Habari za Punde

Mkutano wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mhe.Dkt.Saada Mkuya Azungumza na Waandishi wa Habari Kuhusiana na Utekelezaji wa Majukumu ya Ofisi Yake.

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe.Dkt. Saada Mkuya akisisitiza jambo wakati wa mkutano wake na Waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusiana na utekelezaji wa majukumu ya Ofisi yake, mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Ofisi hiyo Migombani Jijini Zanzibar.

1.0   UTANGULIZI

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais inasimamia maeneo manne ya utekelezaji ambayo ni uratibu na udhibiti wa dawa za kulevya, usimamizi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi, uratibu wa masuala ya watu wenye ulemavu pamoja na uratibu wa juhudi za kupambana na ukimwi.

Ofisi ya Makamu ya Makamu wa Kwanza wa Rais, inasimamia taasisi zifuatazo:-

i)                Ofisi ya Faragha ya Mhe. Makamo wa Kwanza wa Rais;

ii)              Idara ya Mipango, Sera na Utafiti;

iii)            Idara ya Uendeshaji na Utumishi;

iv)             Idara ya Mazingira;

v)               Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu;

vi)             Tume ya Kitaifa ya Uratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya;

vii)      Tume ya Ukimwi; na

viii)    Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira.

2.0   UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU

2.1  Usimamizi wa Mazingira na Mabadaliko ya Tabianchi

i.       Ofisi imeendelea kudhibiti uchimbaji holela wa maliasili zisizorejesheka kwa kutenga maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za uchimbaji wa mchanga na kifusi. Jumla ya maeneo 5 ya mchanga na 2 ya kifusi yamekaguliwa na kupewa ruhusa za kimazingira za kuchimbwa rasilimali hiyo. Maeneo ya mchanga ni Donge Kipange, Donge Mchangani, Pangatupu, Zingwezingwe na Matetema. Maeneo ya kifusi ni Jendele na Fumba.  Operesheni 35 za kusimamia maliasili zisizorejesheka zimefanyika Unguja na Pemba kati ya operesheni 50 zilizopangwa kufanyika.

 

ii.      Ofisi imeendelea kudhibiti uingizaji, biashara na matumizi ya mifuko ya plastiki. Jumla ya tani 2.8 zimekamatwa na kuteketezwa na watu 104 wamefikishwa katika vyombo vya kisheria. Hali hii inaonyesha kuendelea kuwepo kwa wafanyabiashara ambao wamekuwa wanaingiza na kuuza mifuko hiyo.

 

iii.   Katika kusimamia matumizi mazuri ya fukwe na bahari, maeneo 23 (13 Unguja na 10 Pemba) yamefuatiliwa, kusafishwa na baadhi yao kupandwa mikoko. Maeneo hayo ni Kilimani, Kisakasaka, Kibele, Nyamazi, Nungwi, Kiwengwa, Matemwe, Michamvi, Jambiani, Kihinani, Paje, Makunduchi na Chukwani kwa upande wa Unguja na Mkoani, Ole Kichanganazi, Mtangani, Kangani, Wambaa, Tundaua, Vumawimbi, Makangale, Pangawatoro, na Kichanjaani kwa Pemba. 

 

iv.   Katika kuzuia kuendelea kwa athari za mabadiliko ya tabianchi katika ukanda na ufukwe wa pwani wa Msuka Magharibi uliopo Wilaya ya Micheweni Pemba, ukuta wenye urefu wa mita 350 umejengwa ikiwa ni sehemu ya ukuta wa mita 500 unaokusudiwa kujengwa.  Aidha, misingi midogo ya kupitisha maji ya mvua ndani ya ukuta huo wa mita 350 imekamilika.

 

v.      Shughuli za kiuchumi zisizozingatia mazingira, zimeendelea kufanyika katika mitaa na maeneo yetu hapa Zanzibar. Hali hii imepelekea kuwepo kwa kesi 32 (viwanda vya matofali, magereji, maeneo ya kukata mbao na maeneo yanayofanya shughuli za weldings) zinazohusiana na uharibifu na uchafuzi wa mazingira  kwenye makaazi ya watu.

