Na Benny Mwaipaja, Washington D.C
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, amelishukuru Shirika la Fedha la Kimataifa – IMF kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo yan chi kupitia misaada ya kiufundi na kifedha inayoipatia nchi na kiuchangia maboresho ya sera mbalimbali za kiuchumi na kifedha.
Dkt Natu Mwamba ametoa shukrani hizo Jijini Washington D.C, nchini Marekani, wakati akishiriki katika mjadala ulioandaliwa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuhusu matokeo ya ushirikiano kati ya IMF na Tanzania kupitia usaidizi wa kiufundi (Capacity Development), kando ya Mikutano ya Mwaka ya Shirika hilo na Benki ya Dunia.
Katika Mjadala huo, Dkt. Mwamba, aliishukuru IMF kwa niaba ya Serikali kwa kuimarisha ushirikiano na Tanzania ikiwa ni pamoja na kuipatia msaada wa kitaalam wa kuimarisha maeneo ya kisera (Policy Reform Measures) uliotolewa Januari 2024 na baadae kuwezesha upatikanaji wa fedha kupitia Dirisha la Resilient and Sustainability Facility (RSF) iliyoitengea Serikali jumla ya dola za Marekani milioni 786.2 sawa na takribani Shilingi za Tanzania Trilioni 2.14.
Alisema kuwa IMF imekuwa mshirika wa muhimu katika ushirikiano wa kiuchumi na Tanzania. Likiwemo tukio la mwaka 2020, ambapo IMF iliisaidia Tanzania fedha kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa wa UVIKO-19 maarufu kama FEDHA ZA UVIKO.
Aidha, Dkt. Mwamba alisema kuwa IMF imeendelea kushirikiana na Tanzania katika kufufua na kuimarisha Uchumi baada ya janga hilo la UVIKO-19 kwa kutekeleza programu ya Extended Credit Facility (ECF) ya thamani ya dola za Marekani bilioni 1.1 sawa na takribani Shilingi Trilioni 2.4 ambayo utekelezaji wake upo katika hatua za mwisho.
Aliahidi kuwa Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano kati yake na IMF, ambapo kupitia programu ya RSF, itaendelea kupokea msaada zaidi wa kitaalam kutoka IMF ili kukamilisha utekelezaji wa maboresho ya kisera na kupata fedha za dirisha la RSF kwa ajili ya kutekeleza shughuli au miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi.
Miongoni mwa mabadiliko ya kisera yanayokusudiwa ni pamoja na Kusaidia msukumo katika kujumuisha usimamizi wa mabadiliko ya tabianchi kuwa jukumu la msingi la Wizara ya Fedha, kwa kuingiza athari za mabadiliko ya tabianchi katika bajeti, sera ya kodi, upangaji wa matumizi, na usimamizi wa madeni, na kuendeleza uwezo wa kushughulikia masuala ya kijani na ufadhili wa mabadiliko ya tabianchi.
“Kutengeneza mfumo wa ufuatiliaji, picha za setilaiti ili kufuatilia taarifa zinazohusu Tabianchi, na upangaji wa matumizi bora ya ardhi na mapendekezo ya ujenzi wa miundombinu himilivu, mifumo ya tahadhari ya mapema, kwa ufupi” Alisema Dkt. Mwamba
Aliongeza kuwa utaanzishwa mfumo wa matumizi ya ardhi na mpango wa kijiografia (land-use and geospatial planning framework) ambao unajumuisha hatari zinazohusiana na Tabianchi kuzingatiwa katika sekta zote na kujumuisha ngazi zote za Serikali.
Dkt. Mwamba alisema kuwa Serikali itatengeneza mfumo wa hadhari wa hatari mbalimbali na kuimarisha mfumo wa uratibu wa data miongoni mwa wadau wakuu; na kutengeneza mfumo wa kitaifa wa usimamizi wa rasilimali maji ya chini ya ardhi, na kuangalia taratibu za utozaji wa vibali kulingana na matumizi ya kawaida au ya kibishara.
Mwisho
No comments:
Post a Comment