Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya
Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Switbert Mkama akipata maelezo kutoka kwa Bw. Alawi
Hija Mratibu wa Mradi wa Ebarr kwa upande wa Zanzibar kuhusu matumizi ya boti 6
zilizotolewa na Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa
kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini – EBARR unaosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais katika Shehia tatu za Matembwe.
Bw. Makame Ame mmoja wa
wanufaika wa Mradi wa Boti 6 zilizotolewa kupitia Mradi wa
Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini – EBARR unaosimamiwa
na Ofisi ya Makamu wa Rais katika
Shehia tatu za Matembwe akitoa manufaa ya boti hizo katika kikundi chake, leo
Agosti 03, 2022.
Serikali imesema itaendelea
kutafuta fedha za kutekeleza miradi mbalimbali ya kukabiliana na athari za
Mabadiliko ya Tabianchi kwa pande zote mbili za Muungano.
Hayo yamesemwa leo Agosti 3,
2022 na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dkt. Switbert
Mkama alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mradi wa Kuhimili
Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini – EBARR unaotekelezwa
katika Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja
na kusimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Rais.
Akiwa katika eneo la Mbuyutende Dkt.
Mkama ametoa rai kwa wanufaika wa mradi wa
boti (6) za uvuvi zilizotolewa kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mifumo
Ikolojia Vijijini (EBARR) kutumia boti hizo katika shughuli za uvivu na utalii
kama shughuli mbadala ya kujiongezea kipato na kutofanya shughuli zinazochangia
uharibifu wa mazingira kama vile kuchoma mkaa.
Boti
hizo zenye thamani ya shilingi milioni mia moja sitini na mbili zina uwezo wa kubeba
mizigo kiasi cha tani 2.9 kwa wakati mmoja na zimekabidhiwa kwa vikundi vya
wavuvi katika Shehia tatu za Matemwe.
“Boti
hizi ziongeze hamasa kwenu ya kuwa na umoja na mshikamano miongoni mwenu, ziweze
kuwanufaisha na kuwaongezea kipato huku mkizingatia hifadhi ya mazingira” Alisisitiza
Dkt.Mkama
Alisema kuwa Ofisi ya Makamu wa Rais inaendeleza ushirikiano mzuri uliopo
baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SJMT) na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Pia,
ameridhishwa na kasi ya uchimbaji wa visima sita na ujenzi wa minara ya matanki
ya maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na kilimo cha mbogamboga kwa wakazi
wa Shehia 3 za Matemwe-Kijini, Matemwe Mbuyutende na Matemwe Jugakuu.
Nae Mratibu wa Mradi
huo kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. James Nyarobi amesema maeneo ya Mradi
yamechaguliwa kwa kuzingatia maeneo kame yenye jamii za wakulima, wafugaji na
wavuvi kwa lengo la kuongeza uwezo wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika
jamii za vijijini kwa kuimarisha mifumo ikolojia na shughuli mbadala za
kujiongezea kipato.
Katika kukabiliana na
athari za mabadiliko ya tabianchi, Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais
inaratibu utekelezaji wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia
Mifumo ikolojia Vijijini wenye thamani ya Shilingi za kitanzania Bilioni 17 ikiwa
ni ufadhili wa Mfuko wa Mazingira Duniani (GEF). Mradi huu unatekelezwa katika
Wilaya tano nchini, ambazo ni Simanjiro, Kishapu, Mvomero, Mpwapwa na Kaskazini
A Unguja.
No comments:
Post a Comment