Habari za Punde

Muongozo wa Kituo cha Uperesheni ya Dharura na Mawasiliano ,Kujadiliwa

.Akiwasilisha mada Dr Fredrick Methaw Salukele kutoka Chuo Kikuu Cha Dar-es-salamu kwa Wadau wa Maafa, kuhusu Muongozo wa kituo cha Operesheni ya Dharura na Mawasiliano, huko katika Ukumbi wa Kamisheni ya Maafa, Maruhubi .
Wajumbe mbali mbali walioziwasilisha Taasisi zao katika kujadili Muongozo wa Kituo cha Operesheni ya Dharura na Mawasiliano, wakimfuatilia kwa makini Muasilishaji Dr Fredrick Methaw Salukele kutoka Chuo Kikuu Cha Dar-es-salamu, huko katika Ukumbi wa Kamisheni ya Maafa, Maruhubi .

Picha ya pamoja ya Wadau mbali mbali wa Maafa walioshiriki Kikao cha kujadili  Muongozo wa Kituo cha Operesheni ya Dharura na Mawasiliano, huko katika Ukumbi wa Kamisheni ya Maafa, Maruhubi .

 

Na Khadija Khamis –Maelezo .11/02/2022,

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Kamisheni ya kukabiliana na Maafa  Muhidin Ali Muhidin amewataka watendaji wa Taasisi mbali mbali zilizomo katika utekelezaji wa Mpango wa kukabiliana na maafa kufanya kazi kwa mashirikiano kwa mujibu wa muongozo.  

 

Aliyasema hayo huko Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa, Maruhubi wakati wa Kujadili Muongozo wa Kituo cha Operesheni ya Dharura na Mawasiliano  kwa wadau mbali mbali wa maafa . 

 

Alisema masahihisho ya muongozo huo utasaidia utekelezaji bora wa majukumu ya kazi wakati wa maafa yakitokea.

 

Nae Muwasilishaji wa Muongozo wa kituo cha Operesheni ya Dharura na Mawasiliano, Dr. Fredrick Methaw Salukele, kutoka Chuo Kikuu cha Dar-es-salamu ameeleza kuwa muundo umehusisha wadau wote wa maafa pamoja na majukumu yao ya kiutendaji .

Alifahamisha hatua mbali mbali zinazohitajika kuchukuliwa iwapo dharura ikitokea kwa kila mdau kutekeleza majukumu ambayo anapaswa kutekeleza kwa mujibu wa muongozo

Alieleza majukumu na uwajibikaji wa kazi wakati wa dharura ikitokea kwa kila Taasisi husika itawajibika kulingana na muongozo uliopo ikisimamiwa na Meneja na wasaidizi wake .

“Pindipo dharura ikitokea wafanyakazi watakuwepo kazini kwa masaa 24 hadi dharura itakapomalizika watarejea kufanyakazi kwa utaratibu wa kawaida,”alisema Dr Fredrick

Dr Fredrick alieleza utaratibu maalum  wa kupiga simu kipindi cha dharura ambacho majanga yametokea kwa kuwasiliana na wahusika kwa hatua za haraka na baada ya kumaliza tukio, kujipanga upya katika majukumu mengine.  

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Divisheni ya Operesheni na Huduma za Kibinaadam  Haji Faki Hamduni,ameridhishwa na uwasilishwaji wa muongozo  huo ambao umewawezesha washiriki kuwajengea uwezo wa kiutendaji .

Amesema Kamisheni inatoa shukrani kwa Muwasilishaji huyo na kujenga imani kubwa kutokana na muongozo mzuri aliouwasilisha kwa Wadau.

 Muongozo wa kituo cha Operesheni ya Dharura na Mawasiliano ni muendelezo wa majadiliano na mapendekezo mbali mbali yanayotakiwa kubadilishwa kwa mujibu wa makubaliano ya wadau kwa pamoja waliomo katika mpango huo.

Wadau waliohudhuria marekebisho ya Muongozo huo kutoka Taasisi mbali mbali za Serikali ikiwemo Vyombo vya Ulinzi na Usalama, Jeshi la Zimamoto na Uwokozi, Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo ( KMKM) Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA), Mamlaka ya Uwanja wa ndege na Taasisi nyenginezo .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.