Habari za Punde

Utalii wa Urithi ni Muhimu Kuendelezwa Zanzibar -Masoud

 

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amesema kwamba, Utalii wa urithi  ni muhimu kuendelezwa Zanzibar kwa kuwa ndio unoangoza katika kuingiza fedha nyingi za kigeni katika nchi na kuchangia kukuza uchumi na ajira kupitia sekta hiyo.

Mhe. Othman ameyasema hayo huko Makunduchi alipozungunza katika shamra shamra za kuelekea kilele cha Tamasha la Kizimkazi baada ya kuyapokea mashindano ya mbio za baiskeli zilizoanzia mjini Unguja hadi Makunduchi na eneo la Kibuteni hadi Koba Makunduchi kwa wanawake na pia watu Wenye Ulemavu yaliyoanzia viwanja vya Mwenge Makunduchi hadi Koba  katika mashindano  yaliyopewa jina la utalii wa michezo.

Aidha mesema kwamba Zanzibar  inaelekea kupiga hatua kubwa  katika sekta na maendeleo ya utalii kutokana na kuwepo utajiri mkubwa wa rasilimali za vivutio vingi vya urithi, lakini urithi huo hauwezi kuwa na  tija kubwa kama inavyotarajiwa iwapo wageni mbali mbali hawatokuja Zanzibar wakaweza kuona alama hizo muhimu za  urithi wa nchi zilizopo  kihistoria.

Amefahamisha kwamba ili kuurithisha kwa vizazi vya sasa urithi huo, ni vyema alama hizo za kihistoria kukumbushwa kwa kutangazwa kupitia  masauala mbali mbali  yanayowakusanya watu pamoja ikiwemo kuandaa matamasha ya aina  tofauti  likiwemo kama la Kizimkazi.

Mhe. Makamu amesema kwamba miaka 100 iliyopita Zanzibar ilikuwa na iadi ndogo sana ya watu na kwa mujibu wa sensa ya mwaka 1910 idadi ya wakaazi ilikuwa ni laki moja na 97 elfu tu, lakini kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022 idadi hiyo imeongezeka mara kumi zaidi  na kwamba mji wa Zanzibar 1910 ulikuwa na idadi ya watu isiyozidi, 36 elfu  na leo iddi hiyo imeongezeka zaidi ya mara 10.

Aidha Mhe . Othman amesema kwamba kwa kipindi cha nyuma idadi ya watu kwa kuwa walikuwa ni wachache urithi wa kihistoria ilikuwa ni rahisi kuupokea na kuurithisha kwa umma kwa kuwa watu walikuwa wachache lakini kutokana na kuongezeka  idadi yao nilazima kutumika mbinu za ziada kuutangaza yakiwemo matamasha ya aina hiyo.

Amefahamisha kwamba tamasha hilo ni muhimu sana katika kurithisha jamii na hasa vijana ili utalii na umaduni  uwe na faidia na tija kubwa zaidi  katika nchi na wenyewe wananchi pia kufahamu kwamba hizo ndio alama  muhimu za wazanzibari.

Kwa upande mwengine Mhe. Othma amesema kwamba dunia hivi sasa imekuwa na wakaazi wa kidunia huku awali wakiwemo wakaazi wa nchi na kwamba wakaazi hao wakidunia nchi na makaazi yao ni katika mitandao ya kijamii kupitia simu za mikoni ambazo ndio vitambulisho vyao vya kuujua na kuishi vyema ulimwenguni.

Amesema kwamba katika kuishi huko ndani ya dunia hiyo watu wanakutana na mambo mbali mbali ya kidunia na pia kukutana na kupata marafiki na washirika wa kidunia kiasi kwamba wanaweza hata kuyasahau yaliyopo katika nchi yao.

Hivyo  muheshimiwa makamu amesema kwamba  matamasha kama hayo nimuhimu sana kuendelezwa kwa juhudi kubwa kwani yatasaidia sana kukumbusha urithi uliopo na mambo mengine yanahusiana na masuala ya urithi na utamaduni nchini.

Amefahamisha kwamba mkoa huo wa kusini pia unamambo mengi ya urithi likiwemo suala la tawala za jadi  ambalo hata watawala waliokuja wakati huo mwaka 1929 waliweza kuandika kitabu cha utamaduni wa watu wa Zanzibar na kuyafafanua mambo ya kiutamaduni yaliyopo Zanzibar kwa urefu sana na kwamba mengi ya mambo hayo tayari yamesahauliwa na wazanzibari wenyewe.

Hivyo ,amewashauri waandaaji wa tamasha hilo kuyakumbusha mambo mbali mbali ya kiutamaduni ili kurejesha utamaduni wa kuwa na kumbukumbu  za urithi ikiwemo tamasha hilo kuingiza kipengele cha wamalenga ambao ni watunzi walioijua Zanzibar na kupitia tungo zao walieleza ustaarabu wa wazanzibari na mambo mengine mbali mbali ambayo hivi sasa yameanza kusahaulika na wazanzibari wenyewe.

Pia ameshauri kwamba ni vyema katika tamasha hilo kuweka siku maalumu ya wamalenga ili kusaidia kukuza na kuvilea vipaji mbali mbali vilivyopo vijana na  kuonesha umahiri wa lugha ambao unaweza kusaidia kutunza na kuhifadhi utamaduni wa wazanzibari ambao ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi.

Kwa upande wake waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Mudrik Ramadhani Soraga, amesema kwamba tamasha hilo ni fursa maalum kwa watu wa kusini kufungua zaidi sekta ya utalii ambapo pia tamasha limetumika katika kutoa mafunzo kwa makundi mbali mbali yakiwemo wajariamali, wakulima, wafugaji  na wasanii ambapo baadae mafunzo hay0o waliyoyapata yatatumika kupima mafanikio katika mabadiliko ya kiuchumi kwa kila sekta iliyohusishwa.

Amesema kwamba ukuaji wa sekata hiyo ni muhimu katika kutoa fursa za ajira kwa vijana wa Zanzibar na kusaidia kupanua wigo zaidi kwa kufungua fursa pana na kwamba jitihada zinafanyika kupitia wizara hiyo kuvifungua vivutio vingi vya utalii wa asili vilivyopo  Zanzibar ili viweze kuleta manufaa zaidi kwa wazanzibari.

Amesema kwamba pia jitihada hizo zinalenga kuifanya Zanzibar kuwa kituo  muhim u cha utalii afrika na kwengineko duniani kwamba ili kufanikiwa katika lengo na azma hiyo ni lazima jihudi maalum zielekezwe katika kuhifadhi mazingira ya ili Zanzibar ibaki kuwa kivutio kikubwa cha utalii.

Naye Mwenyekiti wa Tamasha hilo Mahfoudh Said Omar, amesema kwamba tamasha hilo linalenga kushirikisha  makundi mengi zaidi ikiwa ni juhudi za pamoja kukuza sekta mama ya utalii hapa Zanzibar.

Amesema kwamba tamasha hilo  ni la kimaendeleo linalogusa kila aina ya watu ndani nan je ya Zanzibar ikiwa ni pamoja na kutumika fursa hiyo kuibua vipaji vya vijana kutoka maeneo mbali mbali  vitakavyochangia jitihada za pamoja za kupunguza tatizo la ajira nchini.













No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.