Na Happiness Shayo - WMU
Wawekezaji wa sekta ya utalii
kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni wanatarajiwa kukutana jijini Arusha
katika Mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO) Kamisheni ya Afrika
unaotarajiwa kufanyika Oktoba 5-7, 2022 jijini Arusha.
Maandalizi ya mkutano huo
wenye kauli mbiu inayosema “Kuujenga Upya Utalii Stahimilivu wa Afrika kwa
Maendeleo Jumuishi ya Kiuchumi na Kijamii” yanafanywa na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza leo katika kikao
cha tatu cha kamati ya kitaifa ya maandalizi ya mkutano huo, Naibu Waziri wa
Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja amesema maandalizi yanaendelea vizuri
huku akiwaelekeza wajumbe wa kamati hiyo kuendelea kufanya kazi vizuri ili
kufanikisha mkutano huo kwa viwango vya juu.
“Ninaamini timu hii ni timu
iliyokamilika hivyo kila mjumbe atumie uwezo wake kufanya kazi vizuri ili
tusimuangushe Mheshimiwa Rais,” Mhe.Masanja amesisitiza.
Naye, Naibu Katibu Mkuu
Wizara ya Maliasili na Utalii, Ndg. Juma Mkomi amesema Wizara itatoa
ushirikiano wa kutosha katika kufanikisha mkutano huo na pia kutatua changamoto
zitakazojitokeza.
Mbali na wawekezaji, mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa UNWTO Ndg. Zurab Pololikashvili, Waziri wa Utalii wa Ivory Coast Ndg. Siandou Fofana na mawaziri wa utalii kutoka nchi wanachama wa UNWTO.
Kwa mujibu wa aya ya 67 ya
Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025, Serikali iliyopo madarakani
inaendelea kuweka mkazo katika kupanua wigo wa bidhaa za utalii ili sekta hiyo
iendelee kuchangia katika pato la Taifa.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja akizungumza na Kamati ya kitaifa ya maandalizi ya Mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO) Kamisheni ya Afrika katika kikao cha tatu kilichofanyika leo jijini Arusha.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja akizungumza na Kamati ya kitaifa ya maandalizi ya Mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO) Kamisheni ya Afrika katika kikao cha tatu kilichofanyika leo jijini Arusha.
No comments:
Post a Comment