 

vi.    Ofisi imeandaa Muongozo wa Kimazingira wa uanzishaji na uendelezaji wa viwanda vya kusaga mawe, kifusi na utengenezaji wa matofali.  Kwa kushirikiana na Masheha, tunakamilisha utaratibu wa jinsi gani shughuli hizo zifanyike bila ya kuwa na athari za kimazingira katika maeneo ya kilimo, ufugaji, afya na makaazi kwa ujumla.

 

vii. Ofisi pia imeandaa Muongozo wa Ufuatiliaji wa Kimazingira kwa ajili ya Hoteli za Kitalii. Muongozo huo umelenga kuziwezesha Hoteli za kitalii kufanya ufuatiliaji binafsi katika utunzaji wa mazingira. Kupitia Muongozo huo Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira, itaweza  kuzifuatilia hoteli hizo ili kuimarisha utunzaji wa mazingira na kushajihisha utalii endelevu katika visiwa vya Zanzibar.

 

viii.   Jumla ya  miradi ya kiuchumi na maendeleo 89 imefanyiwa tathmini za kimazingira, kati ya miradi 99 iliyokuwa imepangwa. Tathmini hizo zinahusu athari za kimazingira (miradi 40), ukaguzi wa kimazingira (miradi tisa) na ripoti za kimazingira (miradi 40).

 

ix.      Serikali imenununa kifaa cha kukusanya taarifa za hali ya hewa ‘Automatic Weather Station” na kufungwa katika eneo la Skuli ya Mohamed Juma Pindua; Mkoani Pemba ili kuhakikisha taarifa za awali za hali ya hewa kwa ajili ya kuimarisha uhimili wa mabadiliko ya tabianchi zinapatikana kwa wakati. Kifaa chengine kama hicho kinategemewa kufungwa Makunduchi Unguja.

 

x.        Katika kuimarisha usimamizi wa mazingira ya ukanda wa pwani ya Hifadhi ya Bahari ya Mkondo wa Pemba (PECCA), Serikali imesafisha bwawa la maji machafu (Waste Water Treatment Facility) lililopo eneo la Bandataka linapokea maji machafu yanayotoka katika Shehia nne za Msingini, Chanjaani, Kichungwani na Madungu za Wilaya ya Chakechake. Usafishaji huo ni katika hatua za awali katika kufanya marekebisho ya mfumo wa bwawa hilo kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa usafishaji wa maji machafu ya bwawa hilo. 

2.2  Udhibiti na Usafirishaji wa Dawa za Kulevya

Zanzibar inakadiriwa kuwa na vijana zaidi ya 10,000 ambao wamo katika matumizi ya dawa za kulevya. Hadi mwishoni mwa mwaka 2020, watu ambao wako katika nyumba za upataji nafuu ni 349. Katika kuimarisha mapambano dhidi ya uingizaji, ulimaji, usambazaji na utumiaji wa dawa za kulevya, Serikali imetekeleza yafuatayo:-

i.     Rasimu ya sheria mpya ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya imeandaliwa na inatarajiwa kuwasilishwa katika kikao cha Baraza la Wawakilishi cha mwezi wa Disemba 2021. Sheria hiyo mpya itaiwezesha Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Dawa za Kulevya  kuwa na nguvu kisheria za kupambana na dawa za kulevya. Kupitia sheria hiyo, tutakuwa na maabara ya pamoja ambayo itahakikisha kwamba tunabaini uhalifu mapema zaidi, pamoja kuwa na kikosi maalumu ambacho kitakuwa na kazi ya kusimamia udhibiti wa uhalifu huu. Lengo letu pia ni kufupisha muda wa usikilizaji wa kesi zinazohusiana na dawa za kulevya.

