Habari za Punde

Dk.Hussein Ameishukuru Bodi ya Taasisi ya "Mkapa Foundation" Kwa Kuona Umuhimu wa Kuichaguwa Zanzibar Kuwa Mwenyeji wa Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Mkapa 2022.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Uongozi wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa ukiongozwa na Mwenyekiti wa Taasisi hiyo (kulia kwa Rais) Dkt.Adeline Kimambo,Dkt.Ellen Mkondya Senkoro na Dkt. Ali Uki, walipofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo 27-11-2021.(Picha na Ikulu)

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi ameishukuru Bodi ya Taasisi ya ‘Mkapa Foundation’ kwa kuona umuhimu wa    kuichaguwa Zanzibar kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya kumbu kumbu ya Rais wa Awamu ya tatu ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Benjamin Mkapa mwaka 2022.                                                                                                   

Dk. Mwinyi ametoa shukrani hizo Ikulu Jijini Zanzibar wakati alipokuwa na kufanya mazungumza na Uongozi wa Bodi ya Taasisi ya ‘Mkapa Foundation’, iliongozwa na Mwenyekiti wake Dk. Adeline Kimambo.

Rais Dk. Mwinyi ameishukuru Taasisi hiyo kwa kazi kubwa inayofanya  na kusema kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itashirikiana na taasisi hiyo kikamilifu ili kufanikisha maadhimisho hayo yanayotarajiwa kufanyika mwezi Julai 2022,  sambamba na kuahidi kuchangia kikamilifu Mfuko wa Wakfu  wa Taasisi hiyo.

Aliipongeza taasisi hiyo kwa namna inavyotekeleza shughuli zake hapa Zanzibar mbali na kuwepo kwa changamoto za rasilimali.

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kuimarisha sekta ya afya hususan katika uimarishaji wa miundo mbinu na kubainisha kutumia kikamilifu mkopo iliopata  kutokana na fedha za Ugonjwa wa UVIKO-19.

Dk. Mwinyi alipongeza juhudi zinazochukuliwa na Taasisi ya ‘Mkapa Foundation’ katika kuimarisha sekta ya afya na kusema kwamba inathamini michango mbali mbali inayotolewa na taasisi hiyo, ikiwemo upatikanaji wa ajira kwa watumishi wake.

Alisema kuwa Serikali inakusudia kutengeneza utaratibu utakaowezesha watumishi walioajiriwa na Taasisi hiyo kuingia katika mfumo wa Serikali baada ya muda wa utumishi wao kumalizika kulingana  na mikataba yao.

Mapema, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya ‘Mkapa Foundation’ Dk. Ellen Mkondya Senkoro alisema maadhimisho ya kumuenzi Hayati Rais Benjamin Mkapa mwaka 2022 yatafanyika Zanzibar, ambapo yataambatana na shughuli mbali mbali ikiwemo Kongamano pamoja na Hotuba za Kitaifa.

Alisema Bodi hiyo iko katika hatua za mwisho za maandalizi ya maadhimisho hayo, ikijipanga kutuma maombi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili  kupata wajumbe watakaoingia katika Kamati ya maandalizi.

Mtendaji huyo alisema kuanzia mwezi Oktoba mwaka 2021, Taasisi ya ‘Mkapa Foundation’ imeanza utekelezaji wa Programu  mbali mbali hapa Zanzibar, ikiwemo ya kupambana na maradhi ya UVICO-19 na Kifua Kikuu.

Alisema taasisi imeajiri wafanyakazi wa kada mbali mbali katika sekta ya afya wapatao 105  Unguja na Pemba ambao wamesambazwa katika vituo 33 vya utoaji huduma, Bandarini na Viwanja vya Ndege, ambapo miongoni mwao watafanyakazi kwa mikataba ya miezi tisa (100) na watumishi watano kwa kipindi cha  mwaka mmoja.

Aidha, alisema taasisi hiyo imeendesha mafunzo mbali mbali kwa watendaji hao  ikiwemo ya maadili ya utumishi wa umma, Mama na mtoto na COVID -19 , huku matokeo ya awali yakionyesha kuwepo  mafanikio ya  ongezeko la wananchi wanajitokeza kuchanja ugonjwa huo .

Vile vile, alisema Taasisi hiyo imekuwa na mashirikiano makubwa  na Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia na  Watoto  Zanzibar katika nyanja mbali mbali, kwa lengo la kuimarisha sekta ya afya.    

Kitengo cha habari,

Ikulu Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Mwenyekiti wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa Dkt.Adeline Kimambo.(kulia kwa Rais) akiwa na ujumbe wake CEO wa Taasisi Dkt. Ellen Mkondya Senkoro na Dkt. Ali Uki,walipofia Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Mwenyekiti wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa Dkt.Adeline Kimambo.(kulia kwa Rais) alipofia Ikulu Jijini Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiagana na Ujumbe wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa, ukiongozwa na Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Dkt. Adeline Kimambo, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akiagana na Ujumbe wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa, ukiongozwa na Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Dkt. Adeline Kimambo, baada ya kumaliza mazungumzo yao yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo,27-11-2021.(Picha na Ikulu)


 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.