Habari za Punde

KONGAMANO LA WANAWAKE WA KIISLAMU LAFANYIKA ZANZIBAR.

Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Mgeni Hassan Juma akizungumza na kulifungua Kongamano la Wanawake wa Kiislam Zanzibar lililofanyika katika ukumbi wa Sheikh.Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Wilaya ya Mjini Unguja Jijini Zanzibar.
Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe.Mgeni Hassan Juma akimkabidhi Cheti Bi.Raya Hamad wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Wanawake wa Kiislam Zanzibar lililofanyika katika ukumbi wa Sheikh.Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Unguja Wilaya ya Mjini Jijini Zanzibar.
Washiriki wa Kongamano la Wanawake wa Kiislam Zanzibar wakifuatalia Mada mbalimbali zilizowasilishwa na watoa mada katika Kongamano la Wanawake wa Kiislam Zanzibar lililofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Wilaya ya Mjini Unguja Jijini Zanzibar.

Na Bahati Habibu    Maelezo  6/10/2022

Wanawake wa Kiislamu Zanzibar wametakiwa kutafuta elimu itakayosaidia kuleta maendeleo na kujenga jamii iliyobora inayofuata misingi na mafundisho ya uislamu alokuja nayo Mtume Muhammad S.W.A.

 

Akizungumza katika kongamano la Wanawake wa kiislamu Zanzibar katika Wiki ya Tamasha la Maulid ya Mtume S.A.W Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe.Mgeni Hassan Juma kwa niaba ya Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi amesema ipo haja kwa wanawake kufuata miongozo ya dini na kuwa mfano bora kwa malezi ya watoto wao na jamii inayowazunguka.

 

Aidha ameitaka jamii kumuandaa mtoto wa kike kwa kumpa elimu itakayomfanya kuwa Mwalimu, mama na  mlezi mzuri kwa watoto wake na kwa jamii kwa ujumla.

 

Mama Mariam, amesema historia ya uislam imemuelezea mwanamke kuwa ni mtu wa mwanzo kuchangia kuenea kwa uislamu na mlezi bora wa familia. 

 

“Mke wa Mtume (SAW) Bibi. Khadija alikuwa mfanya biashara maarufu wakati huohuo alikuwa mama, mke, mlezi na msaidizi wa Mtume kusaidia kuenea kwa dola ya kiislamu duniani.’’ Alisema Mama Mariam Mwinyi.

 

Aidha amesema kongamano hilo limekuja muda muafaka kwani kwa sasa dunia imekuwa ikipiga kelele kwa mwanamke kupewa kipaumbele katika masuala ya uongozi uchumi, siasa  na kushirikishwa katika mabaraza ya kutoa maamuzi.

 

Ameeleza dini ya kiislamu ni dini ambayo imekuja kumuinua mwanamke na  kumpa haki zake katika nyanja mbalimbali ikiwemo kushiriki katika maamuzi na Uongozi kwa kufuata utaratibu unaokubalika katika uislam.

 

Naye mwenyekiti wa kongamano hilo Saida Fereshi amewataka wanawake wa kiislamu kusoma kwa misingi ya kuelewa haki zao sambamba na kuweza kudumisha ndoa zao.

 

Akitaja sababu za kukithiri kwa talaka amesema wanawake wengi wamekosa elimu kuhusu masuala ya ndoa na hivyo kupelekea kuvunjika kwa ndoa hizo na kusababisha watoto kujiingiza katika vikundi viovu kutokana na kukosa malezi ya pande zote mbili.

 

Akitoa shukran Bi Amina Salum Khalfan katika kongamano hilo  ameiomba serikali kuwashirikisha wanawake wakiislamu katika vyombo vya maamuzi ikiwemo baraza la ulamaa na kwenye taasisi za kiislamu.

 

Katika kongamano hilo lililofanyika ukumbi wa Sheikh Idrisaa Abdulwakil kikwajuni Mjini Unguja, mada mbalimbali zilitolewa ikiwa ni pamoja na mada ya Ndoa iliyowasilishwa na sheikh Izudin Alawy kutoka Mombasa Nchini Kenya na “jinsi Uislam ulivyomtukuza Manamke” kutoka kwa Sheikh Abdallah Hamid kutoka Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.