Habari za Punde

SMT imejitolea kuendeleza mazingira mazuri yatakayowawezesha wanawake wanaweza kustawi katika nyanja zote - Mhe.Pembe

Na Maulid Yussuf WMJJWW. DAR ES SALAAM

Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Riziki Pembe Juma amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imejitolea kuendeleza mazingira mazuri yatakayowawezesha wanawake wanaweza kustawi katika nyanja zote.
Mhe.Riziki ameyasema hayo wakati akifungua  Kongamano la Wanawake Viongozi wa Usafiri wa  Sekta ya Anga pamoja na kuzindua nembo ya Jukwaa la Wanawake katika usafiri wa Anga, hafla lililofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Hyatt Regency,  Jijini Dar es salaam.
Amesmea Serikali inatekeleza Sera zinazolenga kukuza usawa wa kijinsia katika kuhakikisha wanaongeza ufikiaji wa elimu na mafunzo pamoja na kutoa fursa za ushauri huku akiweka imani ya kuwekeza kwa wanawake  kwa maendeleo endelevu ya Taifa.
Aidha Mhe. Riziki amewaomba washikadau wote wa Serikali, Viongozi wa sekta, Taasisi za elimu, na mashirika ya kiraia kushirikiana katika kuunda mfumo wa ikolojia utakaosaidia wanawake katika usafiri wa anga na kushirikiana katika kuona sera, programu, na desturi zinaondoa vikwazo vinavyozuia maendeleo ya wanawake katika sekta hii. 
Aidha amefashamisha kuwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ipo tayari kushirikiana na Jukwaa hilo ili kuona inasimama vyema ambapo  amewaomba kuweka maazimio kupitia kongamano hilo ili kuyawasilisha katika Wizara husika kwa lengo la kupaza sauti zao katika kuona fursa zilizopo zinafikiwa kwa wana anga pamoja na tasnia nyengine.
Hata hivyo Mhe. Riziki amesisitiza mashirikiano ya pamoja katika kupita kuwahamasisha wasichana kusomea masomo  yatakayowajenga kujiunga na sekta hii ya anga, kuwapa moyo na kuwaelezea  umuhimu wao kuwa katika fani na tasnia hii ili kuongeza idadi ya wanawake katika sekta hiyo.
Pia ametoa rai katika kuwashindanisha na kuwapatia zawadi mbalimbali wanafunzi juu ya masuala ya anga kama kielelezo cha kuwapa motisha na kuzidi kuwatia moyo katika fani hiyo.
Mhe. Riziki amewaomba kuendelea kuwawezesha wanawake kuchukua nafasi zao zinazostahili katika sekta mbalimbali zikiwemo Marubani, Wahandisi, Waongoza ndege, Wachora ramani za anga, au Viongozi katika sera na udhibiti.
"Ulimwengu unabadilika, hivyo sekta ya anga nayo pia ni lazima ibadilike". amesisitiza Mhe. Riziki.
Amesema Majukwaa mbalimbali ya wanawake duniani kama hilo la Anga,  yamefanya maamuzi madhubuti kuleta ubunifu na mabadiliko katika nyanja mbalimbali ni muhimu ili sauti za wanawake zisikike katika tasnia hii. 
Hata hivyo ametoa shukurani kwa viongozi wa jukwaa la Wanawa katikq sekta ya Anga, kwa kujitolea kufanya kazi hiyo muhimu na kuwaomba kuendelea kuwainua, kubadilishana ujuzi wao, na kuhamasisha vizazi vijavyo kwa kuunda tasnia mahiri ya usafiri wa anga ambayo inaakisi utofauti na nguvu za Taifa.
Naye Makamo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya usafiri wa Anga Tanzania ndugu Mtumwa Khatib Ameir amesema katika kufikia malengo ya kuleta usawa wa kijinsia ni lazima kuzifuata 4R,  alizozielekeza Mhe Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ikiwa ni pamoja na kuwa na uelewa wa pamoja kwa Me na Ke, kujenga mitazamo bora, pamoja na Kuleta mageuzi.
Kwa upande wake  Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania TCAA bwana Salum Ramadhan Msangi amesema hadi sasa ni asilimia 35.08 ndio wanawake waliopo katika sekta ya anga ambapo wanaume ni asilimia 64.62  ambapo bado ni idadi ndogo sana, hivyo jiatihada za ziada zinahitajika ili kuwaelimisha watoto wa kike kusoma fani za anga.
Kongamano hilo la wanawake viongozi wa usafiri wa Anga ni kongamano la kwanza likiwa na kauli mbiu inayosomeka "kuwawezesha viongozi wajao wa kike katika sekta ya anga".

MWISHO

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.