 

ii.     Katika kuimarisha udhibiti wa dawa za kulevya zisirudi tena mitaani, jumla ya kilogram 94.573 zimeteketezwa. Dawa hizo ni bangi, heroini, kokeni na mirungi.  Aidha, tumepitia upya muongozo wa uteketekezaji wa dawa hizo kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Mrajis wa Mahakama Kuu. Hatua kadhaa zinaendelea kuchukuliwa, zikiwemo za udhibiti wa ushahidi wa dawa na usimamizi imara zaidi.

 

iii.     Katika kupunguza usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya, operesheni 52 zilifanyika katika mitaa iliyobainika kuwa ni hatarishi zaidi kwa pindi hiki. Mitaa hiyo ni Kikwajuni, Sogea, Kidongochekundu, Miembeni, Chuini, Jangombe, Migombani, Maeneo ya Mji Mkongwe kwa Wilaya ya Mjini, Nungwi, Chakechake, Pujini, Wete, baadhi ya maeneo ya Makunduchi (Kijini, Miwaleni na Mtegani) na maeneo yote yanayofanyika shughuli za utalii. Doria za mara kwa mara zitaendelea kufanyika ili kupunguza matumizi na biashara ya dawa za kulevya mitaani na kuimarisha mashirikiano baina ya wananchi na Serikali katika kupunguza wimbi la usambazaji wa dawa za kulevya.

 

iv.     Ofisi imebaini ongezeko la matukio 52 (sawa na asilimia 15) ya ukamataji ambapo ujumla ya matukio 393 yameripotiwa kwa kipindi cha Januari – Septemba 2021 ikilinganishwa na matukio 341 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho kwa mwaka uliyopita. Matukio hayo yamepelekea kukamatwa kwa 8.5kg za heroine na kufunguliwa kwa kesi 168, sawa na ongezeko la kesi 19 ikilinganishwa na mwaka uliopita ambapo gramu 761 za heroine zilikamatwa na kufunguliwa kesi 149. Aidha, jumla ya kilogramu 189.3 za bangi zilikamatwa na kufunguliwa kwa kesi 220, sawa na ongezeko la kesi 5 ikilinganishwa na mwaka uliopita ambapo kilogramu 39 za bangi zilikamatwa na kufunguliwa kesi 189. Vilevile, 180g za mirungi zilikamatwa na kufunguliwa kesi 5. Jumla ya gramu 191 za skanka zilikamatwa na kufunguliwa kesi 2.

 

v.     Ofisi, inakamilisha Ujenzi wa Nyumba ya Kurekebisha Tabia iliyopo Kidimni kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya kwa walioamua kuachana na dawa za kulevya na kujenga uwezo wao wa kichumi kwa kuwapa nyenzo za elimu na mafunzo ya stadi za maisha kabla ya kurudi kuungana na jamii katika shughuli za kiuchumi. Kwa upande wa Pemba, imefanikiwa kupata eneo kwa ajili ya ujenzi wa Kituo kama hiki katika kijiji cha Kiembe Raha, Kangagani. Uwepo wa vituo hivi utapunguza unyanyapaa na kuzidisha kukubalika kwa vijana hao ambao wameamua kuachana na matumizi ya dawa za kulevya.

 

vi.     Ofisi imefanikiwa kuanzisha huduma ya simu ya bure (free line) kwa ajili ya kuripoti taarifa za uhalifu wa dawa za kulevya. Kwa sasa, jamii inawasiliana na Tume moja kwa moja kupitia namba ya bure ya 0774 33 33 00 au kupitia simu binafsi za viongozi na watendaji wa Tume. Kupitia huduma hii, Ofisi tayari imeshapokea taarifa 37 na inaendelea kuzifanyia kazi. Huduma hii inawarahisishia wananchi kutoa taarifa zao juu ya uhalifu kwa usiri na kwa haraka jambo ambalo limerejesha imani kwa wananchi katika kutoa taarifa.

 

vii.     Ofisi imeendesha mafunzo ya ulinzi na usalama wa bandari (port security) kwa maafisa kutoka taasisi mbalimbali zinahusika na ulinzi na usalama wa bandari zikiwemo TRA, KMKM, Jeshi la Polisi, ZMA, ZAECA, Zimamoto na Uokozi, na Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka. Mafunzo hayo yalilenga kuimarisha ulinzi na ukaguzi wa abiria na mizigo bandarini.

