Habari za Punde

Ulega: Wafugaji 'wakorofi' wachukuliwe hatua za kisheria

 

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega akiongea na Wananchi wa Kata ya Shungubweni, Wilayani Mkuranga alipokuwa katika ziara yake ya kutatua migogoro ya Wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi aliyoifanya Wilayani humo Novemba 1, 2021

Na. Mbaraka Kambona

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema wafugaji wanaoingiza mifugo yao kulisha katika mashamba ya wakulima ni wahalifu kama wahalifu wengine na ni lazima wachukuliwe  hatua za kisheria.

Ulega aliyasema hayo wakati wa ziara yake ya kutatua migogoro ya  Wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi aliyoifanya Wilayani Mkuranga, Mkoani Pwani jana.

"Ikiwa mtu amevamia shamba la mwenzie na mifugo yake ikala mazao katika shamba hilo, hapo hakuna kupindisha maneno, ni lazima haki itendeke, achukuliwe hatua za kisheria ikiwemo kumfidia yule ambaye mazao yake yameliwa na Mifugo," alisema Ulega

Waziri Ulega alitumia nafasi hiyo pia kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama kufanya kazi ya dhati kabisa kusimamia utatuzi wa migogoro hiyo kwa nia ya kutunza amani na utulivu katika Wilaya hiyo na nchi kwa ujumla.

Pia aliushauri uongozi wa Wilaya kuunda kamati maalum za maridhiano zitakazoshughulika na utatuzi wa migogoro baina ya Wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi ili watu wakae kwa amani na waweze kushirikiana.

Aidha, alimtaka Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Hadija Nasir kuhakikisha anaratibu vizuri zoezi la kuwatoa Wafugaji katika maeneo ambayo hayakupangwa kwa ajili ya shughuli za mifugo na kuwapeleka katika maeneo yaliyopangwa kwa ajili ya kazi ya ufugaji. 

"Sisi Wizara tumekusudia kufanya mapendekezo makubwa  na tumeshakubaliana kuandaa na kupeleka mapendekezo kwa Mamlaka za juu kuomba maeneo ambayo yatapangwa na kuwekewa miundombinu kama maji na majosho kwa ajili ya mifugo ili wafugaji waondoke katika maeneo ambayo yanawakutanisha na nyie wakulima," alifafanua

Kando na mipango hiyo ya Serikali ya kutenga maeneo, Waziri Ulega aliwataka wafugaji hao kuanza kupanga mikakati ya kuvuna mifugo yao ili waanze kupata faida ya kipato lakini pia itasaidia kupunguza migogoro baina yao na watumiaji wengine wa ardhi.

"Hapa zitakuja milioni 200 za kutengeneza Mnada wa Chamgoi utakaowawezesha wafugaji wavune mifugo ili kunufaisha Halmashauri, Taifa na Wafugaji wenyewe," alibainisha

Awali, Wakulima wanaofanya shughuli zao katika Wilaya hiyo akiwemo, Amiri Katundu wa Kijiji cha Dondo Dutani na Ramadhani Kingu wa Kijiji cha Kizapala kwa nyakati tofauti walisema kuwa Wafugaji waliovamia Wilaya hiyo wamewasababishia athari kubwa katika mashamba yao ikiwemo kukosa mavuno ya kutosha kwa sababu mifugo imekula mazao yao.

Naye, Mkuu wa Wilaya hiyo alisema kuwa kufuatia changamoto zilizojitokeza kutokana na uvamizi wa Wafugaji  wameshaanza kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti migogoro kati ya wafugaji hao na watumiaji wengine wa ardhi ikiwemo kufanya oparesheni za kudhibiti uingiaji holela wa mifugo katika Wilaya hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.