Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Viongozi mbalimbali pamoja na Mawakili wa Serikali kabla ya kuzindua Chama cha Mawakili wa Serikali, nembo na Mfumo rasmi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma tarehe 29 Septemba, 2022.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Mawakili wote wa Serikali ambao hawajasajiliwa kwenye rejista ya Mfumo wa Taarifa wa Mawakili wa Serikali kujisajili kabla ya muda kupita ili watambulike na Mfumo wa Kieletroniki wa Taarifa wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ujulikanao kwa jina la OAG-MIS.
Mhe Rais Samia ameyasema
hayo leo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mawakili wa Serikali kabla ya kuzindua
Chama cha Mawakili wa Serikali (Public Bar Association) uliofanyika kwenye
Ukumbi wa Jakaya Kikwete Dodoma wenye Kauli mbiu isemayo, “Utekelezaji wa
Majukumu Unaozingatia Sheria ni Nyenzo Muhimu kwa Maendeleo ya Taifa”.
“Amri inapotoka Wanasheria
wajisajili na muda umetolewa kama mtu hajajisali awe na dharura ya maana sana, ama
alikuwa mgonjwa hospitalini hawezi au alipokuwa hakuna mtandao hakupata taarifa
kwa wakati lakini kama muda utapita na usajili hajafanya basi Mwanasheria Mkuu
nakutaka kusimamia hilo”, amesema Mhe. Rais Samia
Amemtaka Mwanasheria
Mkuu wa Serikali kuwahimiza wale ambao bado hawajajisajili wajisajili kwenye
mfumo wa OAG-MIS vinginevyo baada ya muda kupita hawatatambulika kama Mawakili
wa Serikali na itabidi watafute sekta za nje wajisajili au kupewa msamaha na
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mhe. Rais Samia
amepongeza uanzishwaji wa Chama cha Mawakili wa Serikali cha kitaaluma na
kusema uwepo wake utasaidia zoezi la kuratibu utendaji kazi wa Mawakili wote wa
Serikali walio katika utumishi wa umma nchini na mmepata mlezi mzuri
Mwanasheria Mkuu wa Serikali anayeweza kuwasemea katika masuala yenu ya
kitaaluma, kikazi, kinidhamu na kimaslahi.
“Lakini nimefurahishwa
kusikia kwamba Chama hiki sasa kilichoundwa kitafanya kazi kwa karibu na Chama
cha Mawakili cha Tanganyika (TLS), lakini pia nimefurahishwa na kusikia
uhusiano wa karibu wa kazi baina yenu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar”, amesema Mhe. Rais Samia
Aidha, amesema itakuwa
ni rahisi kuwasiliana kupitia mfumo huo wa Mawakili wa Serikali ambao
ameuzindua na kusema ni dhahiri maboresho hayo yataongeza ari na tija kwa
Mawakili wa Serikali wanapotekeleza majukumu yao katika maeneo mbali mbali
nchini.
Akimkaribisha Mhe.
Rais Samia, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema
mkutano huo ulitanguliwa na kikao kazi cha Wakuu wa Idara na Vitengo wa Wizara,
Taasisi, Idara na Halmashaurizote nchi nzima na kuelezwa kuhusu mpango wa
kuanzisha Chama cha Mawakili wa Serikali.
Dkt. Ndumbaro amesema
chama hiki kitakuwa kikisimamia masuala ya kitaaluma na masuala ya kimaadili ya
Wanasheria na ni fursa nzuri ya kutoa changamoto za kimaadili ambazo zimekuwa
zikiwakabili na itawezekana tu kama Mhe. Rais Samia atakubali ombi la kuzindua
chama hicho.
“Mhe Rais Samia kupitia
Chama cha Mawakili wa Serikali tunatarajia kwamba chama hiki kitaleta umoja
wenye nguvu na jukwaa mahususi kabisa la kuishauri Serikali katika mambo
mbalimbali ya kisheria na tunatarajia kwamba itakuwa ni sehemu ya majidiliano
ya kisheria kwa wanasheria wa Serikali ambalo lilikosekana huko nyuma.
Amewakumbusha Mawakili wa
Serikali kwamba kuwa Wakili wa Serikali ni heshima kubwa na heshima ya kuwa
Wakili inaendana na wajibu hivyo wanapaswa kuitumikia Serikali ipasavyo, kutumia
sheria kupunguza migogoro inayoweza kujitokeza ndani ya Serikali.
Awali Mwanasheria Mkuu wa
Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi amewataka watendaji kuhakikisha
wanawatumia vizuri wanasheria waliopo kwenye rejesta ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali kupata ushauri kabla hajaingia kwenye mikataba au kabla ya kuvunja
mikataba ili wazingatie kanuni na taratibu.
Mhe. Jaji Dkt. Feleshi
amesema chama kitakuwa ni jukwaa la Mawakili kujadili masuala mbalimbali ya
kisheria yakiwepo ya kimafunzo yanayohusiana na utoaji wa huduma za kisheria na
kutatua malalamiko ya kisheria kutoka kwa wadu mbalimbali.
Naye Wakili wa Serikali
kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Bw. Msalama Mkama ameishukuru Serikali
kwa kuwa na maono ya mbali na kuanzisha Chama cha Mawakili wa Serikali ambacho
kitakuwa kama jukwaa kwa Mawakili hao kujadili masuala yao ya msingi kwenye Sekta
ya Sheria.
Bw. Mkama amesema kuwa chama
hicho kitaiwezesha Serikali kuwaunganisha Mawakili na kujadili changamoto zao
kwa pamoja na kuiwezesha Serikali kufahamu idadi na utendaji kazi wa Mawakili
katika Wizara, Taasisi, Sekretariati za Mikoa na Halmashauri zote nchini.
“Chama kitawawezesha
Mawakili kushirikishana katika ujuzi walio nao na kubadilishana uzoefu wa
utendaji kazi katika kusimamia mashauri ya Serikali kutoka kwenye taasisi zao
na pia kutatua changamoto walizonazo kwa kutumia uzoefu walio nao.
Mkutano huo umehudhuriwa na
Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Boniphace Luhende, Mkurugenzi wa Mashtaka, Slyvester Mwakitalu, Viongozi
waandamizi wastaafu wa Sekta ya Sheria nchini akiwemo Mtemi Andrew Chenge.
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali
No comments:
Post a Comment