 

viii.     Jumla ya Asasi Zisizo za Kiserikali 15 zinashirikiana na Ofisi yangu katika mapambano dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya na kutoa elimu kwa jamii.

2.3  Uratibu wa masuala ya UKIMWI

Kufikia Juni 2021, Zanzibar inakadiriwa kuwa na watu 8,147 wanaoishi na virusi vya ukimwi ambapo wanawake ni 5,621 na wanaume ni 2,526. Katika kipindi cha mwaka mmoja, Ofisi imetekeleza yafuatayo:- 

 

i.     Upimaji wa hiari umeongezeka hususan kwa vijana ambapo jumla ya vijana 3,098 walipima VVU (1,577 wanaume na 1,521 wanawake) na mmoja tu kati yao aligundulika kuwa na maambukizo ya VVU. Katika kipindi kama hicho mwaka uliopita, vijana 833 tu ndio waliweza kuhamasika kupima kwa hiyari ambapo wanaume ni 562 na wanawake ni 271.

 

ii.     Zanzibar bado inakabiliwa na tatizo la unyanyapaa kwa wanaoishi na VVU. Ofisi imeendelea kutoa elimu juu ya athari za unyanyapaa kwa njia ya sanaa shirikishi katika shehia 9 za Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba. Aidha, tunaendelea kuhakikisha kuwa masuala ya UKIMWI yanazingatiwa katika sekta zote kwa kuhamasisha Wizara, Taasisi za Serikali na Binafsi pamoja na Mashirika ya Umma kuwa na programu za kupambana na maradhi ya UKIMWI ili kudhibiti maambukizo mapya ya VVU kwa jamii yetu. Kwa sasa, tunashirikiana na Asasi Zisizo Za Kiserikali 47 kwa ajili ya kuendelea na kazi hizo.

 

iii.     Asilimia kubwa ya maambukizo yapo kwa makundi maalum yakiwemo wanawake wanaofanya baishara ya miili yao (12.1%), wanaotumia dawa za kulevya kwa kujidunga (5.1%) na wanaume wanaofanya mapenzi na wanaume wenzao (5%). Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Wizara ya Afya mwaka 2018, jumla ya wanawake 5,554 (4,854 unguja, 700 Pemba) wanakisiwa kujihusisha na biashara ya kuuza miili yao, wanaume 3,300 (3,000 Unguja na 300 Pemba) wanajihusisha na uhusiano wa jinsia moja na watu 2,600 (2,200 Unguja, 400 Pemba) wanakisiwa kutumia dawa za kulevya kwa njia ya kujidunga sindano. Ofisi imeendelea na jitihada za kuyafikia makundi hayo kwa lengo la kuyapa elimu na kupima maambukizo ya VVU kupitia programu za masafa (outreach) Unguja na Pemba. Hadi kufikia Septemba 2021, jumla ya watu 10,378 wa makundi maalumu wamefikiwa na 6,424 walikubali kupima VVU ambapo 69 waligundulika na maambukizo ya VVU.

iv.     Kuanzia Julai 2020 hadi Juni 2021 jumla ya mama wajawazito 56,165 wamefanyiwa uchunguzi wa VVU ambapo kati yao 104 (0.2%) waligundulika na VVU. Aidha watoto 381 waliozaliwa na mama wajawazito walichunguzwa afya zao na 5 waligundulika na maambukizo ya VVU ikiwa ni sawa na asilimia 1.3. Katika kudhibiti maambukizo ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kiwango cha maambukizo chini ya asilimia 5 kinachukuliwa kama ni ishara ya ufanisi katika kuwalinda watoto na maambukizo kutoka kwa mama zao.

