuyapeleka wilayani Mkinga naomba sana yasibaki tena maneno matupu, twendeni tukautekeleze ule mradi haraka iwezekanavyo, Katibu Mkuu unafanya kazi nzuri sana na nina furaha kufanya kazi na wewe, twende tukatimize jukumu la kuyatoa maji, hiki ni kilio cha muda mrefu sana, sisi kama Wizara kupitia Tanga UWASA tuwapelekee huduma ya maji afu na salama watu wa Mkinga" alieleza.

"Sambamba na hapo tuna eneo la vijijini, RUWASA Tanga hamna kisingizio tena, bilioni 21 zinakuha kwa ajili ya kutatua kero ya maji, niwaombe sana fedha hizi zisiende kuishia kwenye makaratasi mtafute Makandarasi wenye uwezo, kuongeza nguvu ya kutumia fedha hizi mlizotengewa kwa Wanakilindi, Wanahandeni, Wanamuheza na Mkinga yake na maeneo mengine yote" alisisitiza.

Hata hivyo Aweso aliwataka watendaji wote katika kila idara inayohusu Wizara hiyo kutumia nafasi yake kutimiza majukumu yake katika utekelezaji wa miradi kwa kufuatilia kwa ukaribu na kukamilisha kwa wakati ili wananchi wapate huduma hiyo badala ya kukaa ofisini na kusubiri viongozi kutoka juu kufika kwenye miradi kabla yao.

"Wizara imeajiri Wataalamu katika kila ngazi, kila mmoja kwa nafasi yake atoke ofisini aende kusimamia na kufuatilia miradi ili Watanzania wapate maji, Mamlaka za maji mna jukumu kila maeneo ambapo mnaona kuna mivujo ya maji twende tukazibe mivujo yetu, leo mwananchi hana maji anapita mtaani anakuta maji yanamwagika bila mpangilio" alisema.

Sambamba na hayo Aweso alisisitiza umuhimu wa kulinda vyanzo vya maji hasa kwa wananchi kwa kuweka dhamira ya pamoja kutokana na kwamba vyanzo hivyo haviongezeka lakini wananchi wanaongezeka kwa kiasi kikubwa hivyo endapo vyanzo hivyo vitaharibiwa ni hatari kwa uhai wa binadhamu kwani maji ni uhai.

"Tumezungumza suala la maji lakini tusisahau kulinda na kutunza vyanzo vya maji kama mboni ya jicho, maji ni uhai lakini pasipo kulinda na kutunza tunakwenda kujihatarishia uhai wetu, lakini hii ni dhamira yetu ya pamoja kuhakikisha tunashirikiana kwa pamoja viongozi, wataalamu wetu na wananchi katika kulinda na kutunza vyanzo vyetu vya maji" alisema.

"Sambamba na kulinda vyanzo pia tuna kulinda mazingira ili maji haya yawe toshelevu kwa vizazi vya sasa na vizazi vinavyokuja" aliongeza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.