Habari za Punde

Naibu Waziri Mhe.Dkt.Mabula Aipa Kongole Manispa Kahama Kusaidia Idara ya Ardhi.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula aangalia magogo aliyoyakuta alipotembelea eneo la Viwanda la Zongomela wilayani Kahama kuona kama eneo hilo limezingatia mpango wa matumizi bora ya ardhi wakati wa ziara yake ya siku mbili katika mkoa wa Shinyanga.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wafanyabiashara katika eneo la Viwanda la Zongomela wilayani Kahama kuona kama eneo hilo limezingatia mpango wa matumizi bora ya ardhi wakati wa ziara yake ya siku mbili katika mkoa wa Shinyanga.

Na Munir Shemweta, WANMM KAHAMA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameipongeza halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga kwa kuijali na kuihudumia vizuri idara ya ardhi tofauti na halmashauri nyingine nchini.

 

Akiwa katika ofisi za Idara ya Ardhi katika Manispaa hiyo tarehe 26 Novemba wakati wa ziara ya kikazi katika mkoa wa Shinyanga Dkt Mabula alisema, halmashauri ya Manispaa ya Kahama imekuwa mfano kwa halmashauri nyingine kutokana na kuijali idara ya ardhi kwa kuipatia vifaa pamoja na ofisi kwa ajiili ya watumishi wake.

 

"Napenda nichukue fursa hii kumpongeza mkurugenzi wa halmashauri ya Manispaa ya Kahama na wilaya nzima kwa namna walivyoonesha ushirikiano kwa sekta ya ardhi maana ni halmashauri pekee ukilinganisha na nyingine kwa kuijali idara ya ardhi na kuona kuwa idara ya ardhi ni sehemu ya halmashauri" alisema Dkt Mabula.

 

Alieleza kuwa, ni  halmashauri chache zinazoijali idara ya ardhi hasa baada ya uamuzi kuhamishiwa wizarani ambapo baadhi ya wakurugenzi walianza kuitenga kwa kudai kuwa siyo sehemu ya halmashauri. Hali hiyo ni tofauti kabisa na mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama aliyeamua kutoa ofisi nzuri na kubwa kwa watumishi wa idara ya ardhi na kuweka wazi kuwa,  hata ukiingia ndani ya ofisi hizo unaona hii ni sehemu ya halmashauri.

 

Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Mabula alitoa rai kwa wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuwa, idara ya ardhi katika halmashauri ni idara kama zilivyo idara nyingine na wanao wajibu wa kuihudumia kwa kuipatia vitendea kazi kwa sababu kazi inazofanya ni za halmashauri na  inafanya miji ipendeze kwa kuwa halmashauri ni mamlaka ya upangaji.

 

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ametembelea eneo la viwanda la Zongomela katika manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga kujionea namna Manispaa hiyo ilivyowapatia eneo wafanyabiashara mbalimbali sambamba na kuona kama eneo hilo limezingatia mpango wa matumizi bora ya ardhi.

 

Akiwa katika eneo hilo linalojulikana kama Ummy Mwalimu Industrial Park ambalo halmashauri ya Manispaa ya Kahama imewapatia wafanyabiashra eneo hilo bure, Dkt Mabula aliitaka idara ya ardhi kuhakikisha inazingatia mipango ya matumizi ya ardhi katika eneo hilo sambamba na kuwapanga wafanyabiashara kulingana na shughuli zao ili kuepuka muingiliano.

 

" Uamuzi wa kuwaleta wafanyabiashra katika eneo hili ni mzuri na napenda niwapongeze lakini ni vizuri mkawapanga hawa wafanyabiashara kulingana na shughuli zao, huwezi kumpanga mama lishe na wanaoranda mbao hata kiafya siyo nzuri" alisema Dkt Mabula

 

Wafanyabiashara hao pamoja na kuishukuru halmashauri ya Manispaa ya Kahama kwa kuwapatia eneo wametaka kushughulikiwa kwa changamoto zinazowakabili katika eneo hilo

 

"Mhe. Waziri kwanza tunashukuru kwa kutembelewa na viongozi hapa Zongomela lakini tunaiomba serikali isikilize changamoto zetu ambapo kubwa ni miundombinu ya barabara pamoja na dampo la kutupia takataka" alisema mfanyabiashara wa Zongomela aliyejitambulisha kwa jina la Renatus Numbi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.