Habari za Punde

MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR- KUFUNGUA MAFUNZO YA WAKANDARASI - NYAMANZI

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akipokea maelezo kutoka kwa Meneja wa Uhusiano wa Shirika la Bandari Zanzibar Ndugu Hassan Juma Amour alipotembelea mabanda ya Maonesho kabla ya Ufunguzi wa Mafunzo ya Kuwaendeleza wataalamu wa Usanifu, Uhandisi na Wakadiriaji Majengo Tanzania iliyofanyika katika Viwanja vya Maonesho Nyamanzi Wilaya ya Magharibi "B" Unguja.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zitaendelea kuweka mazingira mazuri kwa kuziimarisha Taasisi za Ujenzi ili kuhakikisha wataalamu wazawa wanakuza taaluma zao na kushiriki kikamilifu katika Ujenzi wa Miradi  inayojengwa na Watanzania.

Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla katika ufunguzi wa  mafunzo ya kuwaendeleza wataalamu wa Usanifu, Uhandisi na Wakadiriaji Majengo Tanzania hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Viwanja vya Maonesho Nyamanzi Wilaya ya Magharibi “B” Unguja.

Amesema kuwa Serikali zote mbili zimetoa kipaombele kwa wataalamu wa Ujenzi na Makampuni ya ndani ya nchi kupitia Wizara na Taasisi ambazo zimefanya jitihada maalum za kuweka Sera, Sheria na kanuni zenye vigezo rafiki ili kurahisisha maombi ya kazi za ujenzi hapa nchini.

Mhe. Hemed amewataka washiriki wa mafunzo hayo kuitumia vyema nafasi waliyoipata ili kuweza kupata uwelewa mkubwa  na mbinu mbali mbali za ujenzi ikiwemo utumiaji wa njia mbadala ya vyuma hasa Zanzibar ambapo kumekuwa na uhaba  mkubwa wa matumizi mali zisizorejesheka kama vile mchanga  na nyenginezo.

Aidha Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema matumaini makubwa ya Serikali kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuonesha mbinu za kuhifadhi, kuitunza na  kuiendeleza miji ya urithi ambayo inachangia kuongeza pato la Taifa kupitia watalii wanaokuja nchini

Sambamba na hayo ametoa wito kwa Makampuni na wataalamu wa Ujenzi kuendelea kuwa waadilifu katika kutekeleza majukumu yao ikiwemo kuzingatia ubora unaohitajika na muda wa mradi uliopangwa ili iweze kutumika kama ilivyokusudiwa na kudumu kwa muda mrefu kwa faida ya vizazi vya sasa na baadae.

Akiwasilisha Taarifa ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiano na Uchukuzi Katibu Mkuu Wizara hio Dkt. Mngereza Mzee Miraji amesema kufanyika kwa mafunzo haya kunatokana na mashirikiano yaliyopo kwa Pande mbili za Muungano kwa lengo la kuhakikisha tunakuwa na wataalamu wabobevu hasa katika masuala ya kutunza na kuboresha Miji ya Urithi wa dunia.

Dkt Mngereza amesema ushirikiano uliopo katika Sekta za Ujenzi kwa Tanzania Bara na Zanzibar Umesaidia kuimarika kwa Miundombinu ya Barabara na kupelekea kuongezeka kwa Kipato Kwa  mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla  pamoja na kuimarika kwa  huduma za kijamii.

Kwa upande wao Wenyeviti wa Bodi ya Usajili wasanifu, wahandisi na wakadiriaji majengo kutoka Zanzibar na Tanzania Bara wamezishauri Serikali kutumia wataalamu wazalendo katika shuhuli za ujenzi ili majengo na Miji ya Urithi iweze kuwa bora zaidi.

Wamesema wakati umefikwa kwa Serikali kuangalia sheria na miongozo katika masuala ya ujenzi ili kupunguza changamoto ya kujengwa kwa majengo yasiokidhi viwango na ubora na kuendelea kulitia hasara Taifa siku hadi siku.







No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.