STATE HOUSE
ZANZIBAR
OFFICE
OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar January 13, 2022
Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi alikuwa mgeni rasmi
katika Burudani ya muziki wa Taarabu asilia, ilioandaliwa maalum kwa ajili ya
maadhimisho ya kusherehekea miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Hafla
hiyo imefanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdul-wakil, Kikwajuni jijini
Zanzibar, ambapo magwiji wa sanaa ya muziki wa
Taarabu asilia kutoka Kikundi cha Taifa Zanzibar, walionyesha umahiri wao
katika kuchararaza nyuzi na kughani nyimbo mbali mbali na kukonga nyoyo za
mashabiki wa sanaa hiyo kutoka Mikoa yote ya Zanzibar.
Katika
burudani hiyo nyimbo mbali mbali zilizopata kuvuma na kupendwa kutoka kwa
watunzi wabobezi na waimbaji nguli wa sana hiyo zilipata fursa ya kuimbwa na kuibua vifijo na nderemo.
Nyimbo
ya kwanza ambayo ilifungua pazia la burudani hiyo, ilikuwa ni ile ilioendana na
maudhui ya sherehe hizo, ambapo Mwimbaji nguli Al-anisa Fatma Dawa alighani kwa
ustadi mkubwa na kuwafanya watazamaji kuinuka kwenye viti na kumtunza.
Aidha,
kumalizika kwa nyimbo hiyo, kulitoa fursa kwa mwimbaji mahiri Al - anisa Hilda Mohamed
kughani nyimbo maarufu na iliowahi kupata sifa kubwa hapa Zanzibar,
ijuilikanayo kwa jina la ‘Nisubiri hadi lini’.
Kadri
muda ulivyosonga, ndivyo Burudani hiyo ya taarabu iliendelea kunoga na kuufanya usiku huo kuwa maalum kwa wapenzi
na mashabiki wa sanaa hiyo, hususan pale zilipoimbwa nyimbo maarufu kama vile,
Cheo chako, Kibali, Kweli ninae, Mpewa hapokonyeki, Lulu, Ubinafsi na choyo,
Lipi nilopenda kwako na kuhitimishwa na nyimbo ya Wahoi.
Nyimbo
nyengine zenye mnasaba na maudhui ya
sherehe hizo ambazo zilipata nafasi ya kuimbwa na kuibua shwangwe kubwa, ni pamoja na ile ya kumpongerza
Dk. Mwinyi kwa Uongozi wake, ilioimbwa na msanii nguli Nassor Hussein.
Katika
hafla hiyo, ambapo Rais Dk. Mwinyi aliambatana na Mama Mariam Mwinyi, watazamaji na mashabiki wa sanaa ya taarabu
asilia walikoshwa na kupata kile mioyo yao inapenda, baada ya kuwashuhudia
wasanii nguli kama vile Ustadh Idd Sued (mpendwa na wengi) na Profesa Mohamed
Elias wakiendelea kuimba kwa sauti ile ile iliyozoeleka kwa miaka na dahari na
kuthibitisha ule usemi wa ‘vya kale ni dhahabu’.
Viongozi
mbali mbali wa Kitaifa, akiwemo Makamo wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdalla
walishiriki.
Imetayarishwa
na Kitengo cha Habari,
Ikulu Zanzibar
No comments:
Post a Comment