SERIKALI ya
Mapinduzi ya Zanzibar imesema inaongeza jitihada za kukiendeleza Chuo Kikuu cha
Taifa cha Zanzibar (SUZA), kuwa chuo bora zaidi katika kuwaandaa vijana wenye umahiri
na weledi kitaaluma na ubunifu wa kuzitambua fursa na kuzitumia ipasavyo.
Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ambae ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha
Taifa cha Zanzibar (SUZA), Dkt. Hussein Ali Mwinyi aliyasema hayo kwenye mahafali
ya 18 ya chuo hicho yaliyofanyika katika ukumbi wa Dkt. Ali Mohamed Shein Tunguu, Mkoa
wa kusini Unguja, leo Disemba 28, 2022.
Dkt.
Mwinyi alisema kuongezeka kwa idadi kubwa ya wahitimu waliofaulu masomo ya fani
mbalimbali chuoni hapo ni hatua za maendeleo zilizofikiwa na chuo hicho.
Alisema
kwa mwaka huu 2022 idadi ya wahitimu
imeongezeka kufikia 1913 ikilinganioshwa na 1894 waliohitimu mwaka jana hatua
aliyoipongeza kwa tasisi ya elimu ya juu SUZA kwa mafanikio ya kuzalisha wasomi
wa fani mbalimbali ambazo alizitaja kuwa ni nguvu kazi na chachu ya kusukuma
mbele maendeleo ya Zanzibar.
Wakati
huo huo, Dkt. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwapongeza wahitimu kwa hatua
waliyofikia sambamba na kuwasahauri kuitumia vyema elimu waliyoipata hapo kwa
munufaa yao na taifa kwa ujumla.
“Nachukua
fursa hii kukupongezeni kwa mafanikio hayo ya kitaalima ambayo chuo chetu kinaendelea kuyapata” alipongeza Dkt.
Mwinnyi.
Akizungumzia
suala la ushirikiano baina ya Chuo Kikuu cha taifa cha Zanzibar (SUZA) taasisi
nyengine za elimu ya juu za ndani na nje, ikiwemo Wizara ya Elimu na Mafunzo ya
Amali pamoja na wadau wengine wa Elimu, Dkt. Mwinyi alieleza hatua hiyo
itafanikisha azma ya kuleta mageuzi katika sekta ya elimu kuanzia elimu ya
awali hadi elimu ya juu.
“Tutoe
wahitimu wenye uwezo wa kuhimili ushindani uliopo kwenye soko la ajira kwa kutumia elimu walioyoipata” alisema Dkt.
Mwinyi.
Aidha,
alikishauri chuo hicho kuzipatia ufumbuzi wa haraka changamoto zinazopitia ili
kutekeleza majukumu yake ipasavyo.
Hata
hivyo, Dkt. Mwinyi alieleza kuwa serikali inaendelea kuunga mkono jitihada
zinazochukuliwa na chuo hicho kwa kuwapatia misaada ya hali na mali kwa kadri
hali inavyoruhusu.
“Hata
hivyo, bado naendelea kusisitiza haja ya kutafuta njia mbadala za kupata fedha
ikiwemo kuchukua mikopo na kuanzisha miradi ya maendeleo itakayoleta faida kwa
chuo” alieleza Dkt. Mwinyi.
Kuhusu
suala la uhaba wa rasilimali watu unaokikabili chuo hivyo, Rais Dkt. Mwinyi alieleza
haja ya serikali kuajiri watumishi ili kuongeza nguvu katika taasisi za elimu
za elimu ya juu wakiwemo wahadhiri, wakutubi na wataalamu wa maabara na
watumishi wa fani ili kukidhi viwango vya ubora wa elimu ya juu nchini sambamba
na kuimarisha mazingira bora ya kufanyia kazi.
Akizungumza
kwenye Mahafali hayo, Waziri wa Elimu na
Mafunzo ya Amali, Lela Mohamed Mussa, alisema juhudi za serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar ni kutoa vijana wasomi watakaokuwa na uwezo wa kujiajiri
na kuzikimbilia fursa ili kupunguza msongo mkubwa kwa seikali na wazazi.
Alisema
jitihada za Chuo Kikuu cha taifa SUZA ni kuzaliwa wasomi watakaochochea
maendeleo chanya nchini.
Nae Makamu
mkuu wa chuo hicho Prof. Moh’d Makame Haji alisema chuo kinampango wa kujenga
jengo la sayansi ya bahari lenye nia ya kuendeleza dhana ya Uchumi wa Bluu nchini
ambalo alilieleza kwamba fedha zake tayari zimeidhinishwa na serikali.
Imetayarishwa na Idara ya Mawasiliano
Ikulu Zanzibar.
No comments:
Post a Comment