Habari za Punde

SERIKALI KUSHIRIKIANA NA WADAU WA MAENDELEO SEKTA YA KILIMO.

 

Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya Kilimo Bwa. Joseph Kiraiya akizungumza katika  kikao cha majadiliano kati ya Serikali na Wadau wa Maendeleo kuhusu Mkakati wa Nchi wa AGRA TANZANIA katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Jijini Dodoma.
Afisa Mradi kutoka AGRA, Bwa. Liston Njoroge  akiwasilisha Rasimu ya Mkakati wa Nchi ya Tanzania kwa Mapitio ya Kiufundi, Maoni na Michango katika kikao hicho.

Baadhi ya washiriki wakifuatilia kikao kilichofanyika kati ya Serikali na Wadau wa Maendeleo kuhusu Mkakati wa Nchi wa AGRA TANZANIA katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Jijini Dodoma.

(PICHA ZOTE NA OFISI YA WAZIRI MKUU)Na Mwandishi wetu- Dodoma

Serikali imesema itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo kuhakikisha  inatatua changamoto zinazokabili sekta hiyo  ili kuwawezesha wakulima kufanya kilimo kinachoendana na teknolojia  kitakachosaidia kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja  na kuchangia pato la Taifa.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya Kilimo Bwa. Joseph Kiraiya wakati akiongoza kikao cha majadiliano kati ya Serikali na Wadau wa Maendeleo kuhusu Mkakati wa Nchi wa AGRA TANZANIA katika Ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu Jijini Dodoma.

Mkurugenzi huyo alisema  Programu ya kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) ni mpango wa miaka 10  unaolenga kuleta mageuzi ya sekta ya kilimo (Kilimo, Mifugo na Uvuvi), kuongeza uzalishaji wenye tija  na kufanya kilimo kuwa cha kibiashara.

“Mpango huu nia yake ni kuleta mageuzi kwa sekta hii kama tunavyojua ina mchango mkubwa sana katika pato la Nchi yetu hata wakulima kipato chao kitaongezeka, tutakuwa na chakula cha kutosha, usalama wa chakula na lishe,” alisema Mkurugenzi huyo.

Aidha Makamu wa rais anayesimamia Sera kutoka Shirika la Muungano wa Mapinduzi ya Kijani Afrika (AGRA) Dkt. Nwafor Apollos alibainisha kwa shirika hilo liko tayari kufanya kazi na serikali katika kuboresha  mazingira ya kilimo nchini.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.