Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla Akabidhi Tuzo ZFF.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akimkabidhi Tuzo Maalum Mkurugenzi Mwendeshaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ)  Dkt. Muhsin Salim Masoud kwa Mchango mkubwa wa kudhamini Ligi Kuu Zanzibar2021-2022.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akimkabidhi Tuzo ya Shukurani Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamadni na Michezo Fatma Hamad Rajab kwa niaba ya Wizara  ya Habari kwa mchango mkubwa kufanikisha Ligi Kuu Zanzibar 2021-2022.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akimkabidhi Tuzo Mchezaji Bora mwenye thamani wa Ligi Kuu Zanzibar (MVP) Is’hak Said Mwinyi (Babuu) wa Klabu ya KMKM katika hafla ya ugawaji Tuzo za ZFF PBZ Awards 2022 iliyofanyika katika ukumbi wa Abla Beach Apartment Betrasi Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Wadau wa Michezo katika hafla ya usiku wa Tuzo za ZFF PBZ Awards 2022 iliyofanyika Ukumbi wa Abla Beach Apartment Betrasi Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Wadau wa Michezo katika hafla ya usiku wa Tuzo za ZFF PBZ Awards 2022 iliyofanyika Ukumbi wa Abla Beach Apartment Betrasi Zanzibar.

Na.Abdulrahim Khamis.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameupongeza Uongozi wa Benki ya Watu wa Zanzibar kwa kuunga mkono Mpira wa Miguu Zanzibar ili kufanyia kazi dhamira ya Rais Dkt. Mwinyi kutaka kurudisha hadhi ya Michezo Zanzibar.

Mhe. Hemed ameeleza hayo katika hafla ya Usiku wa Tuzo za ZFF PBZ Awards 2022 iliyofanyika katika Ukumbi wa Abla Beach Apartment Betrasi Zanzibar.

Amesema hatua iliyochukuliwa na PBZ kudhamini Ligi Kuu Zanzibar pamoja na Kampuni ya AZAM MEDIA  imesaidia kuleta muamko wa wanamichezo katika ushindani hatua ambayo imewadhihirishia wazanzibari kuwa na ushabiki mkubwa wa Mpira wa Miguu.

Ameeleza kuwa utoaji wa Zawadi kwa washindi na Wadau mbali mbali  wa Michezo unaongeza hamasa, nguvu na hamu ya kuendelea kufanya vizuri wakifahamu kuwa michezo ni Afya na ni Urafiki.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewasihi Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) kukaa pamoja na wadau wa Mpira hasa wachezaji wa Zamani ili kupata maoni yao kwa lengo la kumaliza Changamoto zinazoikabili Tasnia ya Soka Zanzibar.

Aidha ameeleza kuwa ziko changamoto zilizopo baina ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambapo amewataka Viongozi wa pande zote mbili kukaa pamoja ili kumaliza changamoto hizo.

Akigusia ushiriki wa Wachezaji kutoka Zanzibar kwenye kuunda Timu ya Taifa ya Tanzania Mhe. Hemed ameeleza kuwa ni vyema TFF kuweka usawa kwa kuwapa fursa wachezaji kutoka Zanzibar kushiriki katika Timu hiyo ili kukuza vipaji vyao.

Aidha amesema ni vyema kwa Vyama vya Mpira ya Miguu kufanya mapitio Sheria na kanuni za kufundishia wakufunzi wa Mpira hasa gharama za ushiriki ili kutoa fursa kwa wakufunzi kushiriki mafunzo hayo na kuacha kutegemea wakufunzi kutoka nje ya Zanzibar.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed amewashukuru wadau wa Michezo na Wananchi kwa ujumla kwa kudumisha Amani na utulivu viwanjani kipindi cha michuano hatua ambayo imeipa faraja Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Nae Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Fatma Hamad Rajab ameeleza  kuwa Wizara kwa kushirikiana na ZFF  itaendelea kusimamia fedha zinazopatikana kwa ajili ya Michezo ili zitumike kama zilivyokusudiwa na kuwataka wadhamini kuendelea kuunga mkono ili kukuza soka Nchini.

Nae Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) Abdul Latif Ali Yassin ameeleza kuwa hatua iliyochukuliwa na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) pamoja na wadau mbali mbali inaonesha Imani waliokuwa nayo kwa Shirikisho hilo ambapo amewaahidi wadau hao kuendeleza mashirikiano ili kufikia malengo ya kuwepo Mpira wa Miguu Zanzibar.

Ameeleza kuwa hatua ya PBZ kuendelea kudhamini msimamo ujao wa Ligi Kuu Zanzibar inaakisi utayari wao katika kuunga Mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kusimamia Soka Nchini.

Nae Mkurugenzi Muendeshaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) Dkt. Muhsin Salim Masoud ameeleza kuwa PBZ imeona muamko uliopo katika Soka jambo ambalo limewapelekea kuwa wadhamini wakubwa wa Ligi Kuu Zanzibar.

Aidha ameeleza kuwa udhamini wao ni kuunga mkono azma ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kutaka kurudisha hadhi ya Soka Nchini.

Katika hafla hiyo Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) lilitiliana saini makubaliano baina yao na Benki ya watu wa Zanzibar (PBZ) kwa kudhamini Ligi Kuu Zanzibar kwa muda wa Miaka Mitano pamoja na Mkataba wa utayarishaji wa Jezi ya Timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) kwa Kampuni ya Sheria Ngoi Company Limited.

Afisi ya Makmu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

17 /07/2022

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.