 

v.     Katika kuibua mbinu za kudhibiti mazingira hatarishi yanayoweza kupelekea kuongezea kwa maambukizo ya VVU, Ofisi kwa kushirikiana na Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa Unguja na Pemba imeweka utaratibu kudhibiti upigaji wa ngoma na muziki; kufungia kabisa utoaji wa vibali vya ngoma kwa baadhi ya maeneo; kufungia baa na nyumba za kulala wageni na hoteli zinazoendeshwa kinyume na utaratibu au zinazochochea tabia hatarishi; pamoja na kudhibiti bandari zisizorasmi kwa kusimamia uingiaji wa wageni wasiokuwa na shughuli zinazoeleweka.

 

vi.     Elimu ya kuhamasisha mabadiliko ya tabia katika jamii imeendelea kutolewa kupitia vyombo vya habari, mikutano, machapisho, vipeperushi na mitandao ya kijamii ya Instagram, youtube na facebook.

2.4  Usimamizi wa masuala ya Watu wenye Ulemavu

Zanzibar inakisiwa kuwa na idadi ya watu wenye Ulemavu 74,500. Hata hivyo, Mfumo wa kidigitali wa Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu (Jumuishi Database), umefanikiwa kusajili watu 8,488 wenye ulemavu wakiwemo wanawake 4,043 na wanaume 4,445. Ili kuhakikisha kwamba haki na fusra zinapatikana kwa Watu wenye Ulemavu, yafuatayo yametekelezwa:-

 

i.     Ofisi imeimarisha Jumuishi Database kwa kuanzisha moduli ya usajili wa visaidizi (Asset Register) vinavyotolewa kwa wenye ulemavu ili kuleta ufanisi katika utoaji wa visaidizi hivyo na kuweka kumbukumbu sahihi za watu waliopatiwa visaidizi.

 

ii.     Jumla ya visaidizi 302 vya aina mbali mbali vimetolewa, kati ya hivyo visaidizi 104 vimepelekwa Pemba ambavyo wamepewa wanawake 56 na wanaume 48 na visaidizi 198 vimetolewa Unguja ambavyo wamepatiwa wanawake 113 na wanaume 85. Visaidizi hivyo ni viti vya magurudumu miwili 94, fimbo nyeupe 7 na kigari kimoja cha kisasa kinachotumia umeme.

 

iii.     Katika kupunguza wimbi la vitendo vya unyanyasaji kwa Watu wenye Ulemavu, ofisi imepokea na kufuatilia malalamiko 6 ya udhalilishaji Unguja na Pemba na kupelekea kesi 5 kufunguliwa mahakamani ambapo 3 zinaendelea kusikilizwa, mtuhumiwa mmoja ametiwa hatiani na 2 zinaendelea na uchunguzi wa polisi.

 

iv.     Katika kuimarisha zaidi usimamizi wa fursa na haki za watu wenye ulemavu, Ofisi imefanya mapitio ya awali ya Sheria ya Watu wenye Ulemavu (Haki na Fursa) No.9 2006 ambapo rasimu yake inaendelea kupata maoni ya wadau. Ofisi inaamini kuwa marekebisho ya sheria hii yataongeza ufanisi katika utoaji wa haki na fursa kwa Watu wenye Ulemavu pamoja na kuimarisha ukondoishaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu katika sekta mbalimbali zinazogusa maisha yao hali itakayoongeza kasi ya kuwafanya waishi maisha bora zaidi.

 

v.     Ili kuhamasisha uelewa juu ya haki na fursa za watu wenye ulemavu, Ofisi inashirikiana na Taasis Zisizo za Kiserikali 10 kuhamasisha marekebisho ya miundombinu ya majengo hususan ya Serikali kwa ajili ya kuweza kufikika kwa urahisi zaidi. Aidha, miundombinu ya barabara ambayo inaendelea kurekebishwa hususan kuwekwa kwa njia za watembea kwa miguu (walkways), kumesaidia kwa kiasi kikubwa kwa watu wenye ulemavu kupunguza vihatarishi vilivyokuwa vikitokea hapo awali katika barabara zetu.

 

 

 

 

 

2.5 Usikilizaji na utatuzi wa kero na malalamiko ya Wananchi

 

i.     Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, imeanzisha utaratibu wa kuwasikiliza wananchi mbalimbali na kupatiwa ufumbuzi wa hoja zao. Ofisi imefanikisha kupatiwa suluhu ya mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa Nungwi na Serikali ya Mkoa. Aidha, malalamiko ya wananchi wa Kendwa kuhusu kuchukuliwa eneo la soko, yanaendelea kufanyiwa kazi. Ofisi pia ilisimamia na hatimaye kuupatia suluhisho mgogoro baina ya mwekezaji wa kiwanda cha kusaga kokoto na wakulima wa Shehia ya Mwambe, Pemba.

 

ii.     Katika kuweka mbele masuala yenye maslahi kwa umma, Ofisi imefuatilia na kuyafanyia kazi malalamiko ya wananchi dhidi ya wamiliki wa viwanda vinavyofanya shughuli zao katika maeneo ya makaazi ya watu na kuleta kero kwa wananchi. Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuzuia ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha waya za umeme cha kampuni ya ZANTEXAS LTD katika maeneo ya Bweleo baada ya mjenzi kuthibitika kutokuwa na vibali vya mazingira na ZIPA pamoja na kuleta athari za kiafya na kimazingira kwa wanajamii wanaoishi jirani na kiwanda hicho.

 

iii.     Ili kuimarisha mawasiliano yake na umma, Ofisi inatumia mitandao ya kijamii kwa kutoa taarifa na kupokea maoni ya wananchi kupitia “facebook”, “instagram” na tovuti yenye anuani ya www.omkr.go.tz  .

  

iv.     Ofisi pia imeendelea kuyafanyia kazi malalamiko mbalimbali yanayowasilishwa katika mfumo wa “Sema na Rais” ambapo malalamiko 13 yamepokelewa, 6 kati ya hayo yamepatiwa ufumbuzi na 7 yanaendelea kufanyiwa kazi.

 

v.     Ofisi imeandaa Mkataba wa Huduma kwa Mteja (Customer Service Charter) ikiwa ni hatua ya kuimarisha mfumo wa utoaji wa huduma za Ofisi.

 

vi.     Hatua za kupunguza athari za Uviko 19 kwa watumishi wa umma zimeendelea kuchukuliwa kwa kuwajengea uelewa watumishi 273 juu ya kujikinga na maambukizo ya Uviko 19 kwa lengo la kupunguza na kukabiliana na maradhi hayo kwenye maeneo ya kazi na jamii kwa ujumla. Aidha, vifaa vya matumizi kwa ajili ya kinga ikiwemo vitakasa mikono (sanitizers) vimewekwa katika maeneo ya ofisi.

 

3.0   CHANGAMOTO

1.     Ukosefu wa vifaa vya kisasa vya utambuzi wa dawa za kulevya katika viwanja vya ndege na bandari Unguja na Pemba.

2.     Baadhi ya Watu wenye Ulemavu kushindwa kupata matibabu kutokana na kutomudu gharama za matibabu pamoja na uhaba wa dawa hospitalini kwa wenye ulemavu mchanganyiko.

 

3.     Maradhi ya UKIMWI kuzoeleka na kuonekana si tatizo tena katika jamii jambo linalopelekea kuongezeka kwa tabia na mazingira hatarishi  pamoja na maambukizo ya VVU.

 

4.     Umwagaji ovyo wa maji machafu yanayotapishwa kwenye vyoo na makaro katika Manispaa ya Zanzibar.

 

5.     Kuendelea kuwepo shughuli za uchimbaji holela wa mchanga na maliasili nyengine zisizorejesheka

 

4.0   HITIMISHO

Ofisi itaendelea na jitihada za kusimamia masuala ya usimaizi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi, udhibiti wa dawa za kulevya, mapambano dhidi ya UKIMWI na kulinda haki na fursa kwa watu Wenye Ulemavu ili kuinua uchumi na kuimarisha upatikanaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi kupitia dhana nzima ya Uchumi wa Buluu. 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.