Habari za Punde

PSSSF Yaendelea Kuboresha Huduma za Wastaafu Kuhakiki Taarifa Zao kwa Kutumia Alama za Vidole (BIOMETRIC)

Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma, PSSSF, Bw. James Mlowe (kulia) akizungumza na Afisa Uhusiano Mwandamizi, NSSF, Bw. Sebera Fulgence kwenye banda la Ushirikiano namba 13 linalotumiwa kwa pamoja na Mifuko hiyo ya Hifadhi ya Jamii.

NA KHALFAN SAID, SABASABA                                                                                                  

KATIKA kuhakikisha Wastaafu wanapata huduma kwa haraka na kwa urahisi zaidi, Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umeanzisha mfumo wa kielektroniki wa kuhakiki taarifa kwa kutumia alama za vidole (biometric), Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma wa Mfuko huo Bw. James Mlowe amesema.

Bw. Mlowe ameyasema hayo leo Julai 2, 2022 wakati akiwahamasisha Wastaafu na Wanachama wa Mfuko huo wakiwemo wananchi kutembelea banda namba 13 la Ushirikiano baina ya PSSSF na NSSF kwenye Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam katika viwanja vya Julius Nyerere maarufu Sabasaba barabara ya Kilwa jijini.

“PSSSF tuna wastaafu wanaopokea pensheni kila mwezi zaidi ya 160,000, ni utaratibu wa kisheria na kikanuni kwamba Mstaafu anatakiwa kujihakiki mara moja kila mwaka” alisema

Alisema lengo la kuhakiki ni kutaka kujua kuwa taarifa za wastaafu wanaopokea pensheni  kila mwezi zimebadilika au ziko vile vile, zoezi hili limekuwa likifanyika kwa miaka mingi ingawa limekuwa na changamoto mbalimbali.

“Badala ya utaratibu wa awali wa Mstaafu kufika ofisini na kujaza fomu na kuja na viambatanisho mbalimbali tumeona mfumo huu unaleta usumbufu kwahivyo tumekuja na suluhisho ambapo Mstaafu anaweza kujihakiki kwa kutumia alama za vidole (biometric) ambapo mwanachama anaweza kujihakiki sehemu yoyote.” Alifafanua.

Aidha Meneja huyo alisema kwenye siku za usoni mwanachama anaweza kutumia simu janja na kujihakiki popote na wakati wowote.

Amewahimiza wastaafu na wanachama wa PSSSF wanaotembelea Maonesho hayo kufika kwenye banda namba 13 ili waweze kujihakiki na kuchukuliwa alama zao za vidole na kwa hali hiyo huduma ziweze kuwafikia huko waliko.

“Miundombinu yote inayopatikana kwenye ofisi zetu zilizoenea nchi nzima inapatikana hapa sabasaba kwa hivyo mwanachama, mwanachi, fika kwenye banda letu la ushirikiano na NSSF ili tuweze kukuhudumia na kukupa elimu ya hifadhi ya jamii.” Alisema.

Meneja Uhusiano na Elimu kwa Umma, PSSSF, Bw. James Mlowe (kulia) akiwahudumia wanachama kwenye banda la Mfuko huo viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam Julai 2, 2022.


Mwanachama akihudumiwa
Mwanachama akihudumiwa
Mwnaachama akipitia taarifa zake za Michango, baada ya kuhudumiwa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.