Habari za Punde

Waziri Mhe.Dkt.Mabula Aeleza nia ya Serikakli Kutokomeza Makazi Holela Nchini Tanzania.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza wakati wa kikao cha siku moja kati ya Wadau wa Wizara ya Ardhi na Sekta binafsi kujadili changamoto mbalimbali kuhusu sekta ya Ardhi  jijini Dar es Salaam Mei 23, 2022. 

Na Athony Ishengoma na Munir Shemweta, WANMM

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula amesema Wizara yake haitarajii kuwepo makazi holela nchini baada ya mwaka mmoja kwa kuwa serikali ilijiwekea malengo ya miaka kumi ya kurasimisha maeneo ya makazi holela.

Zoezi la urasimishaji makazi holela lilianza mwaka 2013 na linarajiwa kukamilika 2023.

Alisema, serikali inakusudia kupima kila kila kipande cha ardhi hivyo kuwataka Maafisa Ardhi kuhakikisha wanatangulia kupima ardhi tofauti na sasa ambapo wananchi wanawahi kufanya shughuli za ujenzi kabla mipango miji kufanyika.

Dkt. Mabula alisema hayo wakati akifungua kikao cha siku moja kati ya Wadau wa Wizara ya Ardhi na Sekta binafsi kinachofanyika ukumbi wa Msenga Jengo la Millenium Towers Dar es Salaam kujadili changamoto mbalimbali zinazohusu sekta ya Ardhi. 

Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, serikali katika kutekeleza miradi mbalimbali ya upimaji ardhi imeshirikisha sekta binafsi na kulaani tabia ya wabia hao kushindwa kukamilisha kazi zao kwa wakati jambo alilolieleza linachangia suala zima la migogoro inayosikika kwa sasa.

‘’Serikali imetoa kazi kwa sekta binafsi lakini wametukwamisha na ndio kelele unazozisikia kwa sasa’’ Aliongeza Dkt Mabula Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Dkt Mabula amelitaji ongezeko la makazi holela kuwa changamoto kubwa kwa kuwa wananchi wanaonekana kuwa mbele huku wataalamu wakiwa nyuma na kuwataka wataalam hao kujipanga ili kuendana na kasi ya maendeleo.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula changamoto nyingine inayoikumba Wizara yake ya Ardhi kuwa ni wavamizi wa ardhi ambao wameshamiri hususani eneo la Dar es Salaam na kuongeza kuwa wakati mwingine wanavamia ardhi ambayo tayari imemilikishwa kisheria.

Kuhusu fidia ya ardhi, alisema kwa sasa wanachi wanajua thamani ya ardhi tofauti na huko nyuma kwani wakati mwingine wamiliki wa ardhi wanapandisha thamni ya ardhi kuliko thamani halisi inayotakiwa kutokana na uelewa mkubwa wa thamani ya ardhi.

Akigeukia uanzishwaji wa Ofisi za Ardhi za Mikoa Waziri Dkt Mabula alisema, kuna ofisi za ardhi Mikoani lakini wananchi wamekuwa na tabia ya kufuata huduma ya ardhi Wizarani na kuhoji kwa nini ofisi za ardhi zipo mikoani lakini wananchi wanakwenda kufuata huduma Wizarani.

‘’Niwaambie Wananchi kuwa Makamishna wa Ardhi wa Mikoa wanayo mamlaka kamili ya kutatua migogoro ya ardhi mkoani hivyo hauitaji kuja Wizarani’’ Dkt Mabula

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Allan Kijazi alisema, Wizara itambua uhitaji mkubwa wa kuboresha mifumo ya utawala bora katika sekta ya ardhi kwenye kupanga, kupima, kutoa hati miliki na kutatua migogoro ya ardhi.

Kwa mujibu wa Dkt Kijazi, katika kulitambua suala hilo Wizara ya Ardhi imeshaanza kuchukua hatua za kuandaa muongozo wa utawala bora katika maeneo hayo manne ili kuhakikisha sera, sheria, kanuni na miongozo mbalimbali inayosimamia sekta hiyo inajumuisha kanuni za utawala bora.

‘’Nia ya kuimarisha utawala bora kwenye sekta ya ardhi ni kulinda haki za umiliki za waendelezaji sekta ya ardhi kwa kuongeza uwazi uwajibikaji kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na kuhakikisha usawa kwenye kutoa maamuzi ya masuala ya ardhi pamoja na kuimarisha ushirikishwaji wa wadau katika kutoa maamuzi’’ alisema Dkt Allan Kijazi.

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Allan Kijazi akizungumza katika kikao cha Wadau wa Wizara ya Ardhi na Sekta binafsi kujadili changamoto mbalimbali kuhusu sekta ya Ardhi kilichofanyika  jijini Dar es Salaam
Kamishna wa Ardhi nchini Nathaniel Methew Nhonge wakati wa kikao cha  Wadau wa Wizara ya Ardhi na Sekta binafsi kujadili changamoto mbalimbali kuhusu sekta ya Ardhi kilichofanyika  jijini Dar es Salaam
Sehemu ya washiriki wa kikao cha siku moja kati ya Wadau wa Wizara ya Ardhi na Sekta binafsi kujadili changamoto mbalimbali kuhusu sekta ya Ardhi kilichofanyika  jijini Dar es Salaam
Washiriki wa kikao cha Wadau wa Wizara ya Ardhi na Sekta binafsi wakifuatilia hotuba ya ufunguzi iliyotolewa na Waziri wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula  jijini Dar es Salaam 

Sehemu ya washiriki wa kikao cha kikao cha Wadau wa Wizara ya Ardhi na Sekta binafsi kujadili changamoto mbalimbali kuhusu sekta ya Ardhi kilichofanyika  jijini Dar es Salaam Mei 23, 2022. 

(PICHA NA WIZARA YA ARDHI